Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-13 18:24:45    
China kuwa na mazingira ya uchumi wa masoko

cri

    Pamoja na ongezeko la matukio kuhusu bidhaa za China kuchukuliwa hatua na nchi za nje za kupinga bei za Chini zinazouzwa bidhaa hizo, suala la hadhi ya uchumi wa masoko ya China linafuatiliwa na watu wa sekta mbalimbali za nchini. Baadhi ya wanauchumi na maofisa wanaona kuwa hivi sasa China imekuwa na mazingira ya kuwa nchi yenye uchumi wa masoko, lakini inapaswa kuongeza juhudi zaidi kuifanya hadhi ya uchumi wake wa masoko itambuliwe mapema zaidi na nchi mbalimbali duniani, ili kuleta mazingira ya haki na mwafaka ya biashara ya kimataifa kwa viwanda na kampuni zake.

    Katikati ya mwezi Juni mwaka huu, wizara ya biashara ya Marekani ilitangaza matokeo ya mwanzo ya kesi moja ya kupinga uuzaji wa bidhaa kwa bei ya chini sana, ambayo samani kutoka China zitatozwa ushuru wa poromoko la bidhaa kati ya 4.9% na 198%. Hiyo ni moja kati ya kesi kubwa zaidi ya 100 kuhusu Marekani kupinga poromoko la bidhaa za China, ambayo thamani ya bidhaa zinazohusika imefikia dola za kimarekani bilioni 1.2.

    Kuhusu hukumu hiyo, mratibu wa jumuiya ya kampuni za samani nchini China Bw. Jia Qingwen alisema,

    "Naona hukumu hiyo sio ya haki. Sekta ya samani ya China ni ya soko huria kabisa, tena 70% ya samani zilizosafirishwa kwenda nchini Marekani kutoka China, ni zile zinazotengenezwa na viwanda vya ubia kati ya China na nchi za nje, hivyo tunasema kuwa usafirishaji bidhaa wetu ni wa kuambatana na kanuni za uchumi wa masoko. Hatukubaliani na uamuzi wa wizara ya biashara ya Marekani wa kuthibitisha gharama za bidhaa za China kwa kuzilinganisha na zile za nchi nyingine ya tatu."

    Maneno aliyoyasema kuhusu "uthibitishaji wa gharama za bidhaa za China kwa kuzilinganisha na zile za nchi nyingine ya tatu" ni kuwa Marekani hivi sasa bado inaichukulia China kuwa nchi yenye uchumi usio wa masoko. Hivyo ilipofanya uchunguzi wa kupinga poromoko la bei kwa bidhaa za China, mara kwa mara inapiga hesabu kuhusu gharama za bidhaa za China ikilinganisha na zile za aina hiyo za nchi ya tatu, zikiwemo za Korea ya kusini na Singapore. Lakini gharama ya nguvukazi ya nchi hizo ni kubwa kuliko ya China, hivyo ni rahisi kuzichukulia hatua bidhaa za China kwa hoja ya kuuzwa kwa bei ya chini kupita kiasi ikilinganishwa na uzalishaji wa bidhaa za aina hiyo.

    Habari zinasema kuwa hivi sasa China ni nchi ya kwanza ambayo bidhaa zake zilizosafirishwa nchi za nje, mara kwa mara kuchukuliwa hatua za kutozwa zaidi ushuru wa poromoko la bidhaa. Hadi mwaka jana, zaidi ya nchi 30 ambazo zilifanya uchunguzi zaidi ya 500 kuhusu bidhaa zaidi ya aina 4,000 zilizosafirishwa huko kutoka China, na kuiathiri biashara ya nje ya China kwa dola za kimarekani zaidi ya milioni 1.6.

    Baadhi ya wanauchumi na maofisa wa China wamesema kuwa Marekani na Umoja wa Ulaya haziichukulii China kuwa ni nchi yenye uchumi wa masoko na kuzichukulia hatua za kupinga poromoko la bidhaa mara kwa mara, vitendo hivyo si vya haki na haviambatani na hali halisi ya maendeleo ya uchumi wa China ya hivi sasa.

    Kigezo kinachotumiwa na nchi za Ulaya, Marekani na Canada ni kuhusu pande tano ambazo ni pamoja na rasilimali kupatikana kutokana na serikali au masoko; viwanda na makampuni yanaweza kujiamulia mambo yake au la; gharama za mali ghafi zilizotumika ni kutokana na masoko au la; mambo ya fedha yanafuatana na kanuni za uchumi wa masoko au la; na mazingira ya biashara ni ya haki au la.

    Profesa Li Xiaoxi ambaye ni kiongozi wa taasisi ya utafiti wa usimamizi wa uchumi na rasilimali ya chuo kikuu cha ualimu cha Beijing anaona kuwa hivi sasa China imeshatimiza masharti ya kuwa nchi yenye uchumi wa masoko. Alisema,

    "Kutokana na mageuzi yaliyofanywa katika miaka mingi iliyopita, hata kama mambo yetu mengi hayajaweza kufikia viwango vya Marekani na nchi za Ulaya, lakini kwa kawaida, China imefikia kiwango cha msingi wa nchi yenye uchumi wa masoko."

    Profesa Li alisema kuwa kutokana na vigezo vya Marekani na Ulaya, hivi sasa uendeshaji wa shughuli za serikali, viwanda na kampuni, bei za bidhaa masokoni, utaratibu wa mambo ya fedha, mazingira ya biashara na ujenzi wa utaratibu wa sheria, zimetimiza masharti ya kuwa nchi yenye uchumi wa masoko.

    Habari zinasema kuwa hadhi ya hivi sasa ya China ya uchumi usio wa masoko, imefanya viwanda na kampuni nyingi kutotendewa haki katika biashara na nchi za nje. Hivyo, ili kufanya hadhi ya uchumi wa China kuwa wa masoko inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa, tokea mwaka huu, serikali ya China, mashirika ya wakala na viwanda vimeimarisha mawasiliano na nchi zinazohusika.

    Waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai hivi karibuni alipokuwa na mazungumzo na waziri wa biashara wa Marekani Bw. Donald Evans alisema,

    "Tutawaambia wanauchumi na wanaviwanda wa Marekani, wafahamu kuwa mfumo wa uchumi wa masoko wa China umepata maendeleo makubwa, na kuwa na nguvu kubwa katika shughuli za kiuchumi, ama sivyo hautaweza kuwa na ongezeko la 1000% katika miaka 25 iliyopita, na kuleta miujiza duniani."

    Habari zinasema kuwa hivi sasa duniani kuna nchi za New Zealand, Singapore, Malaysia na Thailand zimetambua hadhi ya uchumi wa China kuwa ni wa masoko.

    Mtaalamu wa uchumi wa China Bw. Li Xiaoxi alisema kuwa pamoja na ongezeko la biashara ya nje ya China, hususan biashara ya uingizaji bidhaa kutoka nchi za nje, kupata hadhi ya uchumi wa masoko kwa China, kutanufaisha China na nchi nyingine kwa pamoja.

Idhaa ya Kiswahili 2004-07-13