Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-28 21:02:06    
Mageuzi ya mfumo wa utamaduni yaliyofanyika hivi karibuni nchini China

cri

    Shirika la Maonesho na Utamaduni wa China kwa Nchi za Nje lilianzishwa siku chache zilizopita, kuanzishwa kwa shirika hilo kunamaanisha kuwa mageuzi ya mfumo wa utamaduni nchini China yamepiga hatua nyingine.

    Shirika hilo limeundwa kwa msingi wa Wakala wa Maonesho ya Kimataifa ya Michezo ya Sanaa na Wakala wa Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa. Mawakala hap wawili walikuwa chini ya Wizara ya Utamaduni ya China tangu miaka ya 50 ya karne iliyopita. Kazi za mawakala hao zilikuwa ni kufanya maingiliano ya kiutamaduni na nchi za nje kwa niaba ya serikali, na katika miongo iliyopita mawakala hao walitoa mchango mkubwa katika kustawisha maingiliano ya kiutamaduni na nchi za nje. Mwaka 2003 mawakala hao walifanya maonesho ya michezo ya sanaa na maonesho ya sanaa katika nchi na sehemu 62 kwa watazamaji milioni 16.

    Lakini kutokana na mageuzi yanavyoendelea kwa kina nchini China, mfumo uliopo hauwezi tena kulingana na mfumo wa uchumi unaoendelea, na ushindani wa kimataifa unaozidi kuwa mkali, tofauti kubwa imetokea kati ya maonesho ya nchi za nje yaliyofanywa nchini China na maonesho ya China katika nchi za nje. Kutokana na hali hiyo idara za utamaduni nchini China zilifanya mageuzi ya kiutamaduni, na kuanzisha Shirika la Maonesh na Utamaduni wa China kwa Nchi za Nje. Hii ni hatua kubwa katika mageuzi.

    Waziri wa utamaduni wa China Bw. Sun Jiazheng alisema, kuanzishwa kwa shirika hilo kunamaanisha kuwa uwakala wa maonesho ya sanaa na maonesho ya michezo ya sanaa umemaliza historia yake yenye miaka 50 na kuwa shirika la kibiashara badala ya kuwa chombo cha kiserikali hapo zamani. Shirika hilo limekuwa mfano wa kupeleka mawakala kushiriki katika maonesho ya kiutamaduni kwenye soko. Anasema,

    "Mageuzi hayo ni mfano wa kuigwa kwa idara nyingine za utamaduni, yatasaidia kuunda mashirika ya kushughulikia sanaa tangu kuzalisha hadi kuonesha jukwaani na kufanya maonesho katika nchi za nje."

    Meneja mkuu wa Shirika hilo Bw. Zheng Yu alijawa furaha baada ya mafanikio ya mageuzi hayo, alisema kuwa hii ni hatua ya kwanza, kwani kazi nyingi muhimu zinatusubiri mbele yetu. Kufanya maonesho ya michezo ya sanaa na maonesho ya utamaduni itakuwa ndiyo kazi kubwa kwa msingi huo tutaanzisha kazi nyingi mfululizo za kuendeleza usimamizi wa soko la utamaduni, kuwa wakala wa biashara ya vitu vya sanaa, na biashara ya uchapishaji wa diski za video, biashara za vyombo vya habari na michezo ya televisheni, na litaimarika kwa nguvu kubwa katika mabadiliko ya soko la kimataifa la utamaduni. Sambamba na kazi hizo, pia litabeba jukumu la kueneza utamaduni wa China nje ya nchi na kuingiza utamaduni wa ng'ambo nchini China.

    Bw. Zhang Yu alisema, muhimu ni kuwa mageuzi yatafanywa kwa hisa kwa msingi wa serikali kuwa na hisa za utawala. Anasema,

    "Sisi tutafanya mageuzi kwa hisa, na kutokana na serikali kuwa na hisa za utawala tutapokea wawekezaji ili kuimarisha zaidi utamaduni wetu na biashara yetu na nchi za nje."

