Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-22 21:06:03    
Kenya yapenda kuimarisha mawasiliano na maingiliano kati yake na nchi nyingine za Afrika katika eneo la vijana

cri

    Yafuatayo ni mahojiano kati ya mwandishi wetu wa habari na mkurugenzi mkuu wa idara ya vijana ya Kenya Bwana Japhet Kekie Mwania aliyekuja China kushiriki kwenye tamasha la kwanza la vijana kati ya China na Afrika lililofanyika mwezi Agosti mwaka huu.

    Swali: Bwana Japhet K. Mwania, unaweza kunifahamisha kidogo hali ya vijana nchini Kenya?

    Jibu: Hali ya vijana wa Kenya ni kama hali ya vijana wote wa ulimwengu, shida yao ni mambo ya fedha, mambo ya masomo, lakini serikali ya Kenya imechukua hatua za kuwapatia vijana masomo, ili wafanikishe maisha yao ya baadaye.

    Swali: Je serikali ya Kenya imechukua hatua gani katika kuwaendeleza vijana?

    Jibu: Serikali ya Kenya ina mipango mingi katika kuendeleza vijana wa Kenya. Kwanza ni kutoa elimu bure, Kenya National Youth Service tunachukua vijana wa mitaani na kuwapatia elimu, wengi wamefanikiwa kujiunga tena na jamii.

    Swali: Mwaka juzi, serikali ya Kenya iliutangaza ugonjwa wa ukimwi kuwa janga la taifa. Je Kenya imechukua hatua gani katika kupambana na ukimwi?

    Jibu: Kenya ina idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI, hasa vijana kuanzia umri wa miaka 15 hadi 49. Serikali ya Kenya ikishirikiana na serikali nyingine duniani zinasaidiana kuelimisha vijana juu ya ugonjwa wa huo na athari zake na pia tunawaambia vijana wasifanye mapenzi ovyo.

    Swali: Kushiriki katika tamasha hilo la vijana kati ya China na Afrika kutakusaidia namna gani ?

    Jibu: Kushiriki katika na tamasha hilo kutanisaidia sana kwa mambo mengi, nimepata elimu kubwa ya kuendesha kikosi cha Kenya National Youth Service. Vijana wa Kenya kitu kimoja wanachofanya ni ujenzi wa taifa, tunaendesha miradi ambayo inaweza kuwasaidia wananchi. Na nimeona China imeendelea sana. Jana nilipotembelea ukumbi mkuu wa mikutano ya watu wa China niliambiwa kuwa jumba hilo kubwa lilijengwa kwa muda mfupi sana kwa nguvu ya pamoja ya wananchi, nitawaambia wakenya waungane pamoja ili waweze kufanya kitendo kama hicho.

    Nimeungana na vijana wengine wa Afrika ambao wana maoni tofauti, nimefanikiwa sana na elimu yao katika mkutano huu, pia nimepata elimu kubwa kutoka kwa vijana wa China, nimeona kuwa, nitakuwa na elimu kubwa ya kuendesha kikosi cha vijana hapo baadaye.

    Swali: Kutokana na hali niliyojua wajumbe 132 wa vijana kutoka nchi 44 za Afrika wameshiriki kwenye tamasha hilo, hii ni fursa nzuri kwa wajumbe hao kubadilishana maoni na kujifunza, wewe unaonaje?

    Jibu: Ni kweli, katika nchi za Afrika, Kenya ilitangulia katika kuanzisha kazi za vijana. Kwani Kenya National Youth Service ilianzishwa tarehe mosi Septemba mwaka 1964, mwaka mmoja tu baada ya kupata uhuru. Katika eneo hilo tumepiga hatua kubwa zaidi kuliko nchi nyingine. Idara yangu ina vijana 10,000 wa kiume na kike, ambao wako pamoja wakifanya kazi tofauti. Nchi nyingine za Afrika ni chache sana kufika hatua hiyo. Lakini nimebadilishana maoni na wengine ya kuonesha kuwa, tunapenda kuwasiliana na kushirikiana. Sasa Tanzania na Zambia wameonesha nia ya kuja Kenya kuona jinsi tunavyoendesha kikundi chetu cha National Youth Service.

    Swali: Je hii ni mara ya kwanza kwako kufika China?

    Jibu: Hii ni mara yangu ya kwanza kufika China, nataka kusema kuwa, wakenya wengi hawajui China imefanikiwa katika maendeleo kwa kiwango hiki. Kwa hivyo nawataka wakenya wote na waafrika kujua China ni nchi kubwa ya uchumi duniani, imefanikiwa sana na inaendelea sana. Naomba niweze kutembelea mahali mbalimbali na viwanda ili tufahamu zaidi hali ya viwanda nchini China. Kwa maana sasa nitarudi na mafanikio ambayo ni tofauti na niliyokuja nayo. Kabla ya kufika China nilifikiri kuwa China ni nchi ndogo isiyo na nguvu ya uchumi.

    Kama alivyokuwa akitumai Bw Mwania, baada ya matembezi yao mjini Beijing, wajumbe wa vijana wa Afrika walitembelea sehemu mbalimbali nchini China, na kujionea kwa macho yao wenyewe mabadiliko makubwa yaliyotokea nchini China.

Idhaa ya Kiswahili 2004-09-22