Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-14 15:56:56    
Barua za wasikilizaji 0914

cri
    Bwana Msabah Mbarouk alisema katika barua yake nyingine kuwa, baada ya kufuatilia kwa makini sana juu ya maendeleo makubwa ya kiuchumi yaliyopatikana nchini Jamhuri ya Watu wa China katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili iliyopita, aligundua kwamba siri kubwa ya mafanikio na ufanisi huo ni tabia ya kijadi ya wachina ya kufanya kazi kwa bidii usiku na mchana ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

    Ni wazi kabisa nguvu kazi ya mamilioni ya wachina katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi chini ya sera za marehemu Deng Xiaoping, ndiko leo kulikoligeuza Taifa la China kunawili mbele ya walimwengu.

    Ikiwa China tayari inaadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mzee Deng Xiaoping mwaka huu, basi hapana shaka yoyote maadhimisho hayo yataambatana na mafanikio yaliyopatikana chini ya fikra, mawazo na busara za Mzee Xiaoping katika kuboresha sekta za kiuchumi, kisayansi, kiteknolojia na kijamii kwa Jamhuri ya watu wa China.

    Mwisho angependa kutoa pongezi zangu za dhati kwa viongozi na wananchi wote wa China kutokana na maadhimisho hayo ya kutimia miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mzee Deng Xiaoping kiongozi na mwanamageuzi wa China ya leo na angewazawadia shairi langu fupi juu ya "wasifu" wa Mzee Xiaoping, shairi ambalo linaitwa:

    "Xiaoping ni kiongozi kamwe hatosahaulika"

    Alizaliwa kiongozi, mwenye sifa na ujuzi.

    Xiaoping muokozi, aliokoa jahazi.

    Alileta mapinduzi, kutumia nguvu kazi.

    Xiaoping ni kiongozi, kamwe hatosahaulika.

    Mengi yake mageuzi, yalileta ufumbuzi.

    Aliondoa ajizi, uvivu na usingizi.

    Wachina kuchapakazi, uchumi ukabavizi.

    Xiaoping ni kiongozi, kamwe hatosahaulika.

    Busara zake makini, ziliingia akilini.

    Mawazo yenye thamani, wachina waliyathamini.

    Na kuyaingiza vitendoni, kujua faidae ni nini.

    Xiaoping ni kiongozi, kamwe hatosahaulika.

    Yupo tena duniani, wachina wakutamani.

    Daima wakuthamini, umewatoa kizani.

    Hala pema kwa amani, huko uliko peponi.

    Xiaoping ni kiongozi, kamwe hatosahaulika.

    Tunamshukuru kwa dhati Bwana Mbarouk Msabaha ambaye anafuatilia sana vipindi vyetu kwenye radio na tovuti, na kutuletea makala mbalimbali pamoja na mashairi ya kututia moyo kuchapa kazi zaidi kwa kuwahudumia wasikilizaji wetu.

    Kilulu Kulwa wa sanduku la posta 161 Banriadi Shinyanga Tanzania. Anasema kuwa, mimi msikilizaji wenu ni mzima wa afya njema ninaendelea tu na shghuli za kila siku za ujenzi wa taifa. Anapenda atumie fursa hii kuwashukuru sana kwa barua zenu mlizonitumia ikiwa ni pamoja na picha za wanyama mbali mbali wa China ambao wapo katika hatari ya kutoweka. Hii inaonyesha kwamba rafiki wetu utazidi kuimarika na kustawi siku hadi siku.

    Anasema amefurahi pia kusikia sauti ya mtangazaji dada Josephine Liumba mtangazaji mashuhuri wa Radio Tanzania-Dar es Salaam, ambaye kwa sasa yupo hapo Radio China Kimataifa. ni jambo la kujivunia kwamba kwa sasa mnayo timu kubwa na nzuri ya watumishi wa idhaa ya Kiswahili ya CRI. Hongera sana.

    Bwana Kulwa anasema kuwa, katika makala ya Tazama China ambayo ilitangazwa na dada Josephine Liumba tarehe 15.7.2004 iliyozungumzia mfanya biashara wa kimarekani aliyeko Tanjin. Makala hiyo ilimvutia sana kwa kuwa ilimkumbusha safari yake ya kutoka Beijing kuelekea Tianjin alipokuwa ziarani nchini China mnamo miaka ya mwisho mwa karne ya 20.

    Anasema safari hiyo ilimpa na inaendelea kumpa taswira nzuri kabisa kuhusu nchi ya China na wananchi wake. Ndio maana huwa ana ndoto nyingine ya kuitembelea China, na pia ndoto ya kuandika kitabu chenye hadithi na simulizi nzuri kuhusu safari yake nchini China.

    Bwana Kulwa anasema, anaona Tianjin ni moja ya miji iliyomvutia sana na hataweza kusahau chakula kizuri cha kichina chenye radha safi alichokula katika Hotel moja huko Tianjin, mji ambao upo katika Pwani ya Bahari ya Pasific.

    Kwa sababu hii anatoa pongezi nyingi kwa watayarishaji wa kipindi cha Tazama China na anaomba tuzidi kuandaa makala za aina hiyo, anaamini na kufaraji kwamba siku moja tutatayarisha makala itakayoelezea habari za mji maarufu wa Xian ambako pia aliishi hapo kwa muda wa siku nne.

    Na pia anasema kuwa atafurahi kupata magazeti ya hivi karibuni kutoka Beijing China, kama vile China Today na China Pictorial. Na tunamshukuru sana kwa kutuelezea mengi ya kufurahisha, tutatilia maanani shauri lake la kutangaza makala nyingi zaidi za kuwafurahisha wasikilizaji wetu.

    Msikilizaji wetu Yakub Said wa sanduku la posta 2519 Kakamega Kenya ametuletea barua akisema kuwa, watangazaji wa idhaa ya kiswahili ya Redio China Kimataifa pokeeni salamu nyingi kutoka kwake akitumai tuko boheri na salama. Anasema amepata barua kutoka kwetu hivi karibuni.

    Anatuambia kuwa, yeye husikiliza sana matangazo yetu, na watu wengi hapo kwake Kakamega kijiji cha Maram Kanga wamependezwa sana na matangazo yetu pamoja na vipindi vya idhaa ya kiswahil ya Redio China Kimaraifa. Vipindi kama daraja la urafiki kati ya China na Afrika, kipindi cha jifunze kichina na kipinde cha nchi yetu mbioni na taarifa habari wanaomba angalao wapate baji ya (C.R.I) pamoja na kofia ya C.R.I.

    Anasema anaomba kutumia picha yake na nambari ya uanachama wake kumtengenezee kama kitambulisho cha mwanachama kisha ili aliweke shingoni na hiyo kitambulisho iwe na nembo ya Radio China kimataifa atashukuru sana, na atazidi kutuandikia maoni na mapendekezo. Tunashukuru ombi lake hilo ambalo limeonyesha moyo wake wa kuipendelea Radio China kimataifa, lakini kwa kweli hatutaweza kufanya, tumwobe atuelewe. Akitaka kupata zawadi yenye nembo ya Radio China kimataifa, labda tukipata tunaweza kumtumia.

Idhaa ya Kiswahili 2004-09-14