    Mwaka 2003 mageuzi hayo yalianza kufanyiwa majaribio katika idara 35 zilizoko katika sehemu 9, idara hizo zinahusika na fani mbalimbali za utamaduni za vyombo vya habari, uchapishaji, maktaba, makumbusho, majumba ya utamaduni, vikundi vya michezo ya sanaa, vituo vya filamu na michezo ya televisheni, uchapaji, usambazaji wa machapisho na mashirika ya kuonesha filamu.

    Mageuzi yametofautisha aina za biashara na huduma za utamaduni. Aina ya huduma ni kwa ajili ya huduma ya utamaduni kwa umma, ambayo fedha zake zinatoka serikalini na pia kuhamasisha jamii kushiriki. Na aina ya biashara inaundwa kwa mashirika ya utamaduni na kufanya biashara kutokana na hali ya soko na mahitaji ya uchumi.

    Waziri wa utamaduni Bw. Sun Jiazheng alisema, lengo la kufanya mageuzi hayo ni kuwahamasisha wasanii katika utunzi, kuimarisha zaidi juhudi za kuendeleza sanaa na kuchochea juhudi zote katika jamii kuendeleza utamaduni. Ili kuendeleza fani ya utamaduni aina hizi mbili zinapaswa kushughulikiwa kwa pamoja, yaani huduma za utamaduni ziende sambamba na biashara ya utamaduni. Anasema,

    "Mageuzi ya utamaduni licha ya kuwa na mageuzi ya kawaida katika idara za biashara pia kuna mageuzi yake maalumu, kwa hiyo ni muhimu kufanya mageuzi hayo ya aina mbili kwa pamoja. Pili ni kustawisha huduma za utamaduni kwa ajili ya umma, moja ni kustawisha mashirika ya utamaduni yenye shughuli za kibiashara."

    Imefahamika kuwa makumbusho, maktaba na idara kama hizo za huduma kwa umma, hivi sasa kwa hatua ya kwanza zimefunguliwa bila kiingilio kwa watoto na hatua kwa hatua zitafunguliwa na kuwa bure kwa watu wote, kwa upande mwingine ni kuzifanyia mageuzi idara zilizopo sasa kuwa mashirika ya kibiashara ya utamaduni, na kuvutia idara zenye umiliki wa aina tofauti kushiriki katika mashirika hayo.

    Shirika lenye hisa la Jumba la Tamthilia ya Watoto mjini Beijing ni jaribio la kwanza katika mageuzi hayo. Hapo awali jumba hilo lilikuwa la Kikundi cha Tamthilia ya Watoto cha Bejing ambacho kilikuwa na wachezaji wengi hodari na kiliwahi kutunga tamthilia nyingi nzuri za watoto. Ili kujipatia maendeleo makubwa, mwezi Januari mwaka huu lilibadilishwa na kuwa shirika la tamthilia ya watoto ambalo vyombo vya habari vina hisa za utawala na idara nyingine pia zinashiriki.

     Hivi sasa shirika hilo limetayarisha tamthilia ya muziki iitwayo "Mazonge". Tamthilia hiyo iligharimu yuan milioni 3 ambayo ni gharama kubwa kuliko gharama za matayarisho ya michezo yote ya zamani. Ni jambo la kufurahisha kwamba shirika moja binafsi limenunua tikti zote za duru la kwanza la maonesho ya tamthilia hiyo kwa yuan milioni 1.15. Hali hii haikuwahi kutokea katika historia ya jumba hilo la tamthilia ya watoto.

    Meneja mkuu wa Jumba la Tamthilia ya Watoto Bibi Wang Ying anasema,

     "Njia ya shirika ni pana. Kuleta michezo ya kuwapendeza watoto ni kazi yetu, huku tukianzisha biashara nyingi mfululizo za mavazi, vyakula na vitabu kwa watoto."

    Mbali na kuanzishwa kwa Shirika la Maonesho na Utamaduni kwa Nchi za Nje, pia Shirika Kuu la Uchapishaji la China lilianzishwa mwezi wa nne mwaka huu.

Idhaa ya Kiswahili 2004-06-28