Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-01 21:11:04    
Mlima Wudang

cri

    Mlima Wudang unajulikana kwa mandhari yake nzuri na utamaduni wake mkubwa. Ni sehemu yenye mahekalu mengi ya dini ya Dao, dini ambayo iko nchini China peke yake. Mwaka 1994 mlima Wudang uliorodheshwa kwenye kumbukumbu za urithi wa dunia.

    Mlima Wudang uko kaskazini mwa mkoa wa Hubei kusini mwa China, ni mlima mkubwa wenye umbali wa kilomita 400. Mlima huo una vilele 72, kitu cha ajabu ni kuwa miongoni mwa vilele hivyo 72, 71 vinakiinamia kilele kikuu kiitwacho Tianzhu.

    Licha ya mandhari nzuri, mlima huo unatofautiana na milima mingine kwa kuwa na mahekalu mengi ya dini ya Dao, dini ambayo ipo nchini China peke yake.

    Huko mahekalu yalianza kujengwa tokea karne ya 7 mengi zaidi yalijengwa katika karne ya 15 ya Enzi ya Ming nchini China. Kutokana na historia, mfalme Zhu Li wa Enzi ya Ming alikuwa muumini wa dini ya Dao, akijinadi kuwa kiti chake cha kifalme alipewa na mungu wa dini ya Dao, na mungu huyo alipokuwa duniani alitawa katika mlima Wudang. Kutokana na imani yake kubwa baada ya kumaliza kujenga Kasri la Kifalme na Hekalu la Tiantan mjini Beijing, mwaka 1412 mfalme huyo alianza kujenga mahekalu katika mlima huo kwa kutumia wafanyakazi laki 3, ujenzi ulifanyika kwa miaka 13. Huu ni ujenzi kabambe mlimani nchini China.

    Mahekalu kwenye mlima Wudang yalipangwa kwa dhana ya dini ya Dao na muungano wa madaraka ya kifalme, yakionesha utukufu wa dini na taadhima ya mfalme. Kuna njia ya kilomita 70 iliyotandazwa kwa mabamba ya mawe kuanzia msingi wa mlima hadi kufikia hekalu moja la dhahabu lililopo kileleni Tianzhu. Kwenye pande mbili za njia hiyo yalijengwa mahekalu mengi kwa aina na ukubwa tofauti zaidi ya mia, miongoni mwa mahekalu hayo, 72 ni mapango ya mawe yaliyochimbwa, moja kati ya mapango hayo, ni pango la Laojun.

   Pango la Laojun ni hekalu lililochimbwa mwanzo miongoni mwa mapango yote ya mahekalu. Katikati ya pango hilo kuna sanamu ya mungu wa dini ya Dao aliyekaa. Ingawa uso wa sanamu hiyo umeharibika lakini sanamu yenyewe pia inaonesha jinsi usanii ulivyokuwa wakati wa Enzi ya Tang nchini China katika karne ya 8. Pembeni mwa sanamu kuna maneno yaliyochongwa, ambayo yanaonesha maandiko tofauti ya Kichina katika enzi mbalimbali tokea karne ya 10 hadi 19 nchini China, ni kumbukumbu yenye thamani kubwa ya historia.

    Hekalu la dhahabu ni jengo linalovutia zaidi katika mlima Wudang. Hekalu hilo liko kwenye kilele kikuu cha Tianzhu, hilo ni hekalu kubwa nchini China lililotengenezwa kwa shaba nyeusi na kupakwa rangi ya dhahabu.

    Hekalu hilo lina kimo cha mita 5 na upana wa mita 4, ndani yake kuna sanamu ya shaba ya mungu wa dini ya Dao, uzito wake ni tani 10. Kutokana na historia, sanamu hiyo ilitengenezwa mjini Beijing kwa shaba yenye uzito wa tani 20 na dhahabu kilo 300, na ilisafirishwa kwenda huko mlimani kwa safari ndefu. Kwa sababu shaba inapitisha umeme, kila radi inapopiga mwaga mkali unatokea pembezoni mwa hekalu hilo. Ajabu ni kuwa ingawa hekalu hilo limekuwa linapigwa na radi katika karne nyingi lakini halijaharibika, badala yake linang'ara zaidi. Kadhalika, pia kuna maajabu katika mahekalu mengine. Kwa mfano katika hekalu liitwalo Zhuanshen, ndani yake kuna kengele kubwa, lakini inapogongwa sauti haisikiki ndani bali inasikika nje. Hekalu liitwalo Fuzhen lenye ghorofa 5 lilijengwa gengeni, chini yake lina mhimili wa nguzo moja tu. Mahekalu yote yalijengwa au kuchimbwa kwa kuitumia vizuri hali tofauti ya majabali na kuyafanya mahekalu yalingane na mazingira ya pembezoni yenye miti na michirizi, na kuwa kama picha za kuchorwa.

    Mlima Wudang sio tu ni mlima wa utamaduni wa dini ya Dao, bali pia ni mlima wenye aina nyingi za mimea, hasa mimea ya miti-shamba. Mtaalam mashuhuri wa dawa za miti-shamba katika China ya kale, Li Shizhen, aliwahi kuishi katika mlima huo kwa miaka mingi na alihariri kitabu chake cha "Muhtasari wa Maelezo ya Dawa za Miti-shamba". "Kunfu" ya Kichina katika mlima Wudang pia inajulikana sana, kwa kuwa watawa wa dini ya Dao wanapotawa huwa wanacheza michezo ya "kunfu" ili kuimarisha afya na kujilinda. "Kunfu" katika mlima Wudang ni aina muhimu sawa na "kunfu" ya Shaolin katika "kunfu" za Kichina.

Idhaa ya Kiswahili 2004-09-01