Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-20 20:23:28    
China Kujenga uwanja mpya wa kisasa nchini Tanzania

cri

    Mwezi juni mwaka huu ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa, ulikuja nchini China kuhudhuria mkutano wa Biashara uliofanyika huko Shanghai. Baada ya kumalizika mkutano huo, ujumbe huo ulitembelea miji mingine ya hapa China kufanya ziara, ikiwa ni pamoja na mji wa Beijing.

    Moja kati ya mambo uliyofanya ujumbe huo hapa Beijing, ni kutia saini mikataba mbalimbali ya biashara kati ya China na Tanzania. Moja kati ya mikataba hiyo ni mkataba unaohusu ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo, uliotiwa saini na waziri wa mambo ya nje wa China Bwana Li Zhaoxing na waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania Jakaya Kikwete.

    Kutiwa saini kwa mkataba huo kunatokana na taratibu nyingi zilizofanyika nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na kutangaza zabuni ya ujenzi wa uwanja huo kwa kampuni kubwa mbalimbali. Kampuni kubwa mbalimbali za ujenzi zilishiriki kwenye zabuni hiyo. Kampuni mbili kati ya hizo zilikuwa mbioni kushinda Zabuni hiyo, moja ikiwa ni kutoka Ufaransa na nyingine ikiwa ni kutoka Uholanzi.

    Kampuni ya Ufaransa iliweka kiwango kikubwa sana cha fedha kwa hiyo haikuwa chaguo la Tanzania. Hata kampuni iliyokuwa imeweka kiwango kidogo cha fedha, bado kiwango ilichokuwa imeweka kilikuwa ni kikubwa zaidi ya matarajio ya matumizi ya Tanzania.

    Hata hivyo nia ya watanzania ya ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo haikufa. Baada ya kuona mlango mmoja umefungwa wakaamua kutumia mlango mwingine. Na mlango huu ni mahusiano mazuri ya kidiplomasia yaliyopo kati ya Tanzania na nchi ambazo zimebobea katika masuala ya ujenzi wa viwanja.

    Bila shaka Tanzania na China ni nchi marafiki wa kubwa, na haikuwa vigumu kwa Tanzania kuieleza China nia yake ya ujenzi wa uwanja wa kisasa na matatizo yaliyojitokeza katika kufanikisha lengo. Hili halikuwa gumu kwa China, kwani China ina uzoefu mkubwa sana katika ujenzi wa viwanja vya michezo. Baada ya kuangalia hali ya fedha na usanifu wa uwanja huo mwezi juni mwaka huu serikali ya China na Tanzania zikasaini makubaliano ya ujenzi wa uwanja huo. Kilichokuwa kikisubiriwa ni utekelezaji makubaliano hayo.

    Mwishoni mwa mwezi Julai ujumbe wa watu tisa kutoka Tanzania ulikuja hapa Beijing kushughlikia suala hilo. Mwandishi wa habari wa Radio China Kimataifa alipata fursa ya kuongea na mkuu wa msafara huo ambaye ni mkurugenzi wa Michezo, Wizara ya kazi, vijana na maendeleo ya michezo wa Tanzania Bw Henry Ramadhani, ambaye kwanza alianza kueleza lengo la ujio wao hapa Beijing.

    Ujenzi wa uwanja huo utakamilisha kazi ya China ya kujenga viwanja vya kisasa vya michezo katika miji mikuu yote ya nchi za Afrika Mashariki. Uwanja wa Kasarani mjini Nairobi Kenya, na uwanja wa Nelson Mandela mjini Kampala nchini Uganda vimejengwa na china. Hata katika nchi za Afrika magharibi viwanja vingi michezo vimejengwa na kampuni za China. Miradi ya ujenzi wa viwanja vya michezo, ni moja ya maeneo yanayoonesha uhusiano mkubwa uliopo kati ya China na nchi za Afrika.