Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-15 18:21:03    
Mmarekani Anayeendesha Baa ya Pombe mjini Tianjin

cri

    Tianjin ni mji wa pwani ulioko kaskazini mwa China. Katika mtaa wa Youyi mjini humo, zimekusanyika baa 30 hivi za aina mbalimbali za pombe. Kati ya baa hizo, baa iitwayo The British Heaven Bar inawavutia zaidi wateja wanaotoka nchi mbalimbali. Baada ya kufunguliwa kwa mwezi mmoja tu baa hiyo ilianza kupata faida. Meneja mkuu wa baa hiyo ni mmarekani anayeitwa Chris Hagen, jina lake la kichina ni Mi Kaifeng.

    Alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alijijulisha kwa Kichina kizuri kuwa: "Mimi naitwa Mi Kaifeng, jina hilo nilipewa na mwalimu wangu wa kichina. Mara ya kwanza nilikuja China mwaka 1986 nilipokuwa na umri wa miaka 13 tu, wakati ule mimi sikujua chochote kuhusu China."

    Chris Hagen alizaliwa katika Jimbo la Califonia, nchini Marekani. Mwaka 1986 alifika mjini Tianjin akifuatana na baba yake aliyekuwa akifanya biashara huko Tianjin. Alikaa mjini Tianjin kwa miaka 5 na kusoma katika shule ya kimataifa ya Tianjin. Mwaka 1991 alirudi Marekani na kufanya kazi huko baada ya kuhitimu chuo kikuu.

    Mwaka 1997, kutokana na ushauri wa baba yake, Chris alirudi Tianjin kwa mara ya pili. Alipowasili Tianjin, mara alishangazwa sana na mabadiliko makubwa yaliyotokea katika miaka 6 iliyopita mjini humo. Hivyo kutokana na kushawishiwa na kuungwa mkono wa baba yake, Chris aliamua kuja China kuwekeza vitega uchumi.

    Kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2003, Chris Hagen kwa nyakati tofauti alianzisha baa mbili za pombe. Lakini kutokana na ukosefu wa maarifa, pamoja na kufariki dunia kwa baba yake na yeye mwenyewe kurudi Marekani kujiunga na kijeshi, baa hizo mbili za pombe hazikuendeshwa vizuri.

    Mwanzoni mwa mwaka 2004, Chris Hagen alipiga moyo konde kufungua baa nyingine ya pombe katika mtaa wa Youyi. Baada ya matayarisho ya makini, mwezi Aprili, baa yake iitwayo the British Heaven Bar aliyoiendeshwa pamoja na wachina wengine wawili ilianza kazi rasmi.

    Ukiingia katika baa hiyo, utavutiwa mara moja na hali nyepesi ya hapo. Wageni wanaokwenda kwenye baa hiyo, baadhi yao wanakunywa pombe, wengine wanapiga soga, na wengine wanacheza dansi. japokuwa wageni wenye rangi tofauti wanatoka nchi mbalimbali, lakini nyuso zao zinaonesha ishara ya aina moja, yaani wanaipenda baa hiyo na kufurahia huduma zake.

    Msichana Gertie anayetokea Denmark, anafanya kazi katika kampuni moja ya kimataifa ya usafirishaji wa mizigo. Amekaa mjini Tianjin kwa mwaka mmoja. Japokuwa baa ya the British Heaven ilifunguliwa muda mfupi tu uliopita, lakini Gertie amekuwa akienda mara kwa mara kwenye baa hiyo.

    Alisema kuwa, anapenda hisia ya kukaa nje ya baa hiyo akinywa bia, huku akipiga soga na marafiki, aliona kama amerudi nyumbani kwake Denmark. Anaupenda mji wa Tianjin, anaona kuwa Tianjin ni mji wenye uhai .

    The British Heaven ni baa yenye mtindo maalum wa kimarekani, akiwa mwenyeji wa baa hiyo, Chris Hagen anamsalimia kila mgeni, na kuzungumza nao , kuwafanya wageni kama wamefika nyumbani kwa marafiki zao, wakifika hapa wanajilegeza na kujiburudisha . Kila usiku ndani na nje ya baa hiyo wageni hujaa, japokuwa Chris Hagen anashughulika usiku nzima, lakini hasikii uchovu hata kidogo.

    Mke wa Chris Hagen Gao Liang ni msichana mwenyeji wa Tianjin, mwanzoni alifanya kazi katika baa ya Chris Hagen, walifunga ndoa mwaka 2000. Bibi Gao Liana alisema kuwa, sasa licha ya sura yake, Chris amekuwa mwenyeji kabisa katika njia ya kuzungumza, desturi za chakula na kadhalika. Alisema kuwa:

    "Siku moja alinipigia simu akasema anataka kula tambi, nilimtuma kununua viungo vya kutengenezea tambi. Soko lenyewe liko karibu sana na nyumbani, ni kama dakika kumi tu kwenda na kurudi, lakini nilisubiri kwa nusu saa. Aliporudi, nilimwuliza kwa nini amechelewa kurudi. Alisema, niliposhuka ngazi niliwaona watu wakicheza chess barabarani, sikuweza kujizuia kusimama kuwatazama wakicheza chess."

    Pole pole Chris Hagen amezoea maisha ya Tianjin, na kuweka mzizi mjini Tianjin. Lakini anasema hiyo haitoshi, anaona kuwa, ana wajibu wa kuwafahamisha marafiki zake kutoka nchi za nje kuhusu mambo ya Tianjin. Alisema:

    "Nawapenda watu wa Tianjin na mji wenyewe, naishi hapa vizuri sana. Kwa upande wa uwekezaji, mazingira ya Tianjin pia ni mazuri sana. Kama nikimwona mgeni kutoka Uingereza na Australia, lazima nitamwambia kuwa, Tianjin ni mji wa kimataifa, pia ni mji ambao umekuwa na mabadiliko makubwa katika miaka ya hivi karibuni, bila shaka utakuwa mzuri zaidi katika siku za baadaye."

    Marafiki wapendwa, ukifika Tianjin, ukiwa na nafasi usisahau kutembelea The British Heaven Bar wakati wa usiku. Ukiingia ndani ya baa hiyo, hakika utamkuta mmarekani huyo mrefu akikuelekea na kukusalimia kwa furaha na kwa ukarimu.

Idhaa ya Kiswahili 2004-07-15