Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-29 20:58:55    
MAHOJINO NA WAZIRI WA VIWANDA ZANZIBAR-TANZANIA

cri
    Kwa muda mrefu sasa kumekuwepo kilio kutoka kwa nchi zinazoendeleaa kuhusu kuwepo kwa utaratibu wa biashara ulio wa usawa na haki kwa nchi zote. Mikutano ya shirika la biashara duniani WTO mara kwa mara imekuwa ikizungumzia suala la kuondoa ruzuku kwenye mazao ya kilimo, kitu ambacho nchi za Ulaya na Marekani zimekuwa zikisita. Waziri wa viwanda na biashara wa Zanzibar, Tanzania Mohamed Abood Mohamed anasema:

    Dhana ya kucheza kwenye uwanja mmoja ni ushindani ambao uko sawa kwa ulimwengu, hiyo ni dhana ngumu ,maana  hata Mwalimu huko nyuma alisema unapokuwa na zile ngumi kwenye ulingo kisha ukawachukua wenye uzito mkubwa na uzito mdogo,  ambaye ana uzito mkubwa akimtwanga jamaa ngumi moja tu amemalizika kwa hiyo huwezi kushindanisha watu . Akatoa mfano wa benki yetu ambayo inaitwa NBC (National bank of commerce) , wakati huo huo na City Bank hivi kweli NBC inaweza kufungua ofisi yake New York na ikaweza kujiendesha , lakini ni rahisi sana kwa City Bank kufungua ofisi Dar-es-salaam na ikajiendesha. Kwa hiyo cha msingi ni kwamba si rahisi kushindanisha watu kwa  tofauti za kiuchumi na kiuwezo na bahati mbaya wale ambao wana uwezo mkubwa kiuchumi na kisiasa na nguvu wanasahau kwamba na wao walikuwa huko chini hawako tayari kuwasaidia wenzao kama walivyosaidiwa wao wakati wakianza mchakato ule ,sasa hilo ndio tatizo kubwa linalijitokeza kutaka tukashindane kwa wakati mmoja wakati nguvu si sawa, sasa sisi tunachowaambia kwamba wasaidie kujenga nguvu na uwezo, ili tujue kushindana vizuri hapo ni wajibu wao kusaidia kwa sababu mafanikio yao na rasmali zetu nyingi huko nyuma wakati wakitutawala ndiyo zilisababisha wao wakafika ambako sasa wamefika. Wametumia nguvu sana za Afrika na nchi nyingine maskini ulimwenguni huko nyuma kwa nchi ndogo ndogo hawa wakubwa wa leo kwa kupata masilahi ambayo sasa wanayo. Sasa wao nguvu zile hawako tayari kuzirudisha kwetu ili tuweze kufikia kushindana .Jambo dogo linawasumbua hili la fidia kwenye bidhaa za kilimo na wanaendelea kutoa fidia kwenye bidhaa hizo, na hili ni tatizo sana kiuchumi. kwa sababu wao wana uwezo wa kufidia wakati sisi hatuna uwezo wa kufidia kwa maana ya(ruzuku) lakini sisi kwa sababu hiyo wao wanazungumzia kisiasa sisi tunawauwa watu wetu kama hawapati nafasi ya kushindana katika soko. Kwa hiyo jambo dogo hilo kwao limekuwa gumu na wao wanatulazimisha sisi mambo mengi ya kufanya kwetu. Kwa hiyo cha msingi lazima wakubwa waelewe matatizo tuliyo nayo sisi na lazima waunge nguvu za kweli na wakubaliane na mashariti ya pamoja ndiyo tuweze kufanya biashara iliyo sawa ulimwenguni, lazima watupe muda wa kutosha na mwaka 2008 ni muda mfupi sana lazima muda uongezwe ili tupate muda zaidi tujifunze ili tuufikie huo uwezo wa kushindana kwa pamoja. Sasa wakati mwingine inapotokea kwamba hushushi bei pengine zile gharama zako za maendesho zinapokuwa ni kubwa  huwezi kushusha zaidi ya hapo.

