Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-30 18:11:24    
Wakazi wa Shanghai waweza kuwaona madaktari kwa kutembea kwa dakika 15 tu

cri

    Kila ikifika saa tatu ya Jumatatu asubuhi, mzee Yuan Xuezhong, ambaye anakaa katika ghorofa ya tatu ya jengo moja lililoko katika barabara ya Beiyu mjini Shanghai, huwa anafungua mlango mapema na kutazama nje mara kwa mara, na mtu mmoja aliyemzoea huwa anajitokeza bila kuchelewa. Mtu huyo ni daktari Lu Jianhua kutoka kituo cha huduma ya tiba ya mtaa wa Beixinjing. Kabla ya miaka 6 iliyopita, daktari Lu alipofika huko kwa mara ya kwanza mzee Yuan alilala kitandani kutokana na kufanyiwa operesheni ya kupasua mshipa wa kupumua kutokana na kutokwa damu kwenye ubongo. Wakati ule hakuweza hata kuongea, lakini hivi sasa mzee huyo anaweza kutembea taratibu.

    Hapo zamani, madaktari walikuwa wanakaa hospitali kuwasubiri wagonjwa waliokwenda kuwatafuta, lakini hivi sasa madaktari wanajitahidi kufika katika zahanati za mitaani na majumbani kwa wakazi. Kituo cha huduma za matibabu cha mtaa wa Beixinjing kiliwapanga upya wafanyakazi wa utoaji huduma ya afya wapatao 191, na kuwapanga katika vikundi vya utoaji huduma ya afya, wa wodi na usimamizi. Madaktari wanakwenda mitaani na majumbani kwa wagonjwa kwa kutumia baiskeli. Licha ya kupeleka madaktari kutoa huduma ya afya nje ya hospitali, kituo hicho cha utoaji huduma ya afya kimejenga matawi kumi ya utoaji huduma ya afya ukiwa ni pamoja na kupima nguvu ya msukumo wa damu na kutoa maelekezo ya kiafya kwa watu wenye matatizo.

    Kikiwa "walinzi wa afya" wa wakazi wa eneo hilo, kituo cha utoaji wa huduma ya afya kikishirikiana na mtaa wa Beixinjing, kilianzisha kamati ya kuhimiza huduma za afya inayoshirikisha vitendo vya utawala vya serikali za mtaa na tarafa na wajumbe wa kata katika mfumo wa udhibiti wa maradhi na kuimarisha afya za wakazi. Kutokana na kuungwa mkono na kamati hiyo ya kuhimiza afya, madaktari wa kituo cha utoaji huduma za afya wakitumia muda wao baada ya kazi, walitengeneza mafaili ya afya kwa ajili ya wakazi 101,799 wenye umri wa zaidi ya miaka 15 wa kaya 37,922, ambayo yamehifadhiwa katika kompyuta ili kutoa huduma ya huduma ya afya kwa kuwafuatilia wagonjwa waliogawanyika katika vikundi mbalimbalil kutokana na ugonjwa, vikiwa ni pamoja na vya msukumo mkubwa wa damu, kikoromeo, ugonjwa wa kisukari na saratani.

    Wazo katika kupanga sehemu za kuanzisha matawi ya kituo ni kufikiria kwanza kuwarahisishia wakazi. Kwa kufuata mpango wa mambo ya afya wa mji wa Shanghai, kwa uchache wilaya au mtaa wenye idadi ya wakazi laki moja, inapaswa kuanzisha kituo kimoja cha huduma za afya, na eneo lenye idadi ya watu kutoka elfu 10 hadi elfu 20, linatakiwa kuwekwa tawi moja la kituo cha huduma za afya au zahanati iliyofunguliwa na hospitali. Hivi sasa matawi 422 ya vituo vya huduma za afya yameanzishwa sehemu za mjini, wakati zahanati 2,251 zilianzishwa sehemu za mzunguko wa mji, hivyo wakazi wakitembea kwa miguu kwa muda usiozidi dakika 15, wanaweza kufika kwenye vituo vya huduma za afya au matawi yake.

    Huduma zinazotolewa na vituo vya huduma za afya vya maeneo ya wakazi ya mji wa Shanghai ni za kimsingi na za aina nyingi, ambazo ni pamoja na tahadhari na maambukizi ya maradhi, kuimarisha afya, kurejea katika hali nzuri ya afya baada ya kuugua, pamoja na kueneza elimu ya afya na kutoa maelekezo ya uzazi wa majira badala ya kutoa tiba tu kwa wagonjwa kama ilivyokuwa hapo awali.

    Hivi sasa vituo vya huduma za afya vinaanzisha shughuli za tahadhari na kudhibiti baadhi ya maradhi ya kuambukiza, maradhi ya muda mrefu yasiyo ya kuambukiza, kuimarisha afya za akina mama na watoto, na shughuli nyingine za huduma ikiwemo kutoa chanjo za maradhi ya kuambukiza. Kwa upande mwingine, vituo hivyo vinawahamisha haraka wagonjwa wasiofaa kutibiwa na katika vituo vya huduma za afya na kuwapeleka katika hospitali kubwa au hospitali maalumu. Huduma za afya zinazotolewa na vituo hivyo katika maeneo ya wakazi, zimesifiwa sana na wakazi wa mji huo.

Idhaa ya Kiswahili 2004-09-30