Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-29 20:14:01    
Barua za wasikilizaji 29/6/2004

cri

    Anasema alhamisi tarehe 3/6/2004 kipindi cha tazama China kilimpa fursa ya kujua kuwa mji wa Shangai una majengo ya kizamani ambayo yamefanyiwa na yanafanyiwa ukarabati na mengine kujengwa upya. Anasema huko Zanzibar, mji mkongwe una nyumba nyingi za kizamani karibu za miaka mia moja.mji huo unaoitwa pia stone town, una nyumba nyingi ambazo zimeshaporomoka na kujegwa majumba mapya. Katika kipindi hiki cha tazama China ameweza kufahamu kuwa kuna majengo marefu ya kisasa ya makazi ya wananchi na majengo ya shughuli mbalimbali pamoja na wafanyabiashara. Anasema kwa sasa atajaribu kukichambua kwa makini zaidi kila kipindi atakacho kisikiliza.

    Tarehe 26 Aprili mwaka huu wa 2004, ni siku ambayo kwa kweli wananchi wa China na Tanzania walikuwa na kila sababu ya kusherehekea ili kuadhimisha kumbukumbu kubwa ya kutimiza miaka 40 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya nchi zetu mbili China na Tanzania. Hili lilikuwa tukio kubwa kabisa la kihistoria. Nchini Tanzania pamoja na pilikapilika hizo pia tarehe 26 April mwaka huu wa 2004 ilikuwa ni siku ya kutimiza mwaka 40 tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuzaliwa kwa taifa la Tanzania.

    Katika siku hiyo watanzania walikuwa na shamra shamra kubwa, ambapo kitaifa sherehe hizo zilifanyika katika uwanja wa amani huko Tanzania-Zanzibar. Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania Benjamin William Mkapa kabla ya kuhutubia umati mkubwa wa watu waliohudhuria sherehe hizo, alipokea heshima kubwa kutoka kwa gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ustadi na ufundi mkubwa kwa ajili ya maadhimisho hayo.

    Rais katika hotuba yake aliwakumbusha wananchi jinsi muundo huo wa muungano ulivyo tangu ulivyoasisiwa na wazee wetu marehemu mwalimu Julius K. Nyerere na sheikh Abeid Amani Karume. Anasema rais wa Tanzania alizungumzia pia umuhimu wa kudumisha umoja, amani na mshikamano katika kuuenzi muungano wa Tanzania.

    Anasema baada ya muungano, ambapo nchi ya China ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kuthibitisha na kuitambua Tanzania, China na Tanzania zimekuwa marafiki wa dhati kwa muda mrefu. Tanzania imenufaika sana na uhusiano huu karibu katika nyanja zote za kisiasa kiuchumi na kiutamaduni. Mnamo tarehe 30 mwezi Aprili mwaka huu wa 2004, siku nne tu baada ya maadhimisho ya miaka 40 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania na pia kuundwa kwa muungano wa Tanzania. Rais Benjamin William Mkapa alilihutubia taifa kwa njia ya redio na televisheni na kuzungumzia mambo mengi mazuri ya kupambana na umaskini katika taifa Tanzania.

    Anakumbusha kuwa rais alitoa mifano mingi mizuri inayowahusu wachina wakiwa ni marafiki wakubwa wa Tanzania. Bwana Kulwa pia anamnukuu Rais Mkapa akisema "Nchi inayoongoza kwa kupunguza umaskini katika miaka 20 iliyopita ni Jamhuri ya Watu wa China na siri yake ni moja tu: uwezo wa kujitosheleza kwa chakula, nidhamu ya kazi, ubunifu na uchumi unaokuwa kwa asilimia 10 kwa mwaka". Mwisho wa kumnukuu.

    Akiendelea kuzungumzia mikakati ya kupambana na umaskini, rais Mkapa wa Tanzania alitoa kielelezo kingine tena kuhusu taifa la China, na amemnukuu tena akisema: "Tusione haya kushirikiana na sekta binafsi, ya ndani na nje, kukuza uchumi na kujenga nchi. Hivi ndivyo rafiki zetu wa kudumu, ambao mwezi huu tumesherehekea miaka 40 ya uhusiano na ushirikiano nao, Jamhuri ya Watu wa China, wanavyofanya" mwisho wa kumnukuu.

    Bwana Kulwa aliye ifuatilia sana hotuba hiyo ya tarehe 30, april 2004, amabyo Rais Mkapa aliitumia China kama mfano mzuri wa kuingwa, anamnukuu tena rais Mkapa akisema: "Nawasihi tushabikie siri ya maendeleo niliyoitaja ya marafiki na wafadhili wetu wakubwa, ndugu zetu wachina yaani uwezo wa kujitosheleza kwa chakula, mipango na nidhamu ya kazi, ubunifu na uchumi unaokuwa. Naomba sote tuwe na upeo mpana, tujitume wenyewe kufanya kazi kwa bidi na maarifa... Kwa mali asili na rasilimali nyingine alizotujalia mwenyezi mungu, tukiamua na kujituma, tukiwa waadilifu na wajasiri mali, bila shaka tutafanikiwa"mwisho wa kunukuu.

    Anasema kwa bahati nzuri yeye ni miongoni mwa watanzania ambao wamewahi kuitembelea China na kujionea kwa macho yake mwenyewe, ukarimu wa ndugu wachina, na jinsi walivyo na juhudi katika kufanya kazi ili kujiletea maendeleo yao wenyewe na kwa nchi marafiki zao ikiwemo Tanzania. Tunawapa hongera sana na pia tunawashukuru sana kwa juhudi, maarifa na misaada yao.

    Anasema tutazidi kuwaenzi na kuwakumbuka waasi wa mataifa yetu mawili hayati Mao Zedong-mwenyekiti wa China, na hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere rais wa kwanza wa Tanzania iliyoungana. Wengine ambao nao hatuwezi kusahau mchango wao kwa mataifa yetu ni hayati Sheikh Abed Amani Karume rais wa kwanza wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi, mwasisi wa sera za mageuzi na ufunguaji mlango wazi kwa nchi za nje marehemu Deng Xiaoping, waziri mkuu wa China Chou En Lai ambaye sasa ni marehemu. Shukrani za pekee ziwaendee rais mstaafu wa kizazi cha tatu wa China ambaye ni mwenyekiti wa kamati na baraza la kijeshi la China Jiang Zemin, na rais wa sasa wa China Hu Jintao ambapo katika enzi za utawala wao wameendelea kujenga na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa nchi zetu mbili China na Tanzania. Anasema anawapongeza viongozi wetu wa nchi zetu hizi mbili!!

    Nikiwa msikilizaji wa kudumu wa Radio China Kimataifa na rafiki wa watu wa China. Ninaombea muungano wa amani katika taifa la China na ninapinga ufarakanishaji wa taifa. Tanzania iwe na umoja na China iwe na umoja na umoja ni nguvu, na uhusiano wetu uendelee kudumu milele na milele. Amina.

Idhaa ya Kiswahili 2004-06-29