Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-20 10:58:40    
Wakazi wa Beijing wapenda kufanya mazoezi ya kujenga mwili

cri

    Zamani wachina wengi waliona kuwa kutoumwa ni kuwa na afya nzuri, sasa mawazo hayo yanabadilika. Sasa wanaona kuwa haifai kuzingatia afya zao baada ya kuumwa. Katika siku za kawaida wanatumia muda wao baada ya kazi na kutumia baadhi ya mapato yao katika kufanya mazoezi ya kujenga mwili. Viwanja na majumba ya michezo mbalimbali, bustani na vituo vya kufanyia mazoezi ya kujenga mwili katika mitaa yote, zimekuwa sehemu nzuri za kufanya mazoezi ya kujenga mwili.

    Wilaya ya Shijingshan iko katika sehemu ya magharibi ya mji Beijing. Uwanja wa mchezo wa mpira wa kikapu wa kampuni ya chuma na chuma cha pua ya Beijing ni kituo kikubwa cha kufanyia mazoezi ya kujenga mwili katika wilaya hiyo. Sio tu kuna uwanja wa mpira wa kikapu, bali pia kuna uwanja wa tennis, uwanja wa mpira wa vinyoya unaochezwa kwa miguu na ukumbi wa kufanya mazoezi ya kujenga mwili. Mwandishi wa habari alipofika kwenye jumba hilo, aliona watu wanaofanya mazoezi ya kujenga mwili wakiwa katika kila uwanja na ukumbi wa michezo. Mfanyakazi wa jumba hilo Bw. Fan Shengli alimweleza mwandishi wa habari akisema:

    "Jumba la uwanja wa mpira wa kikapu la kampuni ya chuma na chuma cha pua ya Beijing lilianza kufanya shughuli za kibiashara mwezi Januari mwaka 2002. Kwa mfano, mwanzoni tulikuwa na sehemu saba za uwanja wa mpira wa vinyoya, kadiri wapenzi wa michezo walivyoongezeka, uwanja wa mpira wa vinyoya umeongezeka na kufikia 15. Inapofika siku za mwisho wa wiki, sehemu 15 zinakuwa bado hazitoshi".

    Mwandishi wa habari alimkuta Bw. Zhang aliyekuwa akimaliza kucheza mpira wa vinyoya. Alimwambia mwandishi wa habari kuwa anakwenda huko kucheza mpira wa vinyoya mara mbili kwa wiki. Anasema: "Zana za huku ni nzuri, na watu wanaweza kumudu bei zake. Sasa maisha yetu yamekuwa mazuri siku hadi siku na tunazingatia sana afya zetu".

    Watu wengi wanaofanya mazoezi ya mwili wanaona kuwa kufanya mazoezi ya mwili baada ya kazi za kila siku, sio tu kunaweza kujenga afya, bali pia kunaweza kupunguza hatari ya kuwa na ugonjwa wa moyo. Zaidi ya hayo, uwanja wa kufanyia mazoezi ya mwili unaweza kuwa sehemu ya kupata marafiki wengine.

    Katika majumba mengine ya michezo ya wilaya ya Shijingshan, mwandishi wa habari pia aliona watu wengi wakiwa wanacheza michezo mbalimbali.

    Mfanyakazi wa ofisi ya michezo ya wilaya ya Shijingshan Bw. Ma Yuanwei alipohojiwa na mwandishi wa habari alisema kuwa, watu wanaotaka kucheza michezo katika jumba hilo la michezo wanapaswa kutoa taarifa mapema. Jumba hilo linawavutia wakazi wengi wa mtaa huo.

    Mbali na majumba na viwanja rasmi vya michezo, mitaa mingi ya wilaya ya Shijingshan ina viwanja vidogo vya kufanyia mazoezi ya kujenga mwili. Wakazi wanaweza kucheza michezo mbalimbali karibu na makazi yao. Nje ya milango ya bustani na sehemu zilizo wazi, kuna watu wengi wanaocheza ngoma, kucheza mpira wa vinyoya kwa miguu, kupeperusha tiara na michezo mingine.

    Sio wilaya ya Shijingshan peke yake, katika sehemu nyingine mjini Beijing pia kuna mashabiki wa michezo wanaocheza michezo mbalimbali. Kufanya mazoezi ya kujenga mwili limekuwa ni jambo la muhimu katika maisha ya watu ya kila siku.

Idhaa ya Kiswahili 2004-09-20