Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-26 19:42:37    
Maisha mazuri ya familia kutoka Korea ya kusini mjini Hangzhou

cri

    Hangzhou ni mji mkuu wa mkoa wa Zhejiang ulioko mashariki mwa China wenye mandhari mazuri, chakula kitamu, mazao mengi ya kilimo, na hali nzuri ya utamaduni, ambao husifiwa kuwa ni kama peponi kwa binadamu. Kutokana na China kuendelea kufungua mlango kwa nchi za nje, wageni wengi zaidi wanakwenda mkoani Zhejiang kufanya kazi, kusoma na kuishi mjini humo. Katika kipindi hiki cha leo, tutawaeleza jinsi Bwana Kim Gyeong Seok na familia yake kutoka Korea ya kusini wanavyoishi kwa furaha mjini Hangzhou.

    Miaka mitano iliyopita, Bwana Kim Gyeong Seok na mke wake Bibi Hue Jung Suk walifika Hangzhou pamoja na mabinti zao wawili. Bwana Kim Gyeong Seok ni msanii, yeye ni mwembamba na mpole. Muda si mrefu uliopita, alipata shahada ya pili kutoka kwenye idara ya sanaa ya ufinyanzi wa udongo ya Chuo Kikuu cha Sanaa cha China. Bibi Hue Jung Suk anawahudumia watu wote katika familia yake nyumbani, lakini katika kipindi cha hivi karibuni amekuwa akijishughulisha na matayarisho ya maonesho ya kazi za sanaa ya bwana yake. Baada ya kuishi nchini China kwa miaka mingi, wote wanaweza kuongea vizuri kichina. Bibi. Hue alisema:

    "Tumeishi nchini China kwa miaka 8, mwanzoni tulikuwa tunaishi mjini Tianjing. Kwa sababu mume wangu anashughulikia mambo ya sanaa, hivyo mimi pia napenda utamadani. Mji wa Hangzhou unatufaa sana kwa kuishi."

    Walipotaja mji wa Hangzhou, Bwana Kim na mke wake wote walikuwa na mengi ya kuzungumza. Kutokana na kupenda utamaduni na sanaa za China, baada ya kumaliza masomo ya shahada ya kwanza nchini Korea ya kusini, Bwana Kim aliamua kuja China kujifunza Kichina. Anasema ilikuwa ni bahati kuuchagua mji wa Hangzhou kuendelea na masomo yake ya shahada ya pili, kwa sababu wanaupenda sana mji wa Hangzhou, alisema:

    "Mji wa Hangzhou ni kama picha inayoonesha mandhari ya milima na maji, ni mahali penye mvuto mkubwa. Chuo kikuu nilichosoma kiko karibu na ziwa Xihu linalopendeza. Napenda kuishi katika mji huu kwa sababu napenda sana utaratibu wa maisha ya hapa, utaratibu wa maisha ya kwetu Korea ya kusini ni wa haraka sana, lakini hapa Hangzhou, kila siku nafanya kazi, lakini nahisi kama napumzika."

    Bibi Hue jung Suk anapenda kucheka, kila anapoongea hutabasamu kwa upole. Licha ya kufanya kazi za nyumbani, yeye pia anawafundisha wakazi wa Hangzhou lugha ya Kikorea, na kushughulikia maingiliano ya utamaduni kati ya China na Korea ya kusini. Alisema kuwa, anafurahia utamaduni wa China, vile vile anataka kufikisha utamaduni wa Korea ya kusini nchini China kwa maingiliano yasiyo ya kiserikali kama vile, wakati wa likizo ya mchipuko, aliendesha shughuli za maingiliano ya utamaduni ya China na Korea ya kusini kwa wiki moja katika shule moja ya msingi, kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kutengeneza achali, kuwafahamisha mavazi, sanaa, na nyumba za Korea ya kusini. Siku ya mwisho tuliandaa maonesho. Wanafunzi walipeleka nyumbani achali za kikorea walizotengeneza, na kula pamoja na wazazi wao na wote walifurahi."

    Mabinti wao wote wawili wanasoma kwenye shule moja ya msingi, mwaka huu binti yao wa kwanza ana umri wa miaka 13, wa pili ana miaka 12. Shuleni, hawana tofauti na wanafunzi wenyeji wa China, wanaongea kichina vizuri. Lakini wakifika nyumbani tu, wanaongea kikorea wakichanganya na kichina, na kujifunza historia na utamaduni wa Korea ya kusini. Bibi. Xu alisema:

    "Binti yangu wa kwanza anajifunza kutumia kinanda cha Erhu, wa pili anajifunza kupiga kinanda cha Guzhen, ambavyo vyote ni vinanda vya kijadi vya China. Tunathamini sana utamaduni wa China, hivyo tunataka kila mmoja ajifunze ala moja ya muziki. Kila inapofika wekiendi, huwa nawapeleka watoto kutembelea jumba la makumbusho, au nyumba ya sanaa. Wakiwa na nafasi, tunawapeleka kwenye karakana ya baba yao, kuchezea udongo na kujifunza kutengeneza sanamu kwa mikono. Tuko tayari kufanya maonesho ya sanaa walizotengeneza wanapomaliza masomo ya shule ya msingi."

    Machoni mwa Bi. Hue, wakati wenye furaha mno kwao ni wakati wa kutembea kando ya ziwa la Xihu wakipunga upepo na kujiburudisha kwa mandhari nzuri ya usiku baada ya chakula cha jioni kama wakazi wenyeji. Bi. Hue alisema:

    "Tunaishi kando ya ziwa Xihu. Tukimaliza chakula cha jioni, huenda kutembea kando ya ziwa tukiambatana na mabinti zetu, na kujiburudisha kwa mandhari nzuri ya ziwa Xihu. Wakati mvua inaponyesha na kuangusha theluji katika majira ya joto na majira ya baridi, uzuri wa ziwa Xihu unatofautiana kila majira. Tunakwenda kunywa chai, kutembea, kufanya mazoezi kando ya ziwa Xihu, ziwa Xihu linaonekana kuwa na mandhari tofauti wakati wa asubuhi, mchana na usiku."

    Bibi Hue alisema kuwa, mjini Hangzhou, mabasi yanafika kila mahali, lakini yeye bado anapenda kupanda baiskeli, kwani kupanda baiskeli si kama tu anaweza kutazama mandhari nzuri ya mji huo, bali pia anaweza kujenga afya. Sasa amekuwa na marafiki wengi, anapenda kuwasiliana na kubadilishana chakula kizuri na marafiki zake.

    Bwana Kim alisema kuwa, baada ya kuhitimu masomo, atafungua karakana yake mwenyewe mjini Hangzhou, na kuendelea na masomo ya shahada ya udaktari, na kutoa mchango wake kadiri awezavyo katika kusukuma maingiliano ya utamaduni kati ya China na Korea ya kusini, mke na watoto wake pia watakaa pamoja naye. Mji wa Hangzhou umekuwa ni maskani yao, na ni mahali ambapo panawafurahisha.