Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-16 20:34:34    
Hukumu kuhusu Ukuta wa Utenganishaji Kati ya Israel na Palestina

cri

    Waziri mkuu wa Israel Bw. Ariel Sharon tarehe 11 alieleza kuwa Israel inapinga hukumu iliyotolewa na mahakama ya kimataifa ya Hague kuhusu Israel kujenga ukuta wa utenganishaji. Bwana Sharon alisema hukumu hiyo iliyotolewa na mahakama ya kimataifa ya Hague ina lengo la kisiasa. Baada ya hukumu hiyo kutolewa, Israel imeitaka Marekani kulizuia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio husika.

    Ujenzi wa ukuta wa utenganishaji ni hatua ya kuwazuia wanachama wa makundi yenye msimamo mkali ya Palestina kuingia nchini Israel na kufanya mashambulizi. Kutokana na mpango, Israel itajenga ukuta wa utenganishaji wenye urefu wa kilomita 700 na upana wa mita 100 kwa kufuata mpaka kati ya Israel na Palestina uliowekwa kabla ya vita vya mwaka 1967 na kuzitenganisha kabisa sehemu ya Palestina ya magharibi ya mto Jordan na ardhi ya Israel.

    Ukuta wa utenganishaji utakapokamilika utakuwa wa saruji wenye kimo cha mita kadhaa, seng'enge za umeme wenye nguvu kubwa pamoja na kulindwa na askari doria. Mradi wa ujenzi wa ukuta huo ulianza mwezi Juni mwaka 2002. Tarehe 30 Julai mwaka jana, wizara ya ulinzi ya Israel ilitangaza kuwa kipindi cha kwanza cha mradi huo wenye urefu wa kilomita 110 kimekamilika. Palestina inaona kuwa sehemu kadhaa za Palestina zimechukuliwa ndani ya ukuta huo na sehemu kubwa ya Jerusalem ya mashariki ambayo inachukuliwa na wapalestina kuwa mji mkuu wao pia imekaliwa na ukuta huo.

    Habari zinasema kuwa mpaka hivi sasa, kilomita 200 za ukuta huo zimekamilika. Baada ya ukuta huo mzima kukamilika, utawatenga wapalestina laki 2.3 na sehemu zao pembezoni na kuleta shida kwa maisha ya wapalestina hao.

    Kujenga ukuta wa utenganishaji kwa Israel kunapingwa vikali na Palestina. Mwenyekiti Arafat aliishutumu kuwa Israel inatekeleza ukaburu wa kiyahudi na jumuiya ya kimataifa pia ilishutumu ubabe wa Israel.

    Tarehe 21 Oktoba mwaka jana, mkutano maalum wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio likiitaka Israel kusimamisha ujenzi wa ukuta katika ardhi za Palestina. Tarehe 28 Novemba, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Bw. Kofi Annan aliikosoa Israel kujenga ukuta na kuvunja maazimio husika ya Umoja wa Mataifa katika ripoti yake kuhusu suala la Mashariki ya Kati aliyoitoa. Tarehe 8 Desemba, baraza kuu la Umoja wa Mataifa lilitaka mahakama ya kimataifa kutoa hukumu kuhusu tukio hilo kutokana na ombi la Palestina.

    Kutokana na kukabiliwa na shinikizo la mahakama ya kimataifa kusikiliza ushahidi kuhusu uhalali wa kujenga ukuta wa utenganishaji, serikali ya Israel kwa upande mmoja ilieleza kuendelea kujenga ukuta huo, na kwa upande mwingine ilianza kufikiri kurekebisha mwelekeo wa ukuta huo. Jeshi la Israel lilidokeza kuwa baada ya kurekebisha mwelekeo wa ukuta wa Utenganishaji, urefu wa ukuta huo utafupishwa hadi kilomita 640 na ukuta huo utafupishwa kwa kilomita 80 kuliko usanifu wa mwanzo.

    Tarehe 9 Julai, mahakama ya kimataifa ya Hague ilitangaza rasmi hukumu kuhusu ujenzi wa Israel wa ukuta wa utenganishaji ambao unatakiwa kubomolewa. Lakini wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilieleza wakati huo kuwa hukumu ya mahakama ya kimataifa kuhusu Israel kujenga ukuta wa utenganishaji haina kazi ya kisheria. Kutokana na maazimio husika, ni baraza kuu la Umoja wa Mataifa tu, ndilo lenye haki ya kutekeleza hukumu hiyo.

Idhaa ya Kiswahili 2004-07-16