Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-27 21:35:38    
Maisha mapya ya mkulima Wan Yi na mkewe

cri

    Mkulima Wan Yi ambaye mwaka huu ana umri wa zaidi ya miaka 40, anaishi pamoja na mkewe katika mkoa wa Guizhou. Katika siku za hivi karibuni kila siku wamekuwa wakijishughusha na kazi katika zizi la nguruwe na banda kubwa la maua. Wanafurahi sana kila wanapoona nguruwe wadogo wanakua haraka na maua waliyopanda kuchanua na kutoa maua mazuri yenye rangi mbalimbali. Ingawa Bw. Wan Yi hana maneno mengi, lakini akizungumzia nguruwe waliofuga au maua waliyopanda, anakuwa na maneno mengi chungu nzima,

    "Nguruwe tunaowafuga hivi sasa, ambao ni chotara wa kizazi cha pili, wanakua haraka sana, na wanaweza kuuzwa baada ya kufugwa kwa siku 100 hivi. Marekebisho ya zizi la nguruwe, njia ya ufugaji na usimamizi niliyapata kwenye masomo yaliyooneshwa televisheni. Ninaona kuwa nguruwe wa aina hiyo watapata soko kubwa sana. Mbali na hayo, mwaka huu, nitajenga mabanda zaidi ya 10 ya maua, kutokana na mauzo yake mazuri ya nguruwe. Ufundi wa kupanda maua pia niliupata katika masomo ya televisheni.

    Masomo anayoyasema Bw. Wan Yi ni mafunzo ya kazi yaliyotolewa na idara husika za China katika miaka ya karibuni ili kuongeza pato la wakulima, ambayo yanaeneza ufundi wa kilimo, kuwawezesha wakulima kufahamu sayansi na teknolojia ya kilimo na kupanua mawazo yao katika kukuza njia ya uzalishaji mali.

    Bw. Wan Yi na familia yake wanaishi katika mkoa wa Guizhou, sehemu ya kusini magharibi ya China, ambayo iko nyuma kimaendeleo hapa nchini. Mkoa huo ulianza kutoa mafunzo ya elimu ya kilimo toka mwaka 2003. Ili kuwawezesha wakulima wapate elimu ya kilimo, mkoa huo ulianzisha madarasa ya elimu ya TV katika vijiji vilivyochukuliwa kuwa ni vya majaribio. Kijiji cha Qingshan kilichoko karibu na Guiyang, mji mkuu wa mkoa wa Guiyang, ni moja ya vijiji vya majaribio ya elimu ya TV.

    Ukiingia kwenye darasa la elimu ya TV la kijiji cha Qingshan, TV moja kubwa inavutia sana macho ya watu. Mtunzaji wa darasa la TV, alitoa kanda kadhaa za TV za elimu ya kilimo zikiwemo za elimu za ufugaji wa kondoo, upandaji wa miti ya matufaha na udhibiti wa maradhi ya nguruwe. Ili kuwarahisishia wakulima wa huko kupata elimu hiyo, kanda hizo zimerekebishwa na kutumia lafudhi ya huko Guizhou.

    "Udongo wa aina hiyo, ni laini, na hewa hupenya kwa urahisi, na una samadi nyingi na ni mwafaka kwa kilimo cha maua ya azelia."

    Mtunzaji wa darasa alisema kuwa vitabu na CD zinatumika bila malipo, na wanakijiji wanaweza kuziazima wakati wowote. Licha ya hayo, kijiji hicho kimenunua kompyuta ambayo inaweza kutumiwa kuchukua data kuhusu uzalishaji wa kilimo kutoka kwenye mtandao wa Internet bila malipo kwa ajili ya wanakijiji.

    Hivi sasa, familia ya Bw. Wan Yi na wakulima wengine wa kijiji hicho, wanapenda sana kujifunza katika darasa la TV. Bw. Wan Yi na mkewe, wakitumia elimu ya TV, wamefuga nguruwe 10 pamoja na kujenga mabanda zaidi ya 10 yaliyopandwa maua ya azelia, waridi na mengineyo. Alisema kuwa kujishughulisha na kazi za ufugaji wa nguruwe na kupanda maua, ni wazo alilopata katika masomo ya TV. Kwa kufanya hivyo anaweza kutumia vilivyo rasilimali zake. Alisema,

    "Vinyesi vya nguruwe vinaweza kutumiwa kama samadi kwa upandaji wa maua, hivyo sina haja ya kununua mbolea kwa ajili ya maua, hivyo gharama ya upandaji wa maua inapungua."

    Hapo mwanzoni, Bw. Wan Yi mara kwa mara alikwenda nje kufanya kibarua, aliwahi kufanya kazi za kuchimba madini katika mgodi, kujenga nyumba na kuwa mchuuzi. Alisema kuwa kufanya kazi za kibarua, wakati mwingine anaweza kutopata chochote. Lakini hivi sasa, akiwa nyumbani tu, anaweza kuchuma pesa pia. Bw. Wan Yi aliwahi kupanda maua ya waridi, lakini kutokana na kukosa ujuzi, miche ya maua ya waridi aliyopanda yote ilikufa. Hivi sasa anatumia elimu ya TV, anapanda tena maua ya waridi na sasa hana wasiwasi.

    Mkewe Wan Yi alisema kuwa mbali na kufuga nguruwe na kupanda maua, familia yake inaendelea kulima mpunga. Ingawa shughuli ni nyingi, lakini kazi zao zinawaletea faida kubwa.

    Bw. Wan Yi amepiga hesabu, anaona kuwa mwaka huu familia yake itakuwa na pato zuri, ambalo ni kubwa zaidi kuliko alilopata wakati alipofanya kibarua sehemu za nje. Alisema kuwa kila nguruwe jike analeta faida ya Yuan kati ya 1,600 na 1,800. Kila ua moja la azelia linaleta faida ya Yuan 1. Endapo mwaka huu halitatokea tukio lisilotarajiwa, familia yake itapata Yuan elfu 10 hadi elfu 20 kutokana na mauzo ya maua ya azelia. Licha ya maua ya azelia, mauzo ya maua mengine yanatarajiwa kuwaletea faida kama kiasi hicho.

    Familia nyingine za wakulima wa kijiji cha Qingshan ni kama familia ya Bw. Wan Yi, zinajifunza ujuzi wa uzalishaji mali wa kilimo kwa kupitia TV. Wakulima wa kijiji hicho zamani walikuwa wakijihusisha na kilimo cha zao la mpunga peke yake. Lakini sasa, mafunzo ya elimu ya kilimo ya TV yanabadilisha uzalishaji mali wa kijiji hicho. Hivi sasa wakulima wa kijiji hicho wanapanda vitunguu, nyanya, matunda, na mazao mengine ya kiuchumi. Kupanda maua ya kuuza kumekuwa shughuli muhimu za uzalishaji mali katika kijiji hicho. Inakadiriwa kuwa shughuli za kupanda maua zitawaletea wanakijiji wa kijiji hicho Yuan laki 6. Mkuu wa kijiji, Bw. Yang Lishu alisema kuwa kabla ya kupata mafunzo ya TV, wakulima wa kijiji hicho hawakujua kuendeleza uzalishaji mali kwa elimu ya sayansi na teknolojia, lakini sasa wameona manufaa ya kujua elimu ya sayansi na teknolojia.

Idhaa ya Kiswahili 2004-07-27