Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-05 21:10:08    
Sera za "mahakikisho mawili ya matibabu" kwa "wazee wa aina tatu" kutekelezwa mkoani Shandong nchini China

cri
    Mzee Shang Shaojun aliyemaliza miaka yake ya kulihudumia Jeshi la Ukombozi la China ni mwenyeji wa kijiji cha Gaoze kilichoko wilaya ya Wulian mkoani Shangdong. Ameumwa kichwa kwa miaka mingi na kutokana na gharama kubwa za matibabu alikwenda hospitali mara chache. Lakini katika nusu ya kwanza ya mwaka huu aliwahi kulazwa hospitali mara tano na sasa amepona kabisa. Alisema, "Nashukuru sana sera za serikali kwa sisi 'wazee wa aina tatu'. Gharama za matibabu yangu nilipolazwa zilikuwa yuan elfu 12 na mia 9, na nilirudishiwa yuan elfu 9 mia 9 na senti 48 kutoka wilayani, pesa nilizolipa kutoka mfukoni mwangu ni kiasi kidogo sana, jambo ambalo hata zamani sikuthubutu kulifikiria ."

    "Wazee wa Aina Tatu" ni wazee waliofiwa na jamaa waliojitolea mhanga kwa ajili ya taifa, watu waliopata ulemavu katika vita na wazee waliowahi kulihudumia jeshi. Wilaya ya Wulian ilikuwa ni sehemu iliyokombolewa mapema kabla ya China nzima kukombolewa, na katika wilaya hiyo kuna jumla ya "wazee wa aina tatu" 1632. Kabla ya sera za "mahakikisho mawili ya matibabu" kutekelezwa, matibabu yao yalikuwa ni magumu sana kutokana na gharama kubwa. Kutokana na hali hiyo serikali ya wilaya ya Wulian ilitunga na kutekeleza sera za "mahakikisho mawili ya matibabu", yani hakikisho la matibabu kwa ushirikiano wa kuchangia fedha kutoka kwa watu binafsi na serikali, na hakikisho la matibabu la fursa maalumu kwa "wazee wa aina tatu" mbali na serikali kuwapa yuan 10 kwa mwezi.

    Ofisa wa Idara ya Mambo ya Raia ya Wilaya ya Wulian alieleza, "Mahakikisho Mawili" yanamaanisha mambo matatu: moja ni kuwashirikisha "wazee wa aina tatu" katika bima ya afya vijijini, na pesa zao za bima zinachangiwa na serikali ya wilaya yuan 10 na watu binafsi wanalipa yuan 10. Asilimia 20 ya gharama za matibabu alizotoa mgonjwa zinarejeshwa, na asilimia 30 au 50 ya gharama za kulazwa mgonjwa anarejeshwa kutokana na hali tofauti. Pili ni fursa maalumu kwa "wazee wa aina tatu", nazo ni kuwa asilimia fulani ya gharama zinazobaki baada ya mgonjwa kurejeshewa zinagawanywa katika ngazi nne yaani gharama zilizo chini ya yuan 1000, zaidi ya yuan 1000 hadi 3000, na kutoka yuan 3000 hadi 5000, na kutoka yuan 5000 na kuendelea. Idara ya Mambo ya Raia wilayani inawalipia wagonjwa asilimia 50, 55, 60 na 65. Tatu ni mfuko wa misaada kwa watu wenye magonjwa sugu, yaani gharama za mwaka za kulazwa hospitali zikizidi yuan 5000 baada ya kurejeshewa gharama walizotumia kwa asilimia maalumu watapewa msaada wa yuan 2000 kwa mkupuo. Kwa sera hizo wazee hao wa aina tatu wanaweza kurejeshewa asilimia 65 hadi 84 ya gharama za matibabu. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, serikali ya wilaya ya Wulian iliwalipia wazee hao yuan laki 3.8 gharama za matibabu kwa jumla, watu 419 walilazwa hospitali na jumla ya fedha zilizotumika kwa matibabu zilikuwa yuan milioni 1.2, na fedha zilizorejeshwa kwa wagonjwa jumla zilikuwa yuan laki 9 na elfu 30, kwa wastani pesa zilizowarejeshwa kwa wagonjwa zilikuwa asilimia 75.3 ya gharama zote za matibabu.

    Habari kutoka Idara ya Mambo ya Raia ya Mkoa wa Shandong zinasema kuwa hivi sasa sera za "mahakikisho mawili" kwa ajili ya matibabu ya "wazee wa aina tatu" zimeanza kutekelezwa mkoani kote mkoani Shandong.

Idhaa ya Kiswahili 2004-08-05