Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-24 21:04:14    
Elimu ya China inayowahudumia wachina bilioni 1.3 (sehemu A)

cri

    Katika makala ya kwanza tulipowafahamisha kuhusu hali ya uchumi wa China tulisema kuwa, kabla ya miaka 55 iliyopita Jamhuri ya Watu wa China ilianza ujenzi wa nchi ikiwa na msingi dhaifu sana katika sekta zote. Wakati huo hali ya maendeleo ya elimu ilikuwa nyuma sana, asilimia 80 ya wachina kati ya watu milioni 450, walikuwa hawajui kusoma na kuandika.

    Hivi sasa idadi ya wananchi wa China imeongezeka na kufikia bilioni 1.3. Idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika imepungua na kuwa asilimia 6 ya idadi ya jumla ya watu wa China. Lakini asilimia hiyo 6 inamaanisha kuwa kuna watu zaidi ya milioni 70 nchini China ambao hawajui kusoma wala kuandika. Serikali ya China inapaswa kufanya juhudi kubwa ili kuendeleza elimu.

    China ni nchi yenye eneo kubwa. Kutokana na hali tofauti ya maendeleo katika sehemu mbalimbali, kiwango cha maendeleo cha sehemu ya mashariki ni kikubwa zaidi kuliko sehemu ya magharibi. Katika sekta ya elimu, hali hiyo inaonekana pia kwa udhahiri. Miongoni mwa watu zaidi ya milioni 70 wasiojua kusoma wala kuandika, wengi zaidi wanaishi katika sehemu ya magharibi. Idadi ya watoto waliokwenda shule na wanafunzi waliofuzu kwenda katika shule za sekondari au vyuo vikuu katika sehemu ya magharibi, ni ndogo zaidi kuliko ile ya sehemu ya mashariki na sehemu ya kati. Aidha, katika kiwango cha maendeleo ya elimu katika sehemu za vijijini pia ni cha chini kuliko kile cha mijini nchini China.

    Ilipofika mwaka jana, asilimia 91 ya sehemu za China ilikuwa imetimiza elimu ya lazima ya miaka 9, na asilimia 9 iliyobaki ni ya sehemu za magharibi. Mawasiliano katika sehemu hizo za magharibi ya China ni magumu, hali ya mazingira ya kimaumbile ni mbaya, pia kuna matatizo mengi katika kuendeleza uchumi, hata watu wengi wa huko bado hawawezi kujitosheleza kwa chakula, familia nyingi hazijawa na uwezo wa kuwawezesha kuwapata watoto nafasi za kwenda shule, na vijiji na wilaya kadhaa hazina fedha za kujenga shule rasmi.

    Kutokana na hali hiyo, katika miaka ya hivi karibuni serikali ya China imekuwa ikitenga fedha nyingi ili kuendeleza elimu katika sehemu hizo. Waziri wa elimu wa China Bwana Zhou Ji alifahamisha katika mkutano mmoja akisema:

    Katika miaka ya hivi karibuni, fedha zinazotolewa na serikali ya China katika mambo ya elimu zimekuwa zikiongezeka haraka, na kuchukua asilimia 3.4 kutoka asilimia 2.5 ya thamani ya uzalishaji wa bidhaa nchini China.

    Kuanzia mwaka jana, China ilitenga fedha nyingi zaidi katika kuendeleza elimu vijijini, kuongeza kazi ya ukarabati wa majengo ya shule za vijijini, na kuendeleza elimu ya upashanaji habari, ambapo watoto wa familia nyingi zenye matatizo ya kiuchumi wanapata misaada ya vitabu na misaada mingine bila malipo. Hatua hizo zimeboresha hali ya elimu ya sehemu kubwa ya vijiji vikiwemo vijiji vya sehemu ya magharibi.

    Waziri wa elimu wa China Bwana Zhou Ji alifahamisha kuwa, kuendeleza elimu ya vijiji vya sehemu ya magharibi ya China, ni kazi kubwa zaidi katika kuendeleza elimu ya China katika miaka kadhaa ijayo. Serikali ya China itatenga fedha nyingi zaidi katika kuendeleza elimu ya vijiji vya sehemu ya magharibi ya China. Bwana Zhou alisema:

    Katika miaka kadhaa ijayo, fedha zaidi zitakazotengwa na serikali ya China zitatumika katika kuimarisha elimu vijijini, hasa elimu ya lazima vijijini. Katika miaka kadhaa ijayo, serikali ya China kila mwaka itatenga fedha za renminbi Yuan bilioni 10 kwa ajili ya elimu katika vijijini vya sehemu ya magharibi ya China. Ongezeko kubwa la bajeti hiyo limeonesha nia ya serikali kuu ya kufanikisha maendeleo ya elimu ya sehemu ya magharibi, hasa kuimarisha elimu ya msingi ya sehemu ya magharibi.