Ripoti mpya kabisa iliyotolewa jana huko Bangkok nchini Thailand na mashirika mbalimbali ya kimataifa, yakiwemo Shirika la watoto la Umoja wa mataifa UNICEF, Shirika la Mpango wa Ukimwi la umoja wa Mataifa UNAIDS, na Shirika la misaada la Marekani USAID, imebainisha kuwa, ukanda wa kusini mwa Sahara utakuwa na takribani yatima milioni 50 huku zaidi ya robo tatu ya hao wakiwa wamepoteza mzazi mmoja au wote kutokana na ugonjwa wa ukimwi.
Ripoti hiyo ilitolewa kwa pamoja na Dr.Anne Pertson msaidizi wa masuala ya afya katika shirika la USAID, Bi Carol Bellemy, mkurugenzi mtendaji wa UNICEF na Dk. Peter Piot, mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa maonyesho wa Impact huko Bangkok nchini Thailand unakofanyika mkutano wa 15 wa dunia kuhusu ugonjwa wa ukimwi.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na mtaalamu wa maswala ya utafiti kutoka shirika la Futures Group International Bw. John Stover. Ikipewa jina la: "Watoto Hatarini 2004" ripoti hiyo inatoa takwimu mpya kabisa zikionyesha jinsi idadi ya watoto yatima waliopo chini ya miaka 18 inavyoendelea kuongezeka katika vipindi tofauti kutokana na janga la ugonjwa wa ukimwi.
Kwa kipindi kifupi tu cha kati ya mwaka 2003, idadi ya watoto yatima duniani kote imeongezeka kutoka milioni 11.5 hadi milioni 15 wengi wao wanatoka Afrika.
"Sehemu nyingi katika eneo la kusini mwa Sahara zinaendelea kuona watoto yatima wakiongezeka kila siku kutokana na ugonjwa huu." Alisema Bi Bellemy wakati wa kutoa ripoti hiyo na kuongeza: "ili kuwasaidia watoto waendelee kufurahia maisha, ni vema wazazi wao waendelee kuishi wakiwa na afya njema, watoto wapatiwe elimu nzuri na wawekewe sheria zinazowalinda kutoka katika uzalilishwaji wanaofanyiwa na watu wakubwa."
Kutokana na ripoti hiyo, robo tatu ya wagonjwa wote wa ukimwi duniani, wanatoka wanatoka katika ukanda wa kusini mwa Sahara huku uwiano wa watoto yatima kutokana na ugonjwa huukiwa umepanda kutoka asilimia 28 mwaka 2003.
Tangu mwaka 2000, takribani watoto milioni 3.3 wamepoteza wazazi wao kwa ugonjwa huu. Na ifikapo mwaka 2010 inakadiriwa idadi hiyo itakuwa imepanda hadi kufikia milioni 18.4
"Ripoti hii inaeleza bayana umuhimu wa kuwatunza haraka watoto walioathiriwa na ukimwi,"alisema Dk. Peterson kutoka, shirika la misaada la Marekani la USAID, kisha akaongeza kuwa: "Ndio maana Rais Bush ametoa umuhimu kwa kuwajali watoto na huduma muhimu zinazoambatana na kuahidi kiasi cha dola za kimarekani bilioni 15 kupitia mfuko wake wa PEPFAR.
Katika nchi za ukanda huo, nchi 11 kati ya 43, zaidi ya mtoto mmoja kati ya saba ni yatima na chanzo cha zaidi ya asilimia 50 ya vifo.
"Ili kuepuka kuendelea kuwa na mamilioni ya watoto yatima kutokana na ukimwi, mataifa yote duniani yanapaswa kufanya kila liwezekanalo kuzuia raia wake wasiambukizwe ukimwi." Alisema Dk. Piot wa UNAIDS.
Idhaa ya Kiswahili 2004-07-14
|