Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-28 17:53:43    
Hekalu la Tiantan Mjini Beijing

cri

    Hekalu la Tiantan ni mkusanyiko kamili na mkubwa wa majengo ambayo mpaka sasa limehifadhiwa vizuri. Hekalu hilo lilijengwa kwa ajili ya wafalme kufanya tambiko. Kutokana na mpangilio wa majengo, muundo wa ajabu wa majengo yote, na mapambo ya kifahari, hekalu hilo linajulikana duniani na ni hazina adimu katika urithi wa sanaa za ujenzi duniani. Mwaka 1998 hekalu hilo liliorodheshwa katika urithi wa dunia.

    Hekalu la Tiantan lilijengwa mwaka 1420 kusini ya Kasri la Kifalme la Beijing, jumla ya eneo la hekalu hilo ni mita za mraba milioni 2.7, ni mara nne zaidi ya eneo la Kasri la Kifalme la Beijing. Mpangilio wake wa majengo ni sawa na Kasri la Kifalme, kwamba majengo yote muhimu yamepangwa kwenye mstari wa katikati, na yanaonesha heshima na taadhima.

    Hekalu hilo ni mahali ambapo wafalme wa enzi za Ming na Qing (mwaka 1368 ? 1911) walifanya matambiko kwa ajili ya mavuno mazuri ya kilimo. Aidha chaguo lake la mahali lilipojengwa, au mpangilio na usanifu wa majengo, yote yanaonesha wazi imani ya wahenga wa China kuhusu "mbingu" na "uhsiano kati ya mbingu na dunia" na heshima kubwa kwa mungu.

    Ujenzi wa Hekalu la Tiantan umegawanyika katika sehemu mbili, ya ndani na ya nje. Kwenye sehemu ya kusini baina ya kuta mbili ni ya mraba ikimaanisha dunia, na sehemu ya kaskazini ni ya duara ikimaanisha mbingu. Usanifu huo unatokana na ufahamu wa wahenga wa China kuwa "umbo la mbingu ni la duara na umbo la dunia ni la mraba".

    Jengo kuu katika sehemu ya hekalu hilo ni madhabahu ya duara na ukumbi wa kufanyia matambiko ya kuomba mavuno mazuri ya kilimo. Majengo hayo yalijengwa kwa umbo la duara yakimaanisha mbingu.

    Ukumbi wa kufanyia matambiko ulikuwa mahali pa wafalme kuombea hali ya hewa nzuri na mavuno mazuri ya kilimo. Ukumbi huo wa duara, una kipenyo cha mita 32, na kimo cha mita 40, una penu za matabaka matatu. Jengo hilo lilijengwa kwa muundo wa mbao tupu na halikutumiwa maboriti. Ndani ya ukumbi kuna nguzo nne zenye urefu wa mita 20 ikimaanisha majira manne ya mwaka, na kuna nguzo 12 kwenye duara ya nje, zikimaanisha vipindi 12 vya siku kama wahenga wa China walivyohesabu vipindi vya siku. Kutokana na ukumbi huo kujengwa juu ya jukwaa lenye matabaka matatu ya marumaru, ukumbi huo unaonekana mkubwa na mrefu.

    Madhabahu ya duara ni mahali ambapo wafalme walifanya sherehe ya kumwabudu mungu, ina matabaka matatu ya duara. Kusimama juu ya madhabahu hayo na kuangalia mbali, mbingu buluu kichwani na marumaru nyeupe miguuni, mtu anajiona kama yuko ndotoni. Ubunifu wa madhabahu ya duara pia ni wa ajabu, ambao ulitumia tarakimu "tisa" katika ujenzi wa madhabahu hiyo: Pembezoni mwa jiwe la katikati la madhabahu hiyo yalitandazwa mabamba ya mawe tisa, na mabamba mengine nyongeza yalitandazwa katika duara ya pili, vivyo hivyo kila duara iliyo nje mabamba ya mawe huongezwa tisa mpaka duara ya mwisho ya tisa. Kisha ni matabaka ya duara, jumla kuna matabaka tisa, na kila tabaka lina ngazi tisa, na kila ngazi ya duara ya nje mabamba ya mawe huongezwa tisa zaidi mabamba ya duara ya ndani. Inasemekana kuwa ubunifu huo unatokana na dhana ya wahenga wa China kuwa mbingu ina matabaka tisa na mbingu ya juu kabisa ni ya tisa, ambapo ndipo miungu wanapokaa.

    Muundo wa jengo la duara ni mgumu kuliko la mraba, aidha katika hesabu, matumizi ya vifaa vya ujenzi au katika kazi za kujenga. Muundo wa majengo katika Hekalu la Tiantan ni wa utatanishi na wa kisayansi, ni ishara ya kiwango cha juu cha sayansi ya ujenzi wa China katika karne ya 16.

    Mafundi wa ujenzi wa hekalu hili pia walipiga hatua kubwa katika mapambo na rangi walizotumia. Kwa kawaida, majengo ya kifalme yalikuwa yakipambwa kwa vigae vyenye rangi ya njano ikimaanisha madaraka ya kifalme, lakini majengo katika sehemu ya Hekalu la Tiantan yote yalipambwa kwa rangi ya buluu ikilifananisha hekalu na rangi ya mbingu. Aidha jukwaa la madhababu ya duara, au paa la ukumbi wa kuombea mavuno mazuri au mapaa ya kuta za uzio, yote yaliezekwa kwa vigae vya rangi ya buluu. Rangi hiyo inazidisha hisia za mtu kuwa katika kasri la mbinguni.

    Kuna majengo kadhaa ya ajabu katika ya sehemu ya Hekalu la Tiantan. Mfano mmoja ni jiwe lililopo katikati ya madhababu ya duara. Mtu akisimama katikati ya jiwe hilo na kutoa sauti atasikia mwangwi kutoka pande zote kama vile anaota ndoto. Wafalme walipofanya sherehe hapo na kusema kitu, sauti ilirudia rudia kama inatoka mbinguni, ikimaanisha sauti ya mungu, ili kuwa ni lazima waifuate, la sivyo, wangeonekana wanakwenda kinyume na nia ya mungu. Mfano mwingine ni ukuta wa mwangwi ambao ni wa kwanza katika kuta nne kubwa za mwangwi nchini China. Huu ni ukuta wa duara, mtu akiongea kwa sauti ya kunong'neza kwenye upande mmoja mwengine anasikia katika upande wa pili. Licha ya mifano hiyo miwili, pia kuna jiwe lenye sauti za aina tatu, jiwe la kupashana sauti ya maongezi n.k. Yote hayo yanaonesha elimu kubwa ya wahenga wa China kuhusu nadharia ya sauti.

    Ndani ya sehemu ya Hekalu la Tiantan imepandwa miti mingi, ambayo inaeleza tumaini la wahenga wa China kuishi vema na mazingira bora ya kimaumbile.

    Hekalu la Tiantan ni hazina ya majengo ya kale nchini China, ni majengo ya yanayodhihirisha filosofia ya watu wa China ya kale, na pia ni kumbukumbu ya utamaduni ya kipindi cha historia ya China. Kamati ya Urithi wa Dunia ilitathmini kuwa Hekalu la Tiantan aidha mpangilio wake wa majengo, au kila jengo lake, yote yanaonesha uhusiano wa mbingu na ardhi, na uhusiano huo ndio mtazamo wa watu wa China kuhusu ulimwengu katika enzi za kale.