Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-17 14:07:50    
Makala ya kwanza ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa "Miaka 55 ya China mpya"

cri

     Makala ya kwanza ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa "Miaka 55 ya China mpya"

                          Maendeleo endelevu ya Uchumi wa China

    Ifikapo tarehe mosi Oktoba mwaka huu, Jamhuri ya watu wa China itatimiza miaka 55 tangu kuzaliwa kwake. Katika miaka hiyo iliyopita, maendeleo ya haraka ya uchumi wa China yamevutia macho ya watu, aidha ongezeko la uchumi wa China pia limeweka msingi wa maendeleo ya sekta mbalimbali. Katika makala ya kwanza ya mashindano ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Miaka 55 ya China mpya, tunawafahamisha kuhusu maendeleo madhubuti ya uchumi wa China.

    Katika miaka 55 iliyopita, hatua ya mwanzo ya ujenzi wa China mpya ilitekelezwa katika hali yenye matatizo mengi. Kutokana na kukumbwa na uvamizi na unyang'anyi wa mabeberu kwa zaidi ya miaka mia moja; na kutokana na mapigano ya muda mrefu ya kupigania uhuru wa taifa na demokrasia ya umma, wakati Jamhuri ya watu wa China ilipoasisiwa karibu   sehemu zote nchini China zilikuwa zimeharibiwa vibaya, na shughuli za uchumi zilikuwa zimedidimia kabisa. Msingi wa viwanda vya China ulikuwa dhaifu sana, uzalishaji wa mazao ya kilimo ulikuwa wa chini sana, na upungufu wa bidhaa ulionekana nchini kote. Katika hali hiyo yenye taabu kubwa, wananchi wa China walianza kujenga taifa lao.

    Katika miaka 55 iliyopita, miaka 30 ya mwanzo Jamhuri ya watu wa China iliendelea kwa kufuata mfumo wa Urusi ya zamani, na utaratibu wa uchumi uliotekelezwa katika miaka hiyo 30 ulikuwa wa uchumi wa mipango ya taifa. Katika kipindi hicho, China ilipata maendeleo makubwa, na kiwango cha maisha ya wananchi pia kiliinuka kwa kiasi fulani. Lakini dosari katika uendelezaji wa uchumi wa mipango, zilileta matatizo mengi makubwa kwa uchumi wa China.

    Ilipofika mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, maendeleo ya uchumi wa China yalikutana na vikwazo vikubwa sana. Kuanzia hapo viongozi wa China walianza kufanya mageuzi ya kimsingi ya mfumo wa uchumi, yaani kuufanya mfumo wa mipango ubadilike kwa kuelekea kwenye uchumi wa soko huria wa ujamaa. Wakati huo huo katika hali ya uchumi wa kimataifa uliokuwa unalegalega, China ilianza kuzifungulia mlango zaidi nchi za nje katika sekta mbalimbali, hasa katika sekta ya uchumi.

    Mageuzi ya kiuchumi na ufunguaji mlango uliofanyika kuanzia mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, ulitia nguvu kubwa ya uhai kwa uchumi wa China na kuuwezesha uchumi wa China uendelee kwa haraka sana. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Idara ya takwimu ya China, katika kipindi cha miaka 25 kuanzia mwaka 1978 hadi 2003, wastani wa ongezeko la uchumi wa China ulikuwa ni zaidi ya asilimia 9 kwa mwaka.

    Ongezeko la uchumi kwa miaka mingi mfululizo liliweka msingi kwa serikali kuboresha maisha ya wananchi. Katika zaidi ya miaka 20 iliyopita, serikali ya China iliwawezesha wananchi wake zaidi ya milioni 200 kuondokana na umaskini. Hivi sasa idadi ya watu wa China imefikia bilioni 1.3, na kwa mara ya kwanza, mwaka jana wastani wa pato la kila mwananchi ulizidi dola za kimarekani 1000.

    Maendeleo ya uchumi wa China yanasifiwa na watu kadhaa mashuhuri wa idara za uchumi duniani. Profesa wa Chuo kikuu cha Pennsylvania cha Marekani Bwana Lawrence Klein ambaye aliwahi kupata tuzo ya Nobel ya elimu ya uchumi alipozungumzia maendeleo ya uchumi wa China alisema: Ukienda China, na kujionea barabarani mabadiliko makubwa yaliyotokea katika maisha ya watu, hakika utaona kuwa ongezeko la haraka la uchumi wa China ni ukweli wa mambo.

    Katika mchakato wa maendeleo, uchumi wa China unajiunga na uchumi wa dunia siku hadi siku, na China inazifungulia mlango nchi za nje siku hadi siku katika sekta ya uchumi. Mwaka 2001, China ilijiunga na Shirika la biashara duniani WTO, na hivi sasa China inafanya mazungumzo na Umoja wa Asia ya kusini mashariki kuhusu kuanzisha sehemu ya biashara huru.

