Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-21 19:25:32    
Barua za wasikilizaji 0921

cri
    Hivi karibuni tumepata barua kutoka kwa baadhi ya wasikilizaji wetu, ambao wametuletea majibu yao ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Miaka 55 ya China mpya. Baadhi ya majibu tuliyoletewa na wasikilizaji siyo sahihi sana. Tungependa kuwaarifu wasikilizaji wetu kwamba, msiwe na haraka ya kutuletea majibu. Kuanzia tarehe 26 mwezi huu tutarudia tena matangazo yetu ya makala 4 za chemsha bongo kuhusu ujuzi wa miaka 55 ya China mpya, na huenda tutaweza kurudia tena baadaye. Tunatumai kuwa wasikilizaji wetu mtasikiliza kwa makini makala hizo, ili muweze kujibu maswali hayo kwa usahihi zaidi.

    Sasa tunawasomea baadhi ya barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu. Msikilizaji wetu Homoud A Tamim wa sanduku la posta 267 Kigoma, Tanzania ametuletea barua akianza kwa salamu kwa watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili wa Radio China Kimataifa, akisema anashukuru kama sisi ni wazima. Nasi pia tunashukuru kwa salamu zake, hapa Beijing sote hatujambo.

    Bwana Tamim anasema dhumuni la barua hii ni kutufahamisha kwamba Club ya Tanganyika inaendelea kutusaidia ili matangazo yetu yawafikie watu wengi, wanajitahidi kuwahamasisha watu wasikilize Radio China kimataifa. Anasema hivi karibuni wametoka katika kijiji kimoja kinachoitwa Kalya ambacho kipo hapo Kigoma. Walikwenda kuwataarifu watu wa huko mitabendi zetu na anuani zetu ili waweze kutupata vizuri.

    Anasema kazi hiyo waliifanya kwa siku 6 na waliifanya vizuri na watu waliipokea vizuri lakini walikuwa waliwauliza vitambulisho vya wanachama wa Radio China kimataifa lakini waliwajibu kuwa bado hawajatumiwa. Sasa anasema kuwa wangependa wao kwa pamoja wa Club ya Tanganyika tuwatumie vitambulisho. Pia yeye anaomba tumtumie vitabu ambavyo vinaelezea nchi ya China ya sasa na vinavyoonesha miji ya China mpya. Anasema anaomba tuzingatie hayo kwani ni mambo muhimu sana katika club ya Tanganyika

    Tunawashukuru sana kwa kazi iliyofanywa na klabu hiyo ya wasikilizaji wetu ya kutusaidia kupata wasikilizaji wengi. Tungependa kuwataarifu kuwa hivi karibuni tumewatumia barua na zawadi ndogondogo, kama bado hamjazipokea basi tunadhani kuwa ziko njiani.

    Bwana Tamim anasema pia kuwa amepata mwanachama mwingine ambaye anayeitwa Zaid Mzee naye pia anaomba kuwa mwanachama kupitia club ya Tanganyika naye anasema atafurahi sana kama jina lake litaingia kwenye orodha ya wanachama wetu wa kudumu.

    Sisi tunamkaribisha Zaid Mzee kuwa msikilizaji wetu, tunamtaka tu asikilize kwa makini vipindi vyetu mbalimbali na kutuletea maoni na mapendekezo yake ili tuboreshe zaidi vipindi vyetu na kuwatumikia vizuri wasikilizaji wetu.

    Katika barua yake Bwana Tamim pia anaomba turekebishe jina lake katika orodha ya majina, alisema tuliandika Homoud-A.Tamin sio Tamin ni Tamim anaomba turekebishe. Hapa tunaomba radhi kutokana na kosa la uchapaji. Aidha anaomba tupokee picha yake ndogo ili tumfahamu japo kwa sura. Tunashukuru kwa picha yake, na kama kukiwa na uwezekano tutaiweka picha hiyo kwenye tovuti yetu kwenye sehemu ya sanduku la barua, ili wasikilizaji wengine wanaotembelea tovuti yetu nao pia waweze kukufahamu kwa sura.

    Msikilizaji wetu Ndeeche Mwanga Ommaala wa Jiji la Mombasa sanduku la posta 95547 Kongowea ametuletea barua akisema kuwa, barua yake hii ni kutambua bidii na upendo tulionao kwake kwa kuhakikisha ya kwamba amepata kila aina ya taarifa juu ya vipindi na maendeleo yanayoendelea katika Radio China kimataifa. Anasema amepokea barua yetu nzuri sana ambayo tumemweleza mashindano ya chemsha bongo ya mwaka jana kuhusu utamaduni na utalii wa eneo la magharibi la China.

    Anasema shukrani zake ziwafikie wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili kwa kazi hiyo nzuri ambayo bayana inaonesha ugumu wa kazi iliyopo. Pia anasema anatoa pongezi nyingi kwa ndugu wasikilizaji 10 kutoka Australia, Nepal, India, Sri lanka, Vietnam, Iran, Hungary, Colombia, Benin, na Malaysia waliyoshinda katika mashindano hayo na kupata tuzo maalum.

    Anasema mababu wa Afrika ya mashariki wana usemi unaosema, "asiyekubali kushindwa si mshindani". Anawataka walioshinda waendelee kupeperusha bendera ya ulimi wa mwafrika katika nchi zao na nchi rafiki.

    Anasema jamii ya wabantu ya Abalulya wa kabila la kifalme Kenya ya magharibi, nao wanasema "eshienyu ne shienyu" maana yake chenu ni chenu, au kwa kiswahili tunaweza kusema damu ni nzito kuliko maji. Kwa hivyo, sitawasahau ndugu Ras Franz Manko Ngogo wa Tarime Mara, Tanzania na Ndugu Xavier Telly Wambwa wa Bungoma Kenya kwa nafasi zao katika idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa. Mungu awabariki sana na nyote mwenyezi mungu awajazie kheri. Nami pia mwaka huu nimo kwenye mashindano na ninaahidi kuwa nitaongeza juhudi na huenda siku moja nitatembelea Beijing, China. Pia anawaomba ndugu wote wachina na wengine wote duniani mtembelee Afrika ya mashariki. Afrika ya mashariki ni mkate wenye asali, nyumba ya raha na boma la vivutio vya utalii, historia pamoja na utamaduni.

    Anataka wakati wowote tukifikiria kutembelea bara la Afrika tukumbuke kuwasiliana naye na atatusaidia kupata habari kamilifu kuhusu utalii na kupata malazi maalum, anamaliza kwa kusema karibu Afrika.

    Kweli huyu ni moja ya wasikilizaji wetu wachangamfu sana na mwenye moyo mwema. Tunamshukuru sana, kama tukipata fursa ya kutembelea huko Mombasa basi hakika tutajitahidi tuwasiliane naye, na pia tutawaarifu marafiki zetu kuhusu hiyo.

    Na mwisho tungependa kuwakumbusha tena wasikilizaji wetu kuwa kuanzia tarehe 26 mwezi huu tutarudia matangazo yetu ya makala 4 za chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Miaka 55 ya China mpya, msikose kutusikiliza, na yeyote anayeweza kupata nafasi ya kutembelea tovuti yetu, anaweza kupata makala hizo nne ambazo zimewekwa kwenye tovuti yetu katika kipindi cha sanduku la barua.

Idhaa ya Kiswahili 2004-09-21