Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-12 20:58:56    
Tukumbuke mchango mkubwa wa mwanasiasa mashuhuri wa China

cri
    Tukumbuke mchango mkubwa wa mwanasiasa mashuhuri wa China

    Barani Afrika yuko mwanasiasa mmoja mwenye umri wa miaka zaidi ya 80 anayemkumbuka sana mwanasiasa mashuhuri wa China hayati Deng Xiaoping. Mwanasiasa huyo ni rais wa zamani wa Kenya Daniel Arap Moi.

    Huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya, kuna jengo moja jeupe lenye ghorofa mbili. Jengo hilo ni nyumba ya Mzee Moi. Baada ya kujua kuwa tutakwenda nyumbani kwake kwa ajili ya kumkumbuka Hayati Deng Xiaoping, Mzee Moi alivaa nguo zake kwa makini sana. Alivaa suti ya kijivu, shati jeupe lenye mistari miembamba ya rangi ya kibuluu, viatu vyekundu na ua waridi moja zuri kwenye mfuko wa suti yake. Nguo hizo ni sawa na nguo alizovaa alipokutana na Bw. Deng Xiaoping mjini Beijing.

    Mzee Moi alikuwa na mengi ya kusema alipomtaja Hayati Deng. Alisema kuwa katika miaka ya 80 karne iliyopita, aliwahi kufanya ziara nchini China na kukutana na Hayati Deng mara mbili. Alikumbuka vizuri uchambuzi alioufanya Deng Xiaoping kuhusu hali ya China ya wakati huo na matumaini yake kuhusu mustakabali wa China. Bw. Deng alimwambia kuwa alitaka kujenga China mpya ya kipekee. Ni kweli kuwa Mzee Deng alikuwa mwanasiasa hodari aliyeanzisha sera ya mageuzi na ufunguaji mlango nchini China.

    Kutokana na sauti kubwa na ishara nyingi za mikono, tuliweza kutambua kuwa Mzee Moi anamsifu sana hayati Deng Xiaoping. Alipotaja mazungumzo kati yake na hayati Deng, alisisimka sana akisema kuwa, "Mzee Deng alikuwa mtu wa kipekee, naweza kuona kuwa wananchi wa China wanamtukuza sana. Wakati huo, alikuwa akifikiria mustakabali wa China na njia ya maendeleo ya China. Alikuwa na imani kubwa kuhusu shabaha ya maendeleo ya China, na kutumai kuwa wananchi wa China wanaweza kupata maendeleo kwa nguvu zao wenyewe. Na sasa China imefanikiwa kutimiza lengo hili, na imekuwa nchi yenye nguvu kubwa ya kiuchumi."

    Mzee Moi alikuwa rais wa Kenya kwa miaka 24. Baada ya kustaafu mwaka 2002, alifanya kazi nyingi kwa ajili ya amani, utulivu na maendeleo ya Kenya na Afrika. Alipomkumbuka Bw. Deng Xiaoping, mara kwa mara aliona kuwa ingawa China iko mbali sana na Afrika, lakini mioyo ya watu wa sehemu hizo mbili iko karibu. Alisema kuwa siku zote Kenya ni rafiki wa China, na inashikilia sera ya kuwepo kwa China moja. Aliwahi kufanya ziara nchini China mara mbili. Sasa Kenya ina kituo cha michezo cha taifa, barabara za "China" na vifaa vingine vingi kutokana na misaada ya China. Jamhuri ya Watu wa China ina uhusiano barabara na Kenya.

    Alipotaja suala la amani na maendeleo, alieleza matumaini yake kuwa ataweza kuona Afrika yenye amani, kwani nchi yoyote na bara lolote haliwezi kupata maendeleo bila ya amani. Alitumai bara zima la Afrika litakuwa na amani siku za usoni, na China itatoa mchango mkubwa zaidi katika jambo hilo.

    Mzee Deng Xiaoping alipofariki dunia, Mzee Moi alituma salamu za pole akisema kuwa, Deng Xiaoping atakumbukwa na watu kama mwanzilishi wa mageuzi, ufunguaji mlango na maendeleo ya kisasa ya China ambaye alibadilisha China kuwa nchi yenye ongezeko kubwa kabisa la kiuchumi duniani. Mafanikio hayo yataendelea kusifiwa na dunia nzima, na yatakuwa ni urithi kwa China milele.

    Mzee Moi alisisitiza tena kuwa, "Mzee Deng Xiaoping aliipatia China mali ya thamani. Nina imani kubwa na wananchi wa China."

Idhaa ya Kiswahili 2004-08-12