Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-23 18:16:35    
Polio-ugonjwa unaodhuru sana afya ya watu

cri
    Polio ni ugonjwa unaodhuru sana afya ya watu, ingawa ugonjwa ulidhibitiwa na kuondolewa katika nchi na sehemu nyingi duniani, lakini hivi karibuni ugonjwa huo unaenea sana katika sehemu za magharibi na za kati barani Afrika, na kufuatiliwa sana na shirika la afya duniani WHO.

    Mjumbe wa WHO nchini Cote d'Ivoire tarehe 15 alisema kuwa, kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu, polio imegunduliwa katika nchi nyingi za Afrika Magharibi na kati. Hii inamaanisha kuwa, kuondoa polio kabla ya mwishoni mwa mwaka 2005 ni changamoto kubwa inayolikabili bara la Afrika.

    WHO na washiriki wake walifanya juhudi za kutokomeza ugonjwa wa polio duniani kuanzia mwaka 1988, na kujitahidi kutimiza lengo hilo mwishoni mwa mwaka 2005. Wakati huo, polio inaenea katika nchi zaidi ya 40 barani Afrika. Mwezi Julai, mwaka 1996, mkutano wa viongozi wa OAU ulitoa taarifa ya Yaounde nchini Cameroon, na kuonesha nia ya kuondoa ugonjwa huo unaotishia afya na maisha ya watoto.

    WHO ilianza kutekeleza mipango ya kimkakati ya kutokomeza ugonjwa wa polio barani Afrika kuanzia mwaka 1997, kuhimiza kwa nguvu nchi zinazohusika kutoa chanjo ya polio. Kutokana na juhudi za nchi za Afrika, kuenea kwa polio barani Afrika kulidhibitiwa, nchi 44 za Afrika zilifanikiwa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

    Lakini mwaka 2003, virusi vya polio vilivyoibuka nchini Nigeria na Niger vilianza kuenea nchini Benin, Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Cote d'Ivoire, Ghana na Togo. Mwaka 2004 wagonjwa wapya wa polio waligunduliwa katika nchi hizo, na wengine waligunduliwa nchini Botswana, Guinea, Mali na Sudan.

    Kutokana na takwimu za WHO, wagonjwa zaidi ya 570 walitokea katika Afrika Magharibi, kati yao wanigeria ni 526, wa-Niger 19, wa-Cote d'Ivoire 12, wabenin 6, waburkina Faso 6, wamali 2 na mguinea 1.

    Kutokana na hali hiyo, WHO na mashirika mengine ya kimataifa yaliamua kuchukua hatua za kupambana na polio. Baada ya kutoa chanjo ya polio katika nchi zaidi ya 20 barani Afrika kuanzia mwezi Oktoba mwaka jana, WHO na UNICEF zilipanga kutoa chanjo ya polio katika nchi za Afrika Magharibi na za kati kuanzia tarehe 8, Oktoba mwaka huu. Mbali na hayo, mashirika hayo pia yanatoa sindano ya Vitamin A na kutoa chanjo ya surua katika nchi 22 za Afrika Magharibi na kati. Inakadiria kuwa, watoto milioni 74 wenye chini ya umri wa miaka 5 watapewa chanjo hizo.

    Ili kufanikiwa kuzuia kuenea kwa polio katika Afrika Magharibi na kati mwishoni mwa mwaka 2004, WHO inashirikiana na nchi zinazohusika kuomba jumuiya ya kimataifa kutoa misaada, ili kuhakikisha mapambano dhidi ya polio yanaendelea vizuri. Aidha, WHO pia inafikiria kufanya mkutano wa kikanda wa viongozi wa kuondoa tatizo la polio barani Afrika kila mwaka. Hivi sasa, WHO inajitahidi kufanya majadiliano na ECOWAS na Umoja wa Afrika kuhusu jambo hilo. WHO inatumaini kufanikiwa kuzuia kuenea kwa polio baada ya hatua hizo mfululizo, na kutimiza lengo la kuondoa kabisa ugonjwa huo ulimwenguni kama ilivyopangwa.

2004-09-23