Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-28 17:28:56    
AIDS (UKIMWI) 13

cri
    Eti ni kweli hospitali zinaruhusu wagonjwa wa UKIMWI walio karibu kufa warudi kufia nyumbani?

    Kuna baadhi ya wagonjwa au jamaa zao ambao hupendekeza au kuomba waruhusiwe kurudi nyumbani. Lakini kwa kawaida kabla ya kupewa ruhusa kama hiyo hospitali zinajaribu kuhakikisha kwamba wagonjwa hao hawataendelea kupata shida kubwa huko nyumbani, na kwamba jamaa zao wameelimishwa na kuelewa jinsi ay kuwahudumia, na pia jinsi ya kuchukua tahadhari zinazopasa kuzuia kuambukiza huo ugonjwa kwa watu wengine huko nyumbani.

    Ni tahadhari gani zinazofaa kuchukuliwa wakati wa kuishi na mgonjwa wa UKIMWI nyumbani ili kuzuia wengine wasiambukizwe?

    Ni muhimu kuzingatia baadhi ya mambo yafuatayo:

    1. Msishirikiane naye vitu kama taulo, nyembe na mswaki.

    2. Vijeraha vyovyote katika mwili wa mgonjwa na katika kila mwili wa kila mmoja nyumbani yafaa vifungwe na kitu kisicho ruhusu majimaji yoyote kuingia wala kutoka.

    3. Damu au majimaji yoyote yatakayokuwa yanamtoka mgonjwa mahali popote mwilini yaguswe au yashikweshikwe na mtu ambaye amevaa mipira mikononi.

    4. Ni lazima kunawa mikono kila mara baada ya kumhudumia mgonjwa, na mgonjwa mwenyewe yampasa anawe mikono yake kila mara baada ya kumaliza kujisaidia mwenyewe.

    5. Kinyesi cha mgonjwa au vitambaa anavyotumia wakati wa hedhi, au vitambaa vinavyotumika kupangusa damu na majimaji mengine yatakayokuwa yanamtoka?hivi vyote lazima vitumbukizwe chooni au vifukiwe chini ardhini bila kuchelewa.

    6. Shuka na chupi zenye kuwa na madoa ya usaha, au ya damu, au madoa ya majimaji ya kiume ya uzazi, lazima zichemshwe kwanza kabla ya kufuliwa.

    7. Vitambaa vya mkononi na nguo nyingine za kitandani zifuliwe kwa sabuni na maji moto.

    8. Kushirikiana sahani, vikombe, bakuli, vijiko n.k. hakuna hatari mradi tu vyombo hivyo visafishwe kwa sababu na maji moto.

    9. Kila inapowezekana kwenye sakafu na mahali popote palipodondokea damu, usaha, kinyesi, matapishi, na majimaji mengine toka mwilini mwa mgonjwa panyunyiziwe dawa ya kuua viini vya ugonjwa kwanza k.m. (0.2% sodium hypochlorite) kabla ya kusafishwa na sabuni na maji moto.

    Vyombo vilivyotumika kuhifadhi kinyesi, matapishi, uchafu na majimaji mengine yaliyotoka mwilini mwa mgonjwa visafishwe kwa sabuni na kuchembshwa. Endapo vitaweza kuharibika kwa kuchemshwa, basi vitumbukizwe kwenye dawa za kuua viini vya magonjwa. Dawa hizi za kuua viini vya magonjwa zipo za aina mbalimbali (k.m. sodium hypochlorite, spirit, chlorine, ethanol n.k.)

Idhaa ya Kiswahili 2004-07-28