Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-13 17:00:52    
Tamasha kubwa la vitabu la kimataifa mjini Beijing

cri

    Tamasha kubwa la vitabu la kimataifa limeanza kufanyika mjini Beijing, mashirika zaidi ya 900 kutoka nchi na sehemu 42 duniani yanashiriki kwenye tamasha hilo. Wataalamu wanaona kuwa kutokana na soko la uchapishaji nchini China kuwa wazi zaidi siku hadi siku kwa nchi za nje, washapishaji wa nchi mbalimbali wamekuwa na hamu kubwa ya kushirikiana na China.

    Awali, shughuli za uchapishaji nchini China hazikuwa wazi kwa nchi za nje. Kabla ya miaka ya 80 ya karne iliyopita, shughuli za uchapishaji zilikuwa ni sehemu muhimu katika itikadi ya kisiasa, mashirika ya magazeti, ya uchapishaji wa vitabu, majarida na hata viwanda vya uchapaji, yote yalikuwa ni idara za serikali na yalihodhi kabisa soko la uchapishaji nchini China. Pamoja na hayo China ilichuja sana machapisho ya nchi za nje, haikuwa rahisi kwa wasomaji wa kawaida kupata magazeti au majarida ya nchi za nje ila tu kuweza kuyaona yaliyowekwa ndani ya madirisha ya maonesho katika taasisi na maktaba ya vyuo vikuu.

    Baada ya China kujiunga na WTO mwaka 2001, hali hiyo imebadilika kabisa. Ili kutimiza ahadi zake kwa WTO, China imeharakisha hatua za kufungua wazi katika shughuli za uchapishaji. Tokea tarehe mosi ya mwezi Mei mwaka jana ilipoanza kutekelezwa "kanuni za usimamizi wa mashirika ya nchi za nje ya uchapishaji wa vitabu, magazeti na usambazaji wa majarida nchini China", China imefungua rasmi kwa mashirika ya nchi za nje shughuli za uchapishaji wa vitabu, magazeti na biashara ya rejereja ya majarida. Baada ya tarehe 10 Desemba mwaka huu, biashara ya jumla ya vitabu na magazeti itakuwa wazi kwa nchi za nje. Naibu mkurugenzi wa Idara Kuu ya Uchapishaji ya China Bw. Yu Yongzhan alisema, "Serikali ya China inaheshimu na kulinda hakimiliki, inaunga mkono na kusukuma mbele maingiliano kati ya mashirika ya uchapishaji ya nchini na ya nchi za nje. Kujiunga na WTO kumeleta wakati mzuri wa kustawisha maingiliano hayo.

    Bw. Yu alidokeza kuwa katika nyanja ya uchapaji, mwaka 2002 China iliidhinisha mashirika 102 ya nchi za nje, mwaka jana ilidhinisha mashirika 84, na nusu ya kwanza ya mwaka huu hali iliendelea kuwa nzuri. Katika nyanja ya usambazaji, hivi sasa mashirika ya nchi za nje 11 yamepata leseni, kwa makadirio, hadi mwishoni mwa mwaka huu idadi hiyo itaongezeka kwa kiasi kikubwa.

    Biashara ya haki za kunakili ni sehemu muhimu ya maingiliano na ushirikiano katika shughuli za uchapishaji. Kutokana na takwimu, katika miaka 10 iliyopita, haki za kunakili zilizonunuliwa kutoka nchi za nje ziliongezeka kwa asilimia 20 kwa mwaka, mwaka jana haki hizo zilikuwa karibu elfu 13.

    Bw. Wang Huapeng, mkurugenzi wa idara ya maingiliano na ushirikiano na nchi za nje katika Idara Kuu ya Uchapishaji ya China, anafahamu sana hali ya uchapishaji nchini China na nchi za nje. Alisema, "Katika biashara ya haki za kunakili, tumeingiza haki nyingi kuliko kuuza katika nchi za nje. Hii inatokana na kuwa hali ya sayansi na teknolojia nchini China haijaendelea sana, kwa hiyo tunahitaji kuingiza machapisho mengi ya sayansi na teknolojia kutoka nchi za nje, hii ni hali ya kawaida na hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu. Sababu nyingine ni kuwa shughuli zetu za uchapishaji zina haja ya kujifunza kutoka nchi za nje katika mageuzi yetu."

    Licha ya biashara ya haki za kunakili, ushirikiano wa uchapishaji pia ni sehemu muhimu katika maingiliano ya shughuli za uchapishaji kati ya China na nchi za nje. Ushirikiano wa uchapishaji unakusudia kuifanya China kuwa na haki ya kuhariri na kuchapisha vitabu na majarida ya nchi za nje. Hivi sasa mashirika ya majarida ya China zaidi ya 40 yanashirikiana na mashirika ya nchi za nje, majarida hayo ni kuhusu maonesho ya nguo, samani na vitu vya matumizi ya kila siku.

    "Baraza la Kimataifa la Wachapishaji" ni moja ya shughuli zilizopo katika tamasha hilo la vitabu. Wakuu wa mashirika ya uchapishaji kumi kadhaa yakiwemo kundi la mashirika ya uchapishaji la China, Kundi la Uchapishaji la Pearson la Uingereza na Kundi la Uchapishaji la Hachette la Ufaransa yanashiriki kwenye tamasha hilo. Mtendaji mkuu wa Kundi la Uchapishaji la Pearson la Uingereza Bi. Marjorie Scardino kwenye baraza hilo alisema, "China ni soko kubwa ama kwa machapisho kwa umma, au vitabu au majarida. Kutokana na China kujiunga na WTO tumepata wabia wengi nchini China, ushirikiano wetu upo katika biashara ya haki za kunakili, ushikiano wa mashapisho ya mafundisho ya lugha ya Kiingereza na mambo ya fedha."

    Imefahamika kuwa, ili kufikia kiwango cha juu cha uchapishaji duniani, China imeharakisha mageuzi ya mashirika ya uchapishaji nchini China. Hivi sasa mashirika zaidi ya 500 nchini China yote yatageuzwa kuwa mashirika ya kibiashara isipokuwa tu Shirika la Uchapishaji la Umma ambalo litaendelea na mfumo wake wa huduma kwa umma kama zamani. Mageuzi hayo yameyapatia mashirika ya uchapishaji ya nchini China nguvu za kuendeleza ushirikiano na nchi za nje.

Idhaa ya Kiswahili 2004-09-13