Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-28 13:30:24    
Sikukuu ya Mwezi ya Wachina

cri

    Tarehe 28 Septemba ni tarehe 15 Agosti kwa kalenda ya Kichina, siku hiyo ni sikukuu ya mwezi ya Wachina.

    Usiku wa sikukuu hiyo, mwezi ukiwa juu angani ni wa mviringo na mweupe. Wachina wanaona kwamba mwezi kama huo ni ishara ya kuungana kwa jamaa. Siku hiyo, jamaa wanaoishi katika sehemu mbalimbali huungana pamoja, na kula "keki za mwezi" huku wakiburudika kutokana na mbalamwezi nzuri.

    Yapo masimulizi mengi kuhusu sikukuu ya mwezi miongoni mwa Wachina. Sasa nitawasimulia mojawapo: Inasemekana kwamba zamani za kale mbinguni kulikuwako jua kumi, kutokana na joto kali mito ilikauka, binadamu waliishi kwa shida sana. Alikuwako shujaa mmoja aliyejulikana kama Hou Yi, alikuwa na nguvu nyingi mno. Aliangusha jua tisa kwa mshale na kubakiza moja mbinguni. Tokea hapo Hou Yi akajulikana na kuheshimiwa sana kote duniani. Baadaye alimwoa msichana mzuri na mpole aliyeitwa Chang E. Siku moja mungu mmoja duniani alimpa Ho Yi kidonge kimoja cha dawa akimwambia kwamba akila ataishi milele na kufika mbinguni. Lakini siku ya tarehe 15 Agosti kwa kalenda ya Kichina mkewe Chang E kutokana na udadisi akala ile dawa, mara akapaa angani hadi kwenye kasri mwezini. Lakini huko mwezini kulikuwepo upweke, hakukuwa na kitu ila mti mmoja na sungura mmoja tu mweupe. Ingawa binadamu wanataka kuishi milele lakini hawapendi kukaa katika hali ya ukiwa, kwa hiyo wanaona ni afadhali wakae na familia zao kwa furaha.

    Katika historia ya China, kila mwaka siku hiyo wafalme walikwenda kwenye madhabahu ya mwezi kuuabudu. Desturi hiyo ilianzia Enzi ya Qi miaka 2000 iliyopita hadi enzi ya kifalme ya mwisho, Qing. Miongoni mwa raia pia walikuwa na namna yao ya kuabudu mwezi yaani waliandaa matunda na keki mezani. Desturi hiyo iliyoendelea hadi leo imeku ya kuburudika na mwezi tu. Mwezi unapokuwa mbinguni, familia yote huburudika na mwezi huu kwa pamoja huku wakiongea na kula matunda na keki za mwezi.

    Hali ya hewa ya China inagawanyika katika majira manne tofauti. Lakini kwa nini Wachina wanaburudika na mwezi katikati ya majira ya Autumn? Ni kutokana na ukweli kwamba majira ya baridi jotoridi ni baridi sana, haipendezi kuufurahia mwezi nje ya nyumba; majira ya joto jotoridi ni joto, na mawingu hutanda mbinguni yakiziba mwezi; na majira ya Spring, ni msimu wa kilimo, hawana muda wa kuufurahia mwezi; Ila tu majira ya Autumn ambapo jotoridi si baridi wala joto, mbingu hutakata na pia ni majira ya kuvuna, matunda huiva, watu baada ya kufanya kazi kwa mwaka mzima sasa wanaweza kuufurahia mwezi na kufaidika na mazao yao.

    Kila siku hiyo inapofika, watoto hufurahi sana kwa sababu wanaweza kupata keki tamu za mwezi. Kutokana na taarifa desturi ya kula keki za mwezi nchini China ilianzia Enzi ya Tang, miaka 1,500 iliyopita. Keki za sasa za mwezi ni za aina ya vitobosha, ambapo kila sehemu huwa na keki zake maalumu zinazopikwa kwa makini sana.

    Lifuatalo ni shairi moja la watoto liitwalo "kuufurahia mwezi kwa pamoja", shairi hilo lilikuwa linaimbwa sana na wenyeji wa Beijing wa zamani, likisema, "Sikukuu ya Mwezi hufika kabla ya mayungiyungi kunyauka, wakati huu kila familia hukata kata keki za mwezi. Sikukuu ya Mwezi ni siku ya kuungana kwa familia. Tule, tunywe na tuuangalie mwezi kwa pamoja."

    Wachina wanaona kwamba sikukuu ya mwezi ni siku ya kuungana kwa familia. Siku hiyo kama mtu akishindwa kuungana na jamaa zake huona upweke akiwa katika hali ya "kuinua kichwa kuangalia mwezi na kuinamisha kichwa kukumbuka maskani".

Idhaa ya Kiswahili 2004-09-28