Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-07 18:33:58    
Sekta ya viwanda katika sehemu ya kaskazini ya mkoa wa Jiangsu imekuwa na maendeleo ya haraka

cri

    Sehemu ya kaskazini ya mkoa wa Jiangsu, ambayo ilijulikana kwa "sehemu iliyodidimia kiuchumi" katika mkoa huo, sasa imepata maendeleo makubwa. Viongozi na wakazi wa miji mitano ya Xuzhou, Huaina, Yancheng, Lianyungang na xuqian hawakukaa kusubiri wala kutegemea msaada wa serikali, bali walijitahidi kutatua matatizo sugu yaliyokwamisha maendeleo ya sehemu yake. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, ongezeko la thamani ya uzalishaji mali katika viwanda vya miji hiyo mitano lilikuwa 18.2%, wakati ongezeko la uwekezaji kwenye mali zisizohamishika lilikuwa ni 24.3% na uwekezaji wa moja kwa moja wa wafanyabiashara wa nchi za nje lilikuwa ni 52.7%. Wanauchumi wamechambua kuwa maendeleo ya viwanda vya sehemu ya kaskazini ya mkoa wa Jiangsu yameingia katika kipindi kipya.

    Hali maalumu mojawapo ya uchumi wa mkoa wa Jiangsu ni kuweko tofauti kubwa kati ya sehemu za kusini na kaskazini. Idadi ya wakazi pamoja na eneo la miji hiyo mitano inachukua karibu nusu ya mkoa huo mzima, lakini jumla ya thamani ya uzalishaji ilikuwa pungufu ya robo ya mkoa huo, na tofauti hiyo kubwa ya maendeleo ya uchumi inatokana zaidi na viwanda.

    Hapo awali, baadhi ya sehemu za kaskazini za mkoa huo, zilitumia uzoefu wa sehemu zilizoendelea za kusini mwa mkoa huo, bila kujali hali zake maalumu, na matokeo yake ni kama wahenga walivyosema kuwa haraka haraka haina baraka. Hivi sasa, wanafungamanisha uzalishaji wa mazao ya kilimo wa mashirika makubwa, usindikaji wa mazao ya kilimo na marekebisho ya muundo wa kilimo, wanatoa kipaumbele kwa kazi ya usindikaji wa mazao ya kilimo na kufungua njia yao wenyewe ya maendeleo ya viwanda.

    Wilaya ya Sheyang iko katika pwani ya bahari ya Huang, mazingira ya kimaumbile ya sehemu hiyo yanafaa sana kwa kilimo cha zao la pamba, katika miaka mingi iliyopita, eneo la mashamba ya pamba lilikuwa ni kiasi cha hekta 53,000, na kujulikana kuwa ni wilaya ya kwanza ya pamba nchini. Lakini hapo zamani, pamba iliyokuwa ikizalishwa katika wilaya hiyo iliuzwa nje, ambapo nyongeza kubwa ya thamani ya kazi za usindikaji ilipotea, hali hiyo iliathiri moja kwa moja maendeleo ya uchumi. Katika miaka ya karibuni, wakazi wa Sheyang walianza kulenga maendeleo yake kwa kazi za viwanda, na kuanza kutafuta njia ya kuanzisha mfumo wa kazi za viwanda kutoka kulima zao la pamba, kusokota nyuzi, kufuma vitambaa na kushona nguo. Mwaka 2003, mauzo ya bidhaa za nguo yalikuwa zaidi ya Yuan bilioni 7, ambapo nyongeza za bidhaa za nguo zilichukua 51.3% kati ya nyongeza ya kazi za viwanda, na mchango uliotolewa na viwanda vya nguo ulikuwa ni kiasi cha 38% ya pato la mkoa huo mzima.

    Katika hatua za kuharakisha maendeleo ya viwanda, sehemu mbalimbali za kaskazini mwa mkoa wa Jiangsu, zilitumia vilivyo hali bora ya sehemu zake, kujitahidi kuanzisha mfumo wa viwanda na uzalishaji ili kufikia hali bora ya kiuchumi kutoka hali bora ya rasilimali.

    Hapo zamani, kuomba msaada wa fedha na miradi ya ujenzi lilikuwa ni jambo la kawaida kwa viongozi na wakazi wa sehemu ya kaskazini ya mkoa wa Jiangsu. Lakini hivi sasa, viongozi na wakazi wa sehemu hiyo wametupilia mbali mawazo ya kusubiri, kutegemea na kuomba misaada kutoka ngazi za juu za serikali. Sasa wanatumia ipasavyo fursa nzuri ambayo kampuni za nchi za nje na za sehemu ya kusini mwa mkoa huo kuhamia sehemu ya kaskazini ya mkoa huo, wanavutia mitaji ya kigeni na teknolojia za kisasa.

    Kutokana na takwimu zilizokusanywa na ofisi ya uratibu wa maendeleo ya sehemu ya kaskazini ya mkoa wa Jiangsu kwamba kati ya mwezi Januari na Juni mwaka huu miji hiyo mitano imevutia miradi 1,236 yenye thamani ya Yuan milioni 5 kila mmoja, kati ya miradi hiyo, ile ya viwanda imechukua 70%.

Idhaa ya Kiswahili 2004-09-07