Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-29 18:17:32    
Hadithi ya Bi. Zhang Luping na nyumba yake ya wanyama

cri

    Bi. Zhang Luping mwenye umri wa miaka 50 mwaka huu aliwahi kuwa askari katika kikundi cha michezo ya sanaa kwa miaka zaidi ya kumi. Mwanzoni, marafiki zake waliojua tabia yake ya kupenda wanyama walimletea mbwa na paka wao na waliookotwa mitaani pia. Nyumba ya kwanza ya wanyama hawa ilikuwa ofisi ya Zhang Luping, lakini kutokana na idadi ya wanyama aliowapokea kuongezeka zaidi na zaidi, Bi. Zhang Luping alipaswa kuhamahama pamoja na wanyama wake, kutoka nyumba nzuri la kijijini hadi ghala la kuwekea shehena, na mwishonwe amehamia makazi ya sasa yenye eneo la hekta 3 kwenye kitongoji cha kaskazini cha Beijing.

    Hali ya kuhamahama si kama tu ilimchukua muda mwingi na kugharimu fedha zake zote, bali pia ilimhuzunisha kwa kutoweza kupata maelewano mema kutoka kwa jamii pamoja na jamaa na marafiki zake. Lakini Bi. Zhang Luping alikuwa anashikilia msimamo wake kwamba ataendelea kuwatunza wanyama walioachwa au kujeruhiwa.

    "Nafikiri japokuwa wanyama hawawezi kuongea, lakini wanaweza kuwasiliana na kusikilizana na binadamu, na kuleta furaha kwa binadamu. Wanapoingia katika maisha yangu au wanapohitaji hifadhi yangu, sina sababu ya kuwafukuza."

    Aliposimulia hadithi za wanyama aliowatunza, Bi. Zhang Luping hawezi kujizuia kuwa na huzuni. Alisimulia kuwa, mbwa mmoja alipoachwa na bwana wake alikuwa hataki kuondoka na ili kumfukuza kabisa, bwana wake alimwagia maji ya moto na kumjeruhi vibaya. Wakati nilipomwokota alijificha kichakani kwa kuogopa kuteswa tena.

    Akiishi na wanyama hao, Bi. Zhang Luping hana budi kupiga moyo konde kuendelea na huruma yake hawezi kuacha kiumbe chochote kutahatarishwa maisha na pengine kuuawa ovyo.

    Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kuinuka kwa hali ya maisha, Wachina wengi wanapenda wanyama kipenzi kama mbwa, paka na kadhalika, lakini watu hawa hawana upendo wa kutosha kwa wanyama, wakati mbwa au paka wao wanapougua wanawachukia na kuwaacha katika hali mbaya na watu wengine wanafikia hatua ya kuwanyanyasa. Lengo la Zhang Luping la kuanzisha nyumba ya wanyama licha ya kuwapokea na kuwatunza wanyama hao walioachwa, pia anataka kutoa fursa kwa wakazi au watoto wanaoitembelea nyumba hiyo kuwasiliana na wanyama hao ili wawe na upendo kwa wanyama wengine majumbani mwao. Alisema:

    "Nataka kuifanya nyumba hiyo ya wanyama kama kituo cha kuwaelimisha wakazi wa Beijing. Kama wanyama walioachwa na kunyanyaswa wakiongezeka mjini Beijing, mimi peke yangu nitashindwa kuwashughulikia wanyama hao wote. Hivyo natumaini nitawaelimisha wakazi jinsi ya kupenda maisha na kutunza viumbe wote wa kimaumbile kwa mfano wangu"

    Bi. Zhang Luping bado anaishi peke yake, alisema kuwa, kuishi pamoja na mbwa na paka zaidi ya 400 ndio maisha yake yote, wamemletea furaha na faraja kemkem. Bi. Zhang ameugua saratani kwa miaka 10, lakini hajatumia dawa yoyote, pia hajawahi kwenda hospitali, alisema, wanyama hao ndio wanaompa nguvu na moyo wa kuishi hadi leo hii.

    Hadithi ya Bi. Zhang Luping baada ya kujulikana, inawasisimua watu wengi, ambao wanajaribu kumtafuta ili kumsaidia kuwatunza wanyama hao wadogo, wengine hata wanawachukua nyumbani wanyama ili kupunguza mzigo wake. Mwakilishi wa China wa Mfuko wa Kimataifa wa Kuwapenda Wanyama Bwana Zhang Li alisifu vitendo vya Bi. Zhang Luping, na alitumai kuwa watu wengi zaidi wangejiunga na kazi hiyo ya kuwapenda wanyama. Alisema,

    "Nafikiri fikra za Zhang Luping ni za kisasa na zinastahili kuungwa mkono. Watu wengi wanapowaokoa na kuwatunza wanyama wanakosa fikra sahihi za kuwazingatia wanyama, yaani kutoa huduma kwa wanyama. Hivyo ndivyo Zhang Luping alivyojitahidi kuwatosheleza wanyama mahitaji yao."

    Bi. Zhang Luping licha ya kuwatunza wanyama zaidi ya 400, pia anawasaidia marafiki zake kutunza wanyama wao wanapoondoka nyumbani. Mahojiano yetu yalipokaribia kumalizika, tulimkuta mbwa kipofu aliyechukuliwa na mwalimu mmoja wa chuo kikuu kurudi kumtembelea Zhang Luping. Bi. Zhang alifurahi sana kumwona mbwa huyu mwenye afya. Alisema kuwa, mbwa huyo alipookotwa alikuwa kipofu na mwenye maradhi ya ngozi mwilini. Baada ya matibabu ya makini, maradhi yake yalipona. Mwalimu aliyemchukua mbwa huyo alimtunza kwa makini sana, na pia humrudisha mara kwa mara ili akaguliwe hali yake ya afya.

Idhaa ya Kiswahili 2004-07-29