Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-17 16:48:02    
China yachukua hatua kutatua tatizo la upungufu wa umeme

cri

    Ni zaidi ya siku kumi zimepita tangu mji wa Wuxi, ulioko sehemu ya mashariki ya China, kuwa na hali ya nyuzijoto zaidi ya sentigredi 35. Licha ya kusumbuliwa na joto kali, wakazi wa mji huo pia waliokumbwa na tatizo la upungufu wa umeme. Katika Hoteli ya Ziwa la Tai ya mji huo, meneja bibi Fang Yuejing alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa kutoka na upungufu wa umeme, hoteli yao haina budi kupunguza matumizi ya umeme hadi kiwango cha chini kabisa.

    "Ikifika usiku, tunazima taa za kumulika jengo la hoteli zilizowekwa nje. Hali ya joto ndani ya hoteli imedhibitiwa katika nyuzi 16 za sentigredi; Milango yote ya vyumba na iliyoko katika njia za ndani ya hoteli inafungwa kila wakati ili kuzuia hewa baridi ya ndani isiende nje kwa lengo la kupunguza matumizi ya umeme. Kila siku tunakagua mara tatu hali ya kupunguza matumizi ya umeme."

    Kiongozi mmoja wa mji wa Wuxi alisema kuwa mashirika yanayohusiana na wageni yamesaidiwa na sera za serikali ya mji. Katika majira ya joto ya mwaka huu, umeme unaotolewa na mfumo wa umeme wa mkoa wa Jiangsu kwa mji wa Wuxi ni theluthi mbili tu ya mahitaji yake. Ili kuhakikisha kuwa wakazi wanapata umeme kama kawaida, viwanda vya kawaida vinafanya kazi siku nne na kupumzika siku tatu. Baadhi ya mashirika yamewapa likizo wafanyakazi wao.

    Nchini China hivi sasa kuna zaidi ya mikoa 20 iliyopewa kikomo cha matumizi ya umeme, ambayo ni zaidi ya theluthi mbili ya jumla ya idadi ya mikoa yote ya China. Kutokana na takwimu za shirika la umeme la China, upungufu wa umeme umefikia kilowati milioni 30, kiasi hicho ni zaidi ya kiasi cha uzalishaji wa umeme wa nchi moja ya wastani. Mji wa Wuxi uko katika sehemu ya mashariki ya China, ambayo ni sehemu iliyokumbwa zaidi na upungufu wa umeme. Upungufu wa umeme wa sehemu hiyo umefikia kiasi cha 60% ya upungufu wa umeme wa nchi nzima. Ili kupunguza matumizi ya umeme, taa zote mjini Shanghai zinazotumika kama mapambo wakati wa usiku katika kupamba majengo yaliyoko katika kando mbili za mto Huangpu zimezimwa, na ziwa la Magharibi la mji wa Hangzhou, ambalo ni mandhari maarufu ya utalii, hivi sasa linafunikwa na giza wakati wa usiku.

    Katika miaka michache iliyopita, hakukuwa na tatizo la umeme hata kidogo hapa nchini. Lakini tokea mwaka jana, baadhi ya mikoa ya China ilianza kudhibiti matumizi ya umeme. Mwaka huu, hali ya upungufu wa umeme imekuwa mbaya zaidi. Lakini ni kwa nini hali hiyo inatokea? Mhandisi mkuu wa kamati ya usimamizi wa umeme ya taifa Bw. Yu Xinyang alieleza,

    "Mwaka 1997, kulikuwa na hali ya kulingana kati ya mahitaji na uzalishaji wa umeme, na ilipofika mwaka 1998 na mwaka 1999, uzalishaji wa umeme ulikuwa mwingi zaidi kuliko mahitaji. Lakini kutokana na maendeleo ya kasi ya uchumi katika miaka ya karibuni, hususan kuanzishwa kwa baadhi ya sekta za uzalishaji bidhaa zinazotumia umeme kwa wingi katika baadhi ya mikoa, hali ya upungufu wa umeme ikaanza kutokea."

