Bwana Tellya Wambwa wa Bongoma Kenya ametuletea barua akizungumzia ugonjwa wa ukimwi, pamoja na maoni yake kuna shairi kuhusu ukimwi, anasema angeomba wakuu wa Radio China Kimataifa walichapishe shairi hili katika tovuti (www.cri.cn) kwa lugha tofautitofauti kama vile kingereza, kijapani, kihispaniola, kitaliano, kihindi, kijerumani pamoja na lugha nyingine ili kuwaelimisha watu wasio na virusi vya ukimwi duniani kote. Shairi alilotuletea Bw Wambwa lina kichwa kisemacho " TIBA YAKE KABURINI" na maelezo ya shairi hilo yanasema:
Nalalama ukumbini, ugonjwa hata sana
Ukimwi wapenya ndani, kwa kweli raha hatuna
Tuko na wasiwasi, sote makini hatuna
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini.
Siji kuwashitueni, bali ukweli kunena
Sababu ndugu zangu, shida imepatikana
Hatuwezi asilani, kuanza kudanganyana
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini
Tulikotoka jamani, hata fununu hatuna
Kuutambua mwilini, pia ni vigumu sana
Mapema hujulikani, na matibabu hauna
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini
Huu ugonjwa jamani, huruma kamwe hauna
Waupata tu rahani, na bila kujua tena
Au kwa matibabuni, huenda ukapatikana
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini
Hamu ya kula huoni, hapo ukimwi washona
Wabadilika mwilini, kijivu kuonekana
Kisha wakonda mwili, halafu wakaukiana
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini
Nidhamu tuidhamini, kwa wapenzi sana sana
Jua mmoja mwandani, halafu tujependana
Hamu isituzidini, na yeyote kulalama
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini
Tokeni uasherati, kwani huo si ungwana
Uasherati ndo soko, la ukimwi kufanana
Tusijiuze mwilini, pasi hata kupendana
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini
Tuendapo matemboni, tusilewe tu bayana
Kuonana kimwili, na yeyote toneana
Hapa twende hatarini, kwa tendo kujamiiana
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini
Huko hospitalini, mtufikirie tena
Sindano mtudungeni, zilizosafishika sana
Kwani hasipitalini, eti unambukizana
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini
Kwa sasa twawaombeni, waaguzi kupambana,
Madaktari jaribuni, dawa ije patikana,
Hata dawa ya shambani, ikiwa yawezekana
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini
Tukishindwa wenzanguni, hapo tukipatikana
Tusihamaki lakini, kuanza gawagawana
Wenzetu twafikirini, tusiage na laana
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini
Ninakoma ukingoni, na ujumbe wangu tena
Wasiwasi tuondoeni, kwani haina maana
Lililoko tujikingeni, ushikwapo shikamana
Ukimwi dawa hauna, tiba yake kaburini
Bwana Telly Wambwa anasema, ana matumaini kuwa tutalifurahia shairi lake kuhusu ukimwi. Shairi hili ni kama marudio kwani kuna wakati fulani alituma shairi hili la ukimwi kwa Radio China Kimataifa. Lakini hata hivyo tunashukuru kwa Shairi hili ambalo limeweza kuwakumbusha watu hatari ya Ugonjwa wa Ukimwi. Lakini tusikate tamaa, kwani wataalamu wanafanya utafiti na kutengeneza dawa mpya za kutibu ugonjwa wa ukimwi.
Idhaa ya Kiswahili 2004-08-03
|