Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-02 21:29:11    
Mawasiliano ya utamaduni yahimiza ushirikiano kati ya China na Afrika

cri
    Siku ya sanaa ya "Beijing na Afrika" iliyoendeshwa na Wizara ya utamaduni ya China ilifanyika tarehe 30, Aprili hadi 23, Mei nchini China. Wasanii kutoka nchi 9 za Afrika Misri, Ethiopia, Botswana, Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, Kenya, Mauritius, Nigeria, Afrika ya Kusini na Tanzania waliwaburudisha watazamaji wa Beijing kwa maonesho yao mazuri. Wakati huo huo, maonesho ya sanaa na kazi za mikono, uchoraji na picha yalifanyika katika makumbusho ya sanaa hapa Beijing. Aidha, ujumbe wa utamaduni wa serikali ya nchi 7 za Afrika zikiwemo Botswana, Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, Kenya, Mauritius, Msumbiji, Nigeria na Tanzania pia ulishiriki kwenye maonesho hayo ya Beijing na kutembelea mkoa wa Hu Nan, China. Hili ni siku kubwa kwa sanaa ya Afrika na urafiki kati ya China na Afrika. Limeweka rekodi mpya katika historia ya mawasiliano ya utamaduni kati ya China na Afrika, na kutoa fursa nzuri kwa watazamaji wa China kufahamu na kuburudika na sanaa ya Afrika.

    Mawasiliano ya utamaduni kati ya nchi mbalimbali ni kama daraja la urafiki, na yanazidisha uelewano na ushirikiano kati ya nchi hizo. Waziri mkuu wa zamani wa China Bw. Zhou Enlai alifananisha mambo ya kidiplomasia, uchumi na utamaduni na ndege. Aliona kuwa, mambo ya kidiplomasia ni kama kiongo ndege, uchumi na utamaduni ni kama mabawa yake. Kufananisha huko kunaonesha mchango muhimu wa mawasiliano ya utamaduni na ushirikiano katika mambo ya kidiplomasia ya taifa.

    Serikali ya China siku zote inazingatia sana kuendeleza uhusiano wa utamaduni na nchi za Afrika. Mawasiliano na ushirikiano wa utamaduni unatoa mchango mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa kirafiki na ushirikiano, kuanzisha ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Afrika katika karne mpya na uelewano kati ya serikali na wananchi wa China na nchi za Afrika. Mawasiliano ya utamaduni kati ya China na Afrika yalianzishwa mwaka 1955. China na Misri zilitia saini kanuni ya mkutano wa ushirikiano wa utamaduni kati ya China na Misri mwezi Mei, mwaka huu. Mpaka sasa China imetiliana saini makubaliano ya utamaduni na serikali za nchi 46 barani Afrika, na kuweka mipango ya utekelezaji kutokana na makubaliano hayo. Wizara za utamaduni za China na nchi za Afrika zimefanya kazi nyingi zenye mafanikio chini ya makubaliano na mipango hiyo kwa muda mrefu uliopita.

    Kutokana na takwimu zisizokamilika, China na nchi za Afrika zilipelekeana wajumbe 200 wa utamaduni wa serikali, na kufanya kazi muhimu katika kuhimiza uhusiano wa utamaduni kati ya pande hizo mbili. Kutokana na vitendo hivyo, China na nchi za Afrika zimepelekeana ujumbe mia kadhaa, wakati maelfu ya wasanii wa ujumbe wa utamaduni kati ya China na Afrika walitembeleana katika nusu-karne iliyopita. Wasanii wa China na Afrika wanakaribishwa sana na watazamaji wa nchi hizo kwa uzuri wao wa kipekee na mitindo maalum ya kitaifa, na kupata sifa kubwa kutoka kwa wananchi wa nchi hizo. Jumla ya maonesho yapatayo 100 yalifanyika nchini China na barani Afrika, na kufahamisha matokeo ya sanaa za kisasa za nchi zao, kama vile uchongaji, uchoraji, na sanaa na kazi za mikono katika nchi mbalimbali za Afrika. wakati huo huo, maonesho ya sanaa ya nchi nyingi za Afrika pia yalifanyika nchini China. Pia kutokana na makubaliano ya mawasiliano ya utamaduni, pande hizo mbili zilianzisha shughuli mbalimbali kama vile siku ya utamaduni, wiki ya filamu na maonesho ya vitabu, ili kuhimiza mawasiliano na maelewano kati ya wananchi wa China na Afrika.

    Mkutano wa kwanza wa mawaziri wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ulifanyika mwezi Oktoba, mwaka 2000, hapa Beijing. Hii ilimaanisha kuanzishwa kwa utaratibu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, na kutia uhai mpya kwa ushirikiano wa pande zote kwenye sekta ya utamaduni kati ya pande hizo mbili katika karne mpya. Katika miaka mitatu iliyopita, China ilipeleka vikundi 41 vya utamaduni kwa nchi za Afrika, na kupokea vikundi 52 vya utamaduni barani Afrika. Kutokana na mipango ya mkutano wa pili wa mawaziri wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, wizara ya utamaduni itafanya harakati za "utamaduni wa China barani Afrika" mwaka huu, wakati huo, China itapeleka vikundi 3 vya wasanii kutembelea nchi 12 barani Afrika. Hivi sasa, uhusiano wa kisiasa kati ya China na Afrika ni mzuri, na ushirikiano wa kiuchumi na biashara unapata maendeleo makubwa. Mafanikio hayo yanapatikana kutokana na msingi wa ushirikiano wa utamaduni kati ya pande hizo mbili wa muda mrefu uliopita.

Idhaa ya Kiswahili 2004-07-02