Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-19 19:46:06    
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa apendekeza kuongeza jeshi la kulinda amani nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo

cri

    Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan jana alitoa ripoti kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akipendekeza kuongeza idadi ya askari wa jeshi la kulinda amani nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, ili kuliwezesha jeshi hilo kusaidia serikali ya mpito ya nchi hiyo kuimarisha mchakato wa amani, na kuandaa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utakaofanyika mwezi Juni mwakani.

    Katika ripoti hiyo, Bw. Kofi Annan alisema kuwa, katika miezi michache iliyopita, mchakato wa amani wa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo umekabiliana na changamoto kubwa: vita vililipuka tena katika sehemu ya mashariki ya nchi hiyo, na pia kulitokea jaribio la uasi. Matukio hayo yanaonesha kuwa mchakato wa amani wa nchi hiyo bado haujawa imara, kama mazungumzo ya kisiasa kati ya pande husika hayawezi kupata maendeleo makubwa, mchakato wa amani wa nchi hiyo utakuwa na hatari ya kuvunjika.

    Bw. Annan alisema kuwa, ili kuzuia migogoro, jeshi la Umoja wa Mataifa nchini humo lazima liwe na eneo muhimu la kuendesha shughuli za kulinda amani. Mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa, mji wa mashariki Kivu, na mji wa kusini Kananga lazima yawe maeneo muhimu la kulinda amani. Jeshi la kulinda amani lazima liongezwe nguvu sehemu hizo. Hivyo, amependekeza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liongeze jeshi la kulinda amani kwa askari elfu 13, wakiwa ni pamoja na wachunguzi 760 wa kijeshi na polisi 367. Pia alipendekeza kuandaa ndege nyingi zaidi za uchukuzi, helikopta na zana za mawasiliano kwa jeshi hilo, ili kuongeza uwezo wake wa kukabiliana na hali ya dharura.

    Bw. Annan pia alitaka nchi zilizoendelea kujifunza kwa nchi zinazoendelea, kupeleka jeshi kwenye sehemu hizo ili kuitikia mpango wa Umoja wa Mataifa kuongeza jeshi la kulinda amani.

    Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio mwezi Julai mwaka huu, likifuatilia mgogoro kwenye mchakato wa amani, na kutaka Bw. Kofi Annan kutoa mapendekezo kuhusu kuongeza uwezo wa jeshi la kulinda amani. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka nchini humo mwezi Julai mwaka 1998. mwazoni mwa mwaka 2000, Umoja wa Mataifa ulianza kupeleka jeshi la kulinda amani nchini humo, mpaka sasa kwa ujumla Umoja wa Mataifa umepeleka wanajeshi elfu kumi na mia tano wa kulinda amani nchini humo.