Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-31 09:47:01    
Makabila madogomadogo ya China yanayopewa haki ya kujiendesha (sehemu B)

cri
    Kuhusu utaratibu wa kujiendesha kwa sehemu za makabila madogomadogo na "Sheria ya kujiendesha kwa sehemu za makabila madogomadogo", ofisa wa idara ya sera na kanuni katika Kamati ya mambo ya makabila madogomadogo ya China Bwana Wang Ping alifahamisha kuwa, kanuni za kimsingi za utaratibu wa kujiendesha kwa makabila madogomadogo ni kuwa, chini ya uongozi wa pamoja wa serikali kuu ya China, makabila madogomadogo yanaweza kuanzisha mamlaka yao ya kujiendesha katika sehemu wanazoishi watu wengi wa makabila madogomadogo, na kupewa haki ya kujiendesha.

    "Sheria ya kujiendesha kwa sehemu zenye makabila madogomadogo" ni sheria ambayo imeainisha sehemu inayojiendesha kuwa na madaraka ya kujiendesha katika nyanja za siasa, uchumi, ubunifu wa kanuni na sheria na ujenzi wa utamaduni.

    Mwaka 2001, chombo cha utungaji sheria cha China kiliifanyia marekebisho "Sheria ya kujiendesha kwa sehemu za makabila madogomadogo", kuinua hadhi ya utaratibu wa kujiendesha kwa sehemu za makabila madogomadogo, na kukamilisha zaidi sheria hiyo. Kuhusu hatua hiyo ofisa wa wizara ya mambo ya raia ya China Bwana Wang Ping akifahamisha alisema:

    Baada ya kufanyiwa marekebisho, sheria hiyo imeinua hadhi ya utaratibu wa kujiendesha kwa sehemu za makabila madogomadogo, na kuthibitisha kuwa utaratibu huo ni utaratibu wa kisiasa wa kimsingi wa nchi; sheria hiyo imeimarisha kazi ya kusaidia sehemu za makabila madogomadogo. Vifungu vingi katika sheria hiyo hasa vinavyohusu mambo ya fedha, ushuru, na hifadhi ya ardhi ya nchi, vimeainisha kusaidia sehemu zinazojiendesha za makabila madogomadogo.

    Mbali na sheria ya kujiendesha kwa sehemu za makabila madogomadogo inayotekelezwa nchini kote China, katiba ya China pia imezipa sehemu mbalimbali zinazojiendesha madaraka ya kutunga kanuni zinazofaa hali ya kujiendesha kwa sehemu hizo, kutokana na umaalumu wa makabila na sehemu wanazoishi watu wa makabila hayo. Kwa mfano, kutokana na "Sheria ya idadi ya watu na uzazi wa mpango", kudhibiti idadi ya watu ni sera ya kimsingi ya China. Lakini ili kuhakikisha ongezeko la idadi ya watu wa makabila madogomadogo, serikali inaziruhusu sehemu mbalimbali zinazojiendesha za makabila madogomadogo ziwe na sera zao kuhusu uzazi katika maeneo yao. Kwa kweli "sheria ya idadi ya watu na uzazi wa mpango" inawazuia hasa watu wa kabila la Han.

    Aidha, baadhi ya sehemu zinazojiendesha za makabila madogomadogo pia zilitunga vifungu vyao vya sheria vinavyohusu ndoa kutokana na historia, mila na desturi za makabila hayo, vifungu hivyo vina unyumbufu wa kiasi fulani ikilinganishwa na "sheria ya ndoa" ya China. Kwa mfano; wanawake na wanaume wa makabila madogomadogo wanaoruhusiwa kufunga ndogo ni wenye umri wa chini ya miaka miwili kuliko watu wa kabila la Han. Takwimu zilizokusanywa zinaonesha kuwa, ilipofika mwishoni mwa mwaka 2003, zaidi ya sheria 480 zilitungwa na sehemu za makabila madogomadogo zinazojiendesha.

    Utaratibu wa kujiendesha kwa sehemu za makabila madogomadogo umehakikisha ipasavyo makabila madogomadogo ya China yanashiriki katika usimamizi wa mambo ya nchi na sehemu. Kwa mfano, sheria hiyo imeamua kuwa, maofisa wakuu wa mamlaka ya utawala wa sehemu mbalimbali zinazojiendesha yaani wenyeviti wa serikali za kila mtaa unaojiendesha, wakuu wa tarafa mbalimbali zinazojiendesha, na wakuu wa wilaya zinazojiendesha lazima wawe watu wa makabila madogomadogo.

    Watu wa kabila la Han hawaruhusiwi kushika nyadhifa hizo. Katika mamlaka ya utawala wa ngazi mbalimbali kama vile, utungaji sheria, usalama wa umma na uendeshaji wa mashitaka, watu wengi wa makabila madogomadogo wanashika nyadhifa muhimu.

    Kabila la wakorea ni moja ya makabila madogomadogo ya China. Bwana Kim Byung Ho ni mkorea, yeye ni Profesa wa chuo kikuu cha makabila madogo ya China, na mtaalamu wa utafiti wa sera na nadharia za makabila madogomadogo. Kuhusu hali ilivyo ya sasa na siku za usoni za mambo ya makabila madogomadogo ya China, Profesa Kim alisema kwa lugha ya kikorea:

    Hivi sasa China imeanzisha uhusiano wa makabila ulio wa usawa, mshikamano, urafiki na kusaidiana. Katiba ya China na Sheria ya kujiendesha kwa sehemu za makabila madogomadogo pamoja na sheria zilizotungwa na sehemu zinazojiendesha zimekuwa mfumo wa sheria wenye umaalum wa kichina, mfumo huo utasukuma mbele zaidi maendeleo na kukamilisha utaratibu wa kujiendesha kwa makabila madogomadogo.

    Wasikilizaji wapendwa, sasa tumekwisha wafahamisha hali ya jumla kuhusu maisha na maendeleo ya makabila madogomadogo ya China. Sasa tunatoa maswali mawili, tunataka msikilize kwa makini ili muweze kuyajibu vizuri.

    Swali la kwanza: Nchini China kuna makabila madogomadogo mangapi?

    Swali la pili : Makabila madogomadogo ya China yamepewa haki ya kujiendesha au yanaongozwa moja kwa moja na serikali kuu?

    Wiki ijayo tutawaletea makala ya nne, yaani makala ya mwisho ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Miaka 55 ya China mpya. Tunapenda mkumbuke kuwa kila makala tunayowasomea, pia tunaiweka kwenye tovuti yetu katika kipindi cha sanduku la barua. Karibuni mtembelee tovuti yetu, anuani yake ni www.cri.cn. Chagua kiswahili.

Idhaa ya kiswahili 2004-08-31