    Pamoja na matatizo hayo ambayo nchi zinazoendelea zinakumbana nayo, bado zina nia thabiti ya kuendeleza uchumi wa nchi hizo, ili ziweze kushiriki kikamilifu kwenye biashara za kimataifa. Bwana Ahmed anasema:

    Tutajitahidi kujenga mazingira na moja kati ya tunayofanya sasa ni kutafuta njia ya kupunguza gharama za uzalishaji kwenye maeneo mbalimbali ili tuweze kutoa bidhaa ambazo zitakuwa na ushindani mzuri kwenye soko na vile vile tunajifunza hii tabia ya uthibiti wa viwango ili kutoa bidhaa zenye ubora kwa sababu unapotoa bidhaa zenye ubora na zenye bei nzuri , itasaidia kununulika katika soko kwenye ushindani wa soko la leo, na kama nilivyosema , tunataka tutumie zile rasimali za ndani kwa msingi ili zituwezeshe kuingia vizuri katika soko, kwa sababu ukiagiza mali ghafi kutoka nje halafu uje utengeneze kwako sio rahisi kushindana na aliye kuuzia mali ghafi kwa sababu zimetoka kwake kwa hiyo anapozalisha yeye kitu chake kitakuwa cha nafuu zaidi.Kwa hiyo sisi tunajipa matumaini kuona kwamba tutizame zile bidhaa zetu zilizoko ndani ili tuzitumie hizo katika kuzifanya kuwa na mwisho uliokamilika, halafu tuweze kuingiza katika soko kwa hiyo tunachukuwa ushauri tujitahidi kupunguza lakini sasa inategemea na mauzo ya bidhaa kwasababu kuna maswala ya umeme,maji na usafirishaji wa bidhaa pamoja na kodi, inategemea hali halisi jinsi nchi ilivyo, lakini tunachukuwa hatua mbalimbali za kufikiria katika suala ambalo ni gumu na lina ushindani mkubwa ni swala la umeme ,kwa hiyo hata wenzetu wachina waliokuwa na uzoefu kwenye hili jambo tunawakaribisha waje waangalie kwasababu tuko tayari kuzungumza nao ni namna gani wanaweza kuwekeza kwenye masuala haya hasa ya nishati. Ijapokuwa sasa hivi mambo haya yako chini ya serikali lakini tunapoona yupo mtu anaweza kutupatia unafuu mkubwa kwanini tusizungumze naye tukaangalia sababu moja katika kitu ambacho kitaweza kutupeleka kwenye ushindani wa biashara hii lakini ni suala zima la kuwa na umeme kwa bei nafuu. Kwa sababu hawa wazalishaji wataweza kushindana na mzalishaji mwingine.Ingekuwa mahala pengine bei ya umeme iko chini katika jumuiya ya Afrika mashariki mathalani Kenya bei zao za umeme ziko chini si rahisi mimi niliye Mtanzania bei zetu ziko juu nikaanza kubiashana nao.Sasa mwelekeo ni namna gani tutafanya kupunguza gharama hizi za uzalishaji ili tuwe na bidhaa zitakazoweza kuingia katika ushindani lakini pia bidhaa nzuri.Hivyo jambo kubwa ni hili alilosema waziri kiongozi TAALUMA.

    Hata hivyo mafanikio yameanza kuonekana. Siku za karibuni shirika la biashara la kimataifa WTO lilitamka wazi kuwa ruzuku inayotolewa na Marekani kwa wakulima wa pamba si halali, na kukubaliana na malalamiko ya Brazil. Nchi zinazoendelea zimeanza kupata ushindi katika mazungumzo ya biashara. Hakika hali nzuri zaidi itaonekana katika siku za badaye. Hii bilashaka itasaidia maendeleo ya uchumi wa nchi zinazoendelea.

Idhaa ya Kiswahili 2004-06-29