Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-26 21:10:54    
Msanii wa kuchekesha Yan Shunkai

cri

   

    Msanii wa michezo ya kuchekesha Yan Shunkai alizaliwa mjini Shanghai mwaka 1937. Toka utotoni mwake alikuwa na hamu na michezo ya sanaa. Alipokuwa katika shule ya sekondari mara nyingi alikuwa akicheza michezo jukwaani na kutamani kuwa msanii nyota. Ingawa aliwahi kushiriki katika mitihani mingi ya kujiunga na vyuo vikuu vya tamthilia na filamu, lakini kila mara alishindwa katika mchujo wa mwisho kutokana na sura yake ya kusikitisha. Alipojikumbusha hali hiyo alisema, "Nilisikia uchungu sana baada ya kushindwa kuchaguliwa, kwa sababu matumaini yangu yalikuwa makubwa. Nilipokuwa sekondari, wanafunzi wenzangu walisema nilicheza vizuri, na hakika nitafanikiwa mtihani. Kusema kweli, baadhi ya dosari kama ufupi na sura yangu isiyovutia nilizaliwa nayo hata nikijitahidi namna gani siwezi kuondoa."

    Lakini Yan Shunkai hakufa moyo, mwishowe alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Tamthilia, katika mitihani alionesha akili yake nyepesi, mchezo alioucheza katika mtihani hata uliwachekesha walimu waliomtahini. Yan Shunkai alipasishwa na alipokelewa na chuo hicho kwa kuwa "mwenye sura isiyo ya kawaida".

    Katika miaka minne alipokuwa chuoni, alama zake za masomo zote zilikuwa nzuri. Katika mazoezi ya michezo, mara nyingi alicheza nafasi ndogo, na alijitokeza dakika chache tu jukwaani. Lakini katika dakika hizo chache alicheza kwa makini sana. Katika mchezo alioshiriki kabla ya yeye kuhitimu masomo katika chuo kikuu, uhodari wake wa kuonesha michezo ulimvutia mwongozaji wa filamu Huang Zuolin, akampokea katika Jumba la Michezo ya Sanaa la Shanghai.

    Mchezo uliompatia umaarufu ni filamu ya "Hadithi ya Kweli ya A Q" aliyocheza katika mwaka 1981.

    "Hadithi ya Kweli ya A Q" ni riwaya iliyoandikwa na mwandishi mashuhuri wa China, Luxun. Riwaya hiyo ilimwelezea mkulima A Q aliyeishi mwanzoni mwa karne ya 20 ambapo China ilikuwa katika kipindi cha mwisho cha jamii ya kimwinyi na kupitia masimulizi ya mkulima huyo alionesha jinsi wakulima walivyokuwa wajinga, wapumbavu, wanyonge na walivyojipumbaza kwa kujiliwaza. Mhusika mkuu wa riwaya hiyo A Q anajulikana kwa Wachina wote, na amekuwa kama mwakilishi wa watu waliojidanganya kiroho.

    Ili aweze kuigiza vizuri jinsi alivyokuwa A Q, Yan Shunkai alienda katika kijiji alichoishi A Q, alijigeuza kama mlikuma wa huko, na kuongea kwa lafudhi ya wenyeji na kuishi pamoja na wakulima wa kijijini. Kutokana na uzoefu alioupata katika maisha halisi alikuwa ameelewa kwa undani zaidi A Q alivyokuwa katika riwaya aliyoandikwa na mwandishi Luxun. Katika filamu aliyoigiza, alimuiga vilivyo A Q, mtu wa kuchekesha, kupendwa, kusikitisha na kuchukiza. Kutokana na filamu hiyo Yan Shunkai amekuwa mchezaji maarufu miongoni mwa Wachina na alipata tuzo kubwa ya wachezaji hodari wanaume, na mwaka 1982 alipata tuzo ya "bakora ya dhahabu" katika tamasha la kimataifa la filamu za kuchekesha. Mchezaji Yan Shunkai alisema kuwa filamu ya "Hadithi ya Kweli ya A Q" imempandisha ngazi nyingine katika uchezaji wake. Alisema, "Filamu hiyo ilinisaidia sana katika usanii wangu maishani mwangu. Baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu, filamu hiyo ilinipa nafasi nzuri ya kuendeleza usanii wangu. Kwa kweli filamu hiyo ilinielimisha sana, ni mchezo wa kunipandisha kiwango kipya cha uchezaji."

    Tokea hapo, Yan Shunkai alicheza michezo mingi ya filamu, televisheni na jukwaani, amekuwa mcheza mkuu katika michezo yote ya kuchekesha. Michezo aliyocheza karibu yote inahusiana na maisha ya makabwela ambayo yanatokea siku zote katika maisha ya kawaida.

    Kutokana na kuwa michezo yake inaeleza matukio madogo madogo maishani, watazamaji wanayafahamu vilivyo na walipojiburudisha na michezo yake hupata mafundisho. Akiwa msanii wa kuchekesha, Yan Shunkai siku zote anafuata kanuni yake ya kutowachekesha watazamaji bila lengo. "Sio rahisi hata kidogo kuifanya michezo ya kuchekesha iwe na maana, michezo yangu haikutungwa ovyo bali ni matukio yenye uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya raia na lazima iwafanye watazamaji wafikiri baada ya kuitazama." Yan Shunkai alisema.

    Maisha ya Bw. Yan Kaishun ni ya kawaida kabisa, yeye ni mnyekekevu na mchekeshaji, anapoongea maneno machache tu anawachekesha watu. Anapokuwa na wasaa anapenda kutembelea madukani, na nyumbani kwa watu ili apate nyenzo za michezo yake. Ingawa anakaribia umri wa miaka 70 lakini anaendelea na juhudi zake za kutunga na kushiriki katika michezo. Alisema, "Maneno ya kiongozi mmoja yaliniingia sana akilini mwangu, alisema, kila mchezo alioucheza mchezaji ni bora upate alama ya kujumlisha, bali sio alama ya kutoa katika hesabu, japokuwa asilimia moja tu, lakini ni nyongeza. Kwa hivyo haifai kulegeza juhudi zangu."