Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-10 20:34:49    
Barua za Wasikilizaji 10/8/2004

cri
    Damas M. Bundala ambaye barua zake zinahifadhiwa na Mathias B. Kilima wa sanduku la Barua 52 Victoria, Mahe, Visiwa vya shelisheli. Ametuletea barua ikianza kwa salamu na kutueleza kuwa yeye hajambo. Anasema ni matumaini yake kuwa wasikilizaji wenzake na watangazaji nao ni wazima wa afya na wakiendelea vizuri na kazi ya utangazaji. Ukweli ndiyo huo sisi watangazaji hatujambo, ila tu kila siku tunakuwa na shughuli nyingi za ofisini na studio.

    Bwana Bundala anasema, anapenda kutushukuru kwa barua yetu tuliyomwandikia mwezi wa tatu ambayo tulimwuliza maswali mawili kuhusu bahasha tunazotuma na jingine kuhusu mtandao wa internet. Anasema hakuweza kujibu mapema kwani alikuwa kwenye mitihani. Kuhusu bahasha ambayo imekwisha lipiwa stempu, anasema mara ya kwanza alipkwenda kuulizia posta, mmoja wa wafanyakazi alimwambia kuwa hawezi kutumia, lakini alipokwenda tena hivi karibuni kuongea nao wakamwambia kwamba anaweza kuitumia.

    Anasema, kuhusu mtandao wa internet amejaribu na akapata, hivyo tovuti hiyo ya mtandao inapatikana na atakuwa akiendelea kusoma taarifa zetu na makala mbalimbali kupitia tovuti hiyo.

    Pia anaomba tumjulishe kama tumekwisha pata barua hii, pale itakapotufikia. Anasema anatutakia sote baraka na mafanikio mema katika shughuli zetu zote za kila siku. Nasi tunashukuru sana kwa barua yake na jibu lake ingawa ni fupi lakini ni la dhati sana. Pia tunashukuru kama bahasha tunazo mtumia zinakubalika katika posta ya huko Mahe, tunatumai kuwa mawasiliano yetu yatakuwa rahisi.

    Msikilizaji wetu mwingine Stephen Magoye Kumalija wa Shule ya msingi Kiliwi, sanduku la barua 1421 Mwanza, Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, anafuraha iliyoje kutuandikia barua hii akitumaini kuwa wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa hatujambo.

    Anasema anapenda kutupa pole sana kwa kupotelewa na marafiki zake wa China walioangukiwa na paa la nyumba huko Paris Ufaransa, katika sehemu ya uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris, pamoja na wachina waliofariki huko Kabul Afghanstan, waliokuwa wakifanya kazi ya kandarasi ambao waliuawa kwa kupigwa risasi.

    Vilevile pamoja na hayo yote, anasema hususan katika kipindi chetu cha sanduku la barua anaomba kama upo uwezekano anaomba muda uongezwa wa kipindi hicho cha sanduku la barua. Muda ambao upo kwa sasa hautoshi, muda ukiongezwa angalau dakika kama ishirini wataweza kusikiliza barua nyingi za wasikilizaji wa Redio China kimataifa zikisomwa. Mwisho anasema anautakia urafiki kati yake na wafanyakazi wote wa Redio China kimataifa uendelee na anatutakia kila la kheri na maisha mema katika mwa ka huu wa 2004.

    Tunamshukuru sana msikilizaji huyo kwa maoni yake kwa vipindi vyetu. Kuhusu kuongezwa muda wa kipindi cha hiki cha sanduku la barua, katika kipindi cha hivi karibuni huenda haitawezekana, kwani mpango wa matangazo yetu ulipangwa kutokana na mpango wa jumla wa Radio China kimataifa, si rahisi kwa sisi kuubadili. Lakini kutokana na hali halisi, katika siku za usoni, ombi lililotolewa mara kwa mara na wasikilizaji wetu kuhusu kuongeza muda wa vipindi vyetu litazingatiwa.

    Msikilizaji wetu mwingine Kilulu Kulwa wa Kijiji cha Benki Mtoni Kijichi, sanduku la barua 2503 Dar-es-salaam Tanzania ametuletea barua akisema, anatumai kuwa sisi sote wazima wa afya njema na tunaendelea vizuri na majukumu yetu ya kuwahudumia wasikilizaji. Anasema anaandika barua hii kwa furaha kubwa kwa kuwa matangazo yetu yamekuwa yakisikika vizuri sana katika sehemu mbalimbali za nchi yake ya Tanzania na Afrika mashariki kwa ujumla.

    Anatuambia kuwa kwa mara nyingine tena alikuwa na safari ya kikazi hapo Morogoro na pia katika jiji la Dar-es-salaam. Pamoja na shughuli za kikazi lakini hakukosa kusikiliza matangazo yetu ya idhaa ya kiswahili ya Redio China kimataifa, hivyo yote tuliyotangaza aliyasikia vizuri sana, na kwa sababu hiyo anapenda kutumia fursa hii kutoa shukurani zake za dhati kwa matangazo yetu ya kila siku tunayowatangazia wasikilizaji.

    Vile vile anapenda kutuambia kuwa alikisikiliza kwa makini kipindi cha sanduku la barua cha terhe 20/6 mwaka huu, anashukuru sana kwa kuwa tulinukuu barua zake na kuzisoma katika jumapili hizo hivyo anatushukuru sana. Kwa wakati huu anajiandaa kurejea huko Shinyanga, na atakapokuwa huko atatuandikia barua kutoa taarifa yake ya usikilizaji wa matangazo yetu.

    Vile vile anawasalimu na kuwapongeza sana wasikilizaji wenzake wanaofuatilia vipindi vyote vya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa kwa kutoa maoni yao na mapendekezo mbalimbali.

    Tunamshukuru sana Bwana Kilulu Kulwa, msikilizaji wetu wa tangu zamani sana ambaye pia ni rafiki yetu mzuri ambaye kila mara bila kujali yuko wapi, hawezi kusahau kufuatilia matangazo yetu, na kutusaidia kuwatia moyo wenzake kusikilizaji matangazo yetu na kutuletea maoni na mapendekezo mbalimbali. Na barua alizoandika huwa zinajaa uchangamfu na udhati ambazo hututia moyo wa kuchapa kazi na kuwahudumia zaidi wasikilizaji wetu.

Idhaa ya Kiswahili 2004-08-10