Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-12 20:03:57    
Barua za wasikilizaji 1012

cri

    Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa Kijiji cha Benki Mtoni Kijichi sanduku la posta 2503 Dar es Salaam Tanzania alipokuwa jijini Dar es Salaam alituletea barua akianza kwa salamu kwa wahariri na watangazaji wote wa idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa, na kusema yeye ni mzima na hajambo. Anasema anaendelea na maisha yake akiwa kwenye mapumziko mafupi jijini Dar es salaam na baadaye kurejea huko Shinyanga kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa la Tanzania.

    Anasema anapenda kutujulisha kuwa wakati tukiwatangazia wasikilizaji wetu makala ya kwanza ya mashindano ya ujuzi kuhusu miaka 55 ya kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China yaani Jumapili ya tarehe 15 August 2004, alikuwa yuko jijini Dar es Salaam alisikiliza makala hiyo na pia maswali yake mawili yaliyoulizwa.

    Anasema mpango huu wa mashindano ya ujuzi yanayoendeshwa na Radio China Kimataifa karibu kila mwaka kwa kweli ni mpango mzuri sana wa kuwafahamisha watu wote duniani waielewe vizuri China. Anasema akiwa msikilizaji wetu ataendelea kuwa mshiriki hai wa vipindi vyetu, kutoa maoni na ushauri mbalimbali na pia kujiunga na mashindano ya ujuzi yanayotangazwa na Radio China Kimataifa.

    Bwana Kulwa anasema katika barua yake hii ya leo angependa kutoa ushauri kwamba kwa miaka ijayo tunapotoa shindano fulani, kama tunataka kuwafahamisha watu wengi zaidi wa nchi zinazozungumza Kiswahili ni vizuri kama tungechagua baadhi ya magazeti maarufu yanayochapishwa katika nchi hizo na tutoe tangazo katika magazeti kuhusu shindano lenyewe na anuani.

    Ushauri wake huu ni mzuri, lakini labda kutokana na hali yetu halisi ni vigumu kufanya hivyo kwa sasa. Kwani hivi sasa ni rahisi zaidi kwetu kutoa tangazo la kuendesha mashindano ya chemsha bongo kwenye tovuti yetu, lakini tunajua kuwa kwa wasikilizaji wengi wa nchi za Afrika si rahisi kupata nafasi ya kutembelea tovuti, lakini tuna imani kuwa kadiri utandawazi wa uchumi unavyoendelea duniani, ndivyo hali hiyo inavyoweza kubadilika, ambapo wasikilizaji wetu wengi watatembelea tovuti yetu ili kupata habari mapema kuhusu mashindano ya chemsha bongo yanayoandaliwa na Redio China Kimataifa.

    Bwana Kulwa anasema vilevile tungetaja na zawadi zitakazotolewa kwa washindi wa shindano hilo. Kwani njia hii inaweza kuongeza washiriki wengi zaidi wa mashindano hayo kutoka nchi za Afrika mashariki. Inabidi mbinu mbalimbali zitumike ili kuongeza washiriki wa mashindano hayo kutaka Afrika mashariki.

    Vinginevyo baadhi ya wasikilizaji wanaweza kufikiria kuwa kuna ubaguzi na upendeleo wa namna fulani miongoni mwa idhaa na lugha zinazotangazwa na Radio China kimataifa katika kutoa tuzo kubwa kama ile mialiko na kadhalika. Anasema anaomba Jambo hili tulifikirie kwa makini sana.

    Kuhusu suala hili tunapenda kuwaambia wasikilizaji wetu kuwa tumewahi kusema kuwa sisi tunafanya juhudi kila mara kadiri tuwezavyo kuwasaidia wasikilizaji wetu wapate ushindi wa nafasi maalum bila upendeleo. Mkumbuke kuwa katika idara zote 43 za Radio China kimatazifa nazo zinafanya vivyo hivyo . Kwa hivyo tunasema hakuna upendeleo kabisa. Wasikilizaji wote wa Radio China kimatazifa wana nafasi sawa.

    Na mwisho tunapenda kuwakumbusha wasikilizaji wetu kuwa makala zetu za chemsha bongo zimeshawekwa kwenye tovuti yetu katika kipindi cha sanduku la barua, karibuni mtembelee tovuti yetu na msome makala hizo, ili muweze kujibu maswali vizuri.

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-12