Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-19 13:30:33    
Safari kwenye Ghuba ya Sanniang mjini Qingzhou

cri

Ghuba ya Sanniang ya  Qingzhou iko katika mkoa ujiendeshao wa kabila la wazhuan wa Guagxi, kusini magharibi ya China.

    Kabla ya mwaka mmoja, Ghuba ya Sanniang ilikuwa kijiji cha wavuvi kisichojulika. Kijiji hicho kilikuwa na wakazi elfu moja tu, lakini hivi sasa sehemu hiyo inajulikana kuwa ni kivutio cha utalii. Mandhari nzuri ya huko ya anga buluu, bahari kubwa iliyotulia, pwani, kijiji cha wavuvi, mawe ya ajabu, pamoja na pomboo wa baharini vinawavutia watalii wengi.

    Ghuba ya Sanniang iko kwenye kitongoji cha mji wa Qinzhou, mandhari ya kimaumbile ya sehemu hiyo inapendeza sana. Mawe ya Sanniang yanayosimama kwenye ufukwe yanaonekana kama malaika wanaowasimulia watalii hadithi ya kufurahisha.

   

    Inasemekana kuwa, zamani malaika watatu wa mbinguni, walipoona wakazi wa duniani wa sehemu hiyo wakikumbwa na vurugu za uasi, walimsaidia jenerali mmoja aliyeitwa Vopo kunyamazisha uasi. Baadaye malaika hao walivutiwa na hisia za upendo kati ya wakazi wa duniani, wakabaki na kuolewa na vijana wavuvi wa huko. Hatimaye mungu alipata habari kuhusu malaika hao watatu walioondoka mbinguni bila kukubaliwa, alimtaka mfalme wa bahari kuwakamata. Mfalme wa bahari akazusha kimbunga kikali na mawimbi yaliyokwenda kasi baharini karibu kubomoa kijiji cha wavuvi. Malaika hao watatu walipambana kishujaa na mfalme wa baharini, wakageuka kuwa mawe makubwa matatu yanayosimama kwenye ufukwe ili kijiji cha wavuvi kisishambuliwe na kimbunga na mawimbi. Tangu hapo wakazi wa kijiji hicho, wavuvi wa huko waliyaita mawe matatu kuwa mawe ya Sanniang kwa kuwakumbuka malaika hao watatu. Sanniang, kwa kichina maana yake ni malaika watatu, na maskani ya wavuvi hao pia yalipewa jina la ghuba ya Sanniang.

    Naibu meya wa mji wa Qinzhou Bwana Huang Dingsong anatufahamisha: Kwenye bahari ya ghuba hiyo, kuna pomboo wa rangi tofauti ambao ni kivutio peke yake cha sehemu hiyo ya mkoa wa Guangxi, hata ni kivutio cha China pekee duniani. Nchini China, na duniani kote, ni nadra kugunduliwa kwa pomboo wa rangi mbalimbali tofauti katika eneo moja tu la bahari. Watalii waliofika huko wengi walivutiwa zaidi na pomboo wa kupendeza.

    Katika ghuba ya Sanniang yenye mandhari nzuri na maji safi, kuna pomboo wa rangi tofauti, nyeupe, nyekundu, manjano, ya kijivu. Pomboo hao wenye tabia ya uchangamfu wanapenda kuchezacheza baharini, vitendo vyao ni vyepesi vya kupendeza, pomboo hao ni wenye hulka ya kufanya maonesho mbele ya binadamu. Baadhi yao hata huthubutu kutembea mpaka karibu na meli za watalii, wakipigapiga maji baharini, na kukabiliana karibu kabisa na watalii. Kuanzia mwezi Januari mwaka huu, hali ya ajabu ilitokea kwenye ghuba hiyo, ambapo pomboo wapatao mia moja hivi hukusanyika huku wakichezacheza kwa furaha baharini. Katika eneo moja tu la bahari kujitokeza kwa pomboo wengi namna hii, hiki kweli ni kivutio cha pekee.

 

    Mkulima Wang Mao wa kijiji cha huko alisema: Mimi ni mvuvi, nimewahi kwenda sehemu nyingi kuvua samaki, lakini naona, maskani yangu Ghuba ya Sanniang ni pazuri kuliko sehemu nyingine zote.

    Watalii waliokwenda huko walituambia: Ghuba ya Sanniang inatuvutia kwa bahari yake kubwa, mawe ya ajabu, hewa na maji safi, pamoja na pomboo weupe ambao wanapatikana China peke yake. Aidha tunapenda kukaa nyumbani kwa wavuvi wa kijiji cha huko, ambao ni wachangamfu na wakarimu.

Idhaa ya Kiswahili 2004-07-19