Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-30 16:56:00    
Libya inayozifunguliwa mlango nchi za nje

cri
    Wakati mwandishi wa habari alipowasili nchini Libya, aligundua nchi hiyo ipo katika jitihada za kuendeleza kazi ya utalii: Kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Tripoli, ndege nyingi zinazosafiri nchi za nje zinaruka na kutua; kwenye soko la kazi za mikono, wauzaji wa bidhaa rejareja wanajadiliana bei na wanunuzi kwa lugha ya kiingereza rahisi?Ingawa hiyo ni hali ya kawaida ambayo inatokea kila siku katika sehemu nyingine ulimwenguni, lakini hayo ni matokeo makubwa sana kwa nchi hiyo iliyowekewa vikwazo vya kimataifa kwa miaka 13. Baada ya Umoja wa Mataifa kuondoa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Libya, nchi hiyo imechukua hatua gani na bado inakabiliwa na matatizo gani?

    Ndani ya ofisi ya Bw. Faris, picha zenye mandhari nzuri ya kimaumbile na masalio ya historia ya Libya zimebandikwa ukutani. Bw. Faris alimwambia mwandishi wa habari kuwa, uendelezaji wa utalii ni sera muhimu ya Libya. Utalii utaleta ajira mpya na fedha za kigeni kwa Libya, vilevile ni dirisha kubwa la kuioneshea dunia hali ya Libya kwa nchi za nje. Watalii watajisikia ukarimu wa walibya na msimamo wa serikali ya Libya wa kufungua mlango kwa nchi za nje. Kutokana na hayo, serikali ya Libya ilianzisha Idara ya uwekezaji vitega uchumi na uendelezaji wa utalii, ili kuweka mkazo katika kazi hiyo.

    Bw. Faris alisema kwa fahari kubwa kuwa, Libya ina maliasili nzuri ya utalii. Kwanza hali yake ya kijiografia ni nzuri sana. Nchi hiyo iko katika pwani ya kusini ya bahari ya Mediterranean wakati ukanda wake wa pwani unafikia kilomita 100. Hali yake ya hewa ya kimediterranean inawaburudisha sana watalii. Kuna majangwa yasiyo na mipaka katika sehemu ya kusini ya nchi hiyo, wakati maziwa kwenye sehemu ya jangwa na maporomoko ya maji milimani ni mandhari za pekee zinazowavutia watalii sana. Aidha, Libya ina historia ndefu na utamaduni wa kung'ara ambavyo vimeleta urithi mwingi wa kihistoria na kiutamaduni. Mwanzoni mwa mwaka huu, wanaakiolojia waligundua piramidi kadhaa kwenye jangwa lililoko kusini mwa Libya. Hivi sasa, wanaakiolojia wanajitahidi kufanya uchimbuaji na uthibitishaji ili kuifanya kuwa sehemu mpya ya utalii.

    Lakini Bw. Faris pia alikiri kuwa, Libya bado inakabiliwa na matatizo mengi. Kwanza, haina uwezo wa kutosha kuwahudumia vizuri watalii kutokana na suala la miundo mbinu. Takwimu zinaonesha kuwa, hivi sasa kuna vitanda elfu 20 tu ndani ya hoteli mbalimbali nchini Libya, vingi kati yao hivyo ni vibovu sana. Aidha, Libya haina kiasi kikubwa cha watu wanaofahamu kazi ya utalii. Mbali na hayo, kutokana na mapambano kati yake na Marekani na nchi nyingine za magharibi, lugha za kigeni hususan Kiingereza zilichukuliwa kama ni lugha za wapinzani na kupigwa marufuku kutumika. Hivyo, vijana wachache sana wanafahamu lugha za kigeni, na wapo wahudumu wachache wanaofahamu lugha za kigeni katika hoteli zinazowapokea wageni. Aidha, sheria kuhusu kudai kuwataka wageni wote kuwa na tafsiri ya pasipoti kwa lugha za kiaarabu vilevile zinaweka vikwazo kwa maendeleo ya kazi ya utalii nchini Libya. Kutokana na hali hizo mbalimbali, watu laki 5.5 tu walifanya utalii nchini Libya mwaka 2001.

    Lakini Bw. Faris alisema, hivi sasa serikali ya Libya inachukua hatua mfululizo ili kuendeleza utalii. Mwezi Aprili, mwaka huu, serikali ilitoa amri ya kutaka idara mbalimbali za serikali kuunga mkono maendeleo ya utalii, kazi ya kodi, mikopo na usimamizi wa utawala wa kiserikali, na kuweka sera nyingi zenye ufanisi kwa nchi za nje kuweka vitega uchumi katika utalii nchini Libya. Wakati huo huo, Libya inatilia mkazo kufanya ujenzi wa miundo mbinu, na kujenga hoteli zenye kiwango cha juu huko Tripoli na miji mikubwa ya pwani. Pia inapangakuongeza idadi ya hotelini nchini kote kufikia laki 1 ifikapo mwaka 2010.

    Kwa upande mwingine, Idara ya uwekezaji vitega uchumi na uendelezaji wa utalii pia inajitahidi kushiriki kwenye maonesho mbalimbali ya utalii ulimwenguni, tokea mwaka huu uanze imefanya harakati za kutangaza utalii wa Libya huko Paris, London na Milan. Hivi sasa Libya inaanza kuandaa watu wanaoshughulikia utalii, na kuanzisha masomo ya utalii katika vyuo vikuu kadhaa, na kuongeza masomo ya lugha za kigeni katika shule za msingi na sekondari, ili kuhimiza vijana kujifunza lugha za kigeni tokea utotoni. Bw. Faris alisema, juhudi za serikali ya Libya zimeleta matokeo mazuri, watu wanaofanya utalii nchini Libya kutoka nchi za nje mwaka 2003 walifikia laki 9.6, na mwaka huu inatazamia kufikia milioni 1.5. Hayo ni mafanikio makubwa kwa nchi hiyo ambayo ya watu wake haijafikia milioni 5.

    Mwishoni mwa maelezo yake, Bw. Faris alitoa mwaliko kwa wananchi wa China: "Tunawakaribisha sana wachina kufanya utalii na kufanya biashara nchini Libya! Mlango wa Libya siku zote uko wazi kwa dunia nzima, hususan marafiki zetu wema wachina!"

Idhaa ya Kiswahili 2004-07-30