Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-26 19:39:41    
Matumizi ya nishati mpya yana mustakbali mzuri nchini China

cri

    Wakati soko la mafuta duniani likiwa linayumba yumba na katika baadhi ya miji ya China kuna mgao wa umeme, wataalamu wa nishati wa China wameanza kuzingatia kuendeleza nishati mpya na nishati zinazoweza kutumika tena. Utafiti uliofanywa na wataalamu hao unadhihirisha kuwa matumizi ya nishati mpya nchni China yana mustakbali.

    Katika siku zijazo, China itaendeleza kwa nguvu nishati zinazoweza kutumika tena na nishati mpya kama vile nishati ya upepo, nishati ya jua, nishati ya joto chini ya ardhi na nishati ya viumbe. Ifikapo mwaka 2015, matumizi ya nishati hizo yatachukua asilimia 2 ya matumizi ya jumla ya nishati nchini China.

    Mkurugenzi wa ofisi ya mpango wa kuendeleza nishati zinazoweza kutumika tena katika Kamati ya mageuzi na maendeleo ya China Bw. Zhou Fengqi alisema kuwa, China inatunga sheria ya kuhimiza maendeleo ya nishati zinazoweza kutumika tena, ili kuhimiza matumizi makubwa ya nishati hizo.

    China ina nishati mpya nyingi na nishati zinazoweza kutumika tena. Takwimu husika zinaonesha kuwa, eneo linalopata mwanga wa jua kwa saa zaidi ya 2200 kwa mwaka ni zaidi ya theluthi mbili ya ardhi yote, hivyo China ina hali nzuri na thamani kubwa ya kuendeleza nishati hiyo.

    Utafiti uliofanywa na taasisi ya nishati ya China unaonesha kuwa, tukitupia macho kipindi kirefu cha siku za usoni, matumizi ya nishati mpya na nishati zinazoweza kutumika tena yanaweza kuboresha hatua kwa hatua miundo ya nishati ambayo inachukua makaa ya mawe kama nishati kuu, kuhimiza utumiaji unaofaa zaidi wa nishati za kawaida, kupunguza tatizo la mazingira linalohusika na nishati, na kuyawezesha maendeleo ya nishati, uchumi na mazingira yaende sambamba na kutimiza lengo la maendeleo endelevu.

    Kwa hali ya hivi karibuni, maendeleo ya nishati mpya na nishati zinazoweza kutumika tena yanaweza kuongeza na kuboresha utoaji wa nishati, pia yanafanya kazi muhimu sana katika kutatua tatizo la upungufu wa umeme na nishati katika sehemu za mipakani na visiwani.

    Makadirio yanaonesha kuwa, ifikapo mwaka 2015, matumizi ya nishati mpya na nishati zinazoweza kutumika tena yatapunguza utoaji wa hewa chafu, kuleta nafasi laki 5 za ajira na kutatua tatizo la ukosefu wa umeme kwa familia zaidi ya milioni 5 za wakulima na wafugaji wa sehemu za mbali.

    Maendeleo na matumizi ya nishati mpya na nishati zinazoweza kutumika tena yameanza kushindaniwa na wawekezaji vitega uchumi mbalimbali nchini China.

    Hivi karibuni, katika mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani ambapo kuna utajiri wa rasilimali ya nishati ya upepo, shirika moja la Canada na mji wa Er Lian Hao Te zimetia saini kwenye mkataba, zikipanga kujenga uwanja mkubwa kabisa barani Asia wenye uwezo wa kuzalisha kilowati milioni 10 za umeme kwa nishati ya upepo.

    Lakini utafiti uliofanywa na taasisi ya nishati ya China pia unadhihirisha kuwa, kutokana na hali ya jumla, shughuli za nishati mpya hazina nguvu kubwa na uwezo wake wa ushindani ni dhaifu, baadhi ya matatizo makubwa yanayozuia maendeleo ya shughuli hizo bado hayajatatuliwa kikamilifu, na kutakiwa kuharakisha maendeleo ya teknolojia na ubunifu wa mfumo mpya, ili kusukuma mbele maendeleo ya shughuli hizo kwa kasi.