    Bw. Yu alisema kuwa kasi ya maendeleo ya uchumi wa China ilikuwa kubwa kuliko kasi ya ujenzi mitambo ya kuzalisha umeme. Hiyo ni sababu muhimu iliyoleta hali ya upungufu wa umeme. Sababu ya pili ni kuwa idara husika hazikuweza kukadiria barabara ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme kutokana na maendeleo ya kasi ya uchumi. Katika miaka fulani idara hizo zilipunguza miradi ya ujenzi wa mitambo ya uzalishaji wa umeme, hali ambayo imesababisha ujenzi wa miradi ya uzalishaji wa umeme kushindwa kufuata kasi ya ongezeko la uchumi. Kwa mfano mfumo wa umeme wa sehemu ya kaskazini ya China ambao kati ya mwaka 2001 na mwaka 2003, ulikuwa na uwezo wa kuzalisha kilowati milioni 3 za umeme, ulikuwa na ongezeko la 10%, lakini katika kipindi hicho, ongezeko la mahitaji ya umeme lilikuwa zaidi ya 20%.

    Aidha, maendeleo ya kasi ya baadhi ya sekta za uzalishaji mali zinazotumia umeme kwa wingi ikiwa ni pamoja na viwanda vya kuzalisha aluminium, kuyeyusha madini na kemikali, yamezidisha hali ya upungufu wa umeme. Sababu nyingine ni kuwa joto kali katika majira ya joto ya mwaka jana na mwaka huu limewafanya wakazi wengi kununua Viyoyozi, hali ambayo imechangia upungufu wa umeme.

    Kuhusu hatua zinazochukuliwa ili kubadilisha hali ya upungufu wa umeme, wataalamu wanasema kuwa, kwa kuwa ujenzi wa viwanda vya uzalishaji unahitaji muda ikiwa ni pamoja na kuchagua mahali, majadiliano, uidhinishaji na ujenzi, kwa hivi sasa hatua inayoweza kuchukuliwa ni kuimarisha usimamizi wa mifumo ya umeme, kuharakisha ujenzi wa miradi ya uzalishaji wa umeme inayojengwa sasa, ili kupunguza tatizo la upungufu wa umeme.

    Naibu mkurugenzi wa ofisi utendaji ya meneja mkuu wa kampuni ya mifumo ya umeme ya China Bw. Wang Guanghui alisema kuwa suala kubwa la kwanza ni kuhakikisha kuwa wakazi wanapata umeme, na uzalishaji wa mazao ya kilimo usiathiriwe na tatizo la upungufu wa umeme. Kwa upande mwingine, tunapaswa kudhibiti matumizi ya umeme ya viwanda vinavyotumia umeme kwa wingi, lakini uzalishaji wake ni mdogo. Hivi sasa tumefikiria kutumia ziada ya umeme ya mifumo mingine nchini ili kupunguza tatizo la upungufu wa umeme. Alisema,

    "Ili kukabiliana na hali ngumu ya upungufu wa umeme, tumeimarisha usimamizi na kutumia uwezo wetu ambao bado haujatumika, kuimarisha nguvu ya ujenzi wa mifumo ya umeme, na kujitahidi kupambana na matatizo ya upungufu wa umeme ya mwaka huu kwa kushirikiana na vituo vingine vya uzalishaji umeme."

    Hata hivyo, wataalamu wanasema kuwa hata hivyo hatua hizo bado haziwezi kutatua kabisa tatizo la upungufu wa umeme. Habari zinasema kuwa mbali na miradi mikubwa ya ujenzi wa vituo vya kuzalisha umeme wa mikoa, hivi sasa serikali kuu inajenga mradi wa kuzalisha umeme wenye uwezo wa kilowati milioni 139 za umeme, kiasi hicho ni theluthi moja ya uwezo wa hivi sasa wa kuzalisha umeme. Hivyo, wataalamu wanasema kuwa baada ya miaka mitatu hivi, hali ya upungufu wa umeme itapunguzwa kwa kiwango kikubwa.

Idhaa ya Kiswahili 2004-08-17