    Wakati huo huo China inajitahidi kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya pande mbilimbili au pande nyingi na Marekani na Umoja wa Ulaya. Katika miaka ya hivi karibuni, kiwango cha jumla cha ushuru wa forodha nchini China kimekuwa kikipungua siku hadi siku, wastani wa ushuru ulipungua na kufikia asilimia 10.4 za sasa kutoka asilimia 15.3 ya mwaka 2001 kabla ya kujiunga na WTO.

    Kuhusu biashara na nje, katika mwaka 2003 thamani ya biashara ya China na nje ilikuwa ni zaidi ya dola za kimarekani bilioni 800, ilichukua nafasi ya 4 duniani ikizifuata Marekani, Ujerumani na Japan. Na kwa ujumla, ilipofika mwezi wa Juni mwaka huu, thamani ya vitega uchumi vya nje nchini China ilikuwa ni zaidi ya dola za kimarekani bilioni 500.

    Mwaka 2002 na 2003, kwa miaka miwili mfululizo, China ilikuwa nchi iliyovutia vitega uchumi vingi zaidi kutoka nje kuliko nchi nyingine zote duniani. Wakati huo huo uagizaji wa bidhaa kutoka nchi za nje na uwekezaji wa China katika nchi za nje pia umekuwa ukiongezeka zaidi siku hadi siku. Hivi sasa China imekuwa nchi ya tatu ya uagizaji wa bidhaa duniani na ni nchi ya 5 duniani yenye vitega uchumi vingi katika nchi za nje.

    Katika hali hiyo, viongozi wa China waliahidi mara kwa mara kuwa, China itaendelea kufungua soko lake kwa dunia nzima. Siku chache zilizopita, naibu waziri mkuu wa China Bibi Wu Yi aliahidi kwenye mkutano mmoja wa uchumi duniani akisema: Kuzifungulia mlango zaidi nchi za nje ni sera ya kimsingi inayofuatwa na serikali ya China kwa muda mrefu, China itainua kiwango cha ufunguaji mlango kwa nje katika sekta mbalimbali, kufuta hatua za ushuru usio wa forodha siku hadi siku, na kupanua eneo la uwekezaji kwa wafanyabiashara wa nje.

    Habari zilisema kuwa, China italegeza zaidi masharti ya kuruhusu kuingia katika soko la mawasiliano ya posta na simu, benki, bima, pamoja na mauzo ya rejareja. Katika miaka ya hivi karibuni, wakati shughuli za uchumi zikiendelea kupanuliwa, njia ya ongezeko la uchumi wa China pia inabadilika, ambapo shughuli ambazo zinatumia nishati kupita kiasi au haraka, ama kuleta uchafuzi zaidi kwa mazingira zimezuiliwa, na mikakati ya maendeleo endelevu inatekelezwa kwa uhalisi. Naibu mkuu wa Idara ya takwimu ya China Bwana Qiu Xiaohua akifahamisha alisema: Shughuli zinazotegemewa kuleta ongezeko la uchumi siyo shughuli zile za jadi zinazohitaji nguvukazi nyingi sana, hivi sasa shughuli za kuwekeza mitaji mingi na zenye teknolojia nyingi zimeanza kuwa shughuli muhimu sana zinazotegemewa katika kuleta ongezeko la uchumi wa China. Shughuli za upashanaji habari za elektroniki, shughuli za ujenzi wa makazi na shughuli za utengenezaji wa magari zimekuwa nguvu muhimu ya kusukuma mbele ongezeko la uchumi wa China.

    Kuhusu uhusiano kati ya uchumi wa China na uchumi wa dunia, watu wengi wa idara za uchumi wanasema kuwa, ongezeko la uchumi wa China linasaidia kuleta usitawi na maendeleo ya uchumi wa dunia. Dk He Fan wa Idara ya utafiti wa uchumi na siasa ya dunia katika Taasisi ya sayansi ya jamii ya China ana maoni kama hayo, alisema:

    Kutokana na hali ya ujumla tunaweza kuona kuwa, maendeleo ya China yamesukuma mbele uchumi wa dunia nzima. Kwa upande mmoja, kujitokeza kwa China kunasaidia nchi zilizoendelea kuharakisha marekebisho ya miundo ya uzalishaji wa bidhaa nchini mwao, na kuzipatia nafasi nzuri za uwekezaji; kwa upande mwingine, kujitokeza kwa China pia kumeleta fursa nyingi zaidi kwa nchi zinazoendelea zilizoko pembezoni mwa China.

   Wapenzi wasikilizaji, mpaka sasa tumekwisha waelezea hali kuhusu maendeleo ya uchumi wa China katika miaka 55 iliyopita tangu kuzaliwa kwa China mpya. Sasa tunawataka msikilize kwa makini na mjibu maswali mawili yafuatayo:

   La kwanza. Katika kipindi cha miaka 25 kuanzia mwaka 1978 hadi 2003 wastani wa ongezeko la uchumi wa China kwa mwaka ulikuwa ni zaidi ya asilimia ngapi?

   La pili, Kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, serikali ya China imewawezesha wananchi wake wangapi kuondokana na umaskini?

   Katika kipindi kijacho tutawaletea makala ya pili ya kuwafahamisha hali ya maendeleo kwenye mambo ya elimu katika China mpya.