Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-14 19:01:46    
Maendeleo ya mikahawa nchini China

cri
    Tarehe 9 jioni, baada ya kurudi nyumbani kutoka kazini Bw. Chang Jiang pamoja na mkewe na mtoto wake walikwenda kwenye mkahawa mmoja uliopo karibu na nyumbani kwake, waliagiza vitoweo vya aina tatu, walikuwa wanakula na huku wakiongea. Kula kwenye mikahawa, hivi sasa limekuwa ni jambo la kawaida kabisa kwa wananchi wa China, na mkahawa huo ni moja tu kati ya mikahawa milioni 3.5 iliyopo nchini China.

    Katika miaka ya karibuni, kutokana na kuwa maisha ya wananchi wa China kuwa bora, fikra za namna ya kuendesha maisha zimebadilika, watu wengi zaidi wanapendelea kula kwenye mikahawa badala ya kujipikia nyumbani. Wanakula katika mikahawa sio kwa ajili ya tafrija ya sikukuu, siku za harusi au kujumuika kwa marafiki, bali ni jambo la kawaida kwa watu wengi wa China.

    Kabla ya miaka 20 iliyopita, mjini Beijing kulikuwa na mkahawa moja tu binafsi. Mwezi Oktoba mwaka 1980, Bi. Liu Guixian aliyekuwa na umri wa miaka 46 wakati huo, kwa kutumia pesa alizokopa kutoka kwa mtu binafsi yuani kumi kadhaa na mkopo wa yuani 500 kutoka benki alianzisha mkahawa moja karibu na nyumbani kwake mjini Beijing. Jamaa yake alisema "Wakati huo kuanzisha mkahawa ilikuwa ni njia ya kujipatia riziki tu".

    Naibu katibu mkuu wa Shirikisho la Wapishi la China Bw. Bian Jiang alisema, "Lakini sasa shughuli za mikahawa sio tena njia ya kuendesha maisha, bali imekuwa aina moja ya utamaduni wa chakula na ni biashara inayostawi kwa nguvu nchini China."

    Mageuzi ya kiuchumi nchini China yameleta maendeleo ya haraka ya uchumi wa China na kutokana na jinsi mageuzi yanavyoendelea shughuli za mikahawa pia zinastawi haraka. Baada ya miaka 20 kupita, sasa kumekuwa na mikahawa milioni 3.5 nchini China, na wafanyakazi zaidi ya milioni 18 katika mikahawa.

    Bi. Yao Nan anayefanya kazi katika shirika moja la kigeni, hana muda wa kupika kutokana na shughuli nyingi, karibu kila siku anakula mkahawani. Baadhi ya wakati anakula peke yake na baadhi ya wakati anawaalika wengine, malipo ya chakula ni kiasi cha yuani kumi hivi, na malipo makubwa hayazidi yuani mia tano. Bi. Yao Na alisema, "Maisha yangu hayawezi kuachana na mikahawa."

    Idadi kubwa ya wateja inasukuma mbele shughuli za mikahawa, hivi sasa mikahawa imekuwa sekta inayostawi kwa nguvu katika soko la matumizi ya wateja. Taarifa za hivi karibuni kutoka Wizara ya Biashara ya China zinasema kuwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2004 biashara ya mikahawa ilikuwa yuani bilioni 337.31, hili ni ongezeko la 24.5% kuliko mwaka jana. Mikahawa nchini China imekuwa ya aina nyingi, kuna aina ya mikahawa kwa umma na pia kuna aina ya mikahawa ya chakula maalumu, shughuli za mikahawa imekuwa ni biashara kubwa nchini China.

    Ingawa mikahawa inaongezeka haraka, lakini uendeshaji wake pia una matatizo yake. Kutokana na ongezeko la mikahawa, ushindani kati yao umekuwa mkali, hali hiyo inawapasa wenye mikahawa kuiendesha kwa kufanya mageuzi mara kwa mara na kujitahidi kutoa huduma bora zaidi. Baadhi ya mikahawa hairidhiki na maendeleo yake katika mji mmoja tu, bali inaanzishwa katika miji mingine na hata katika nchi za nje. Baadhi ya mikahawa licha ya huduma za chakula mikahawani, pia inapika vyakula vyenye chapa zao na kuviuza, na baadhi ya mikahawa imeanzisha shule za kuandaa wapishi.

    Bw. Bian Jian alisema, "Kutokana na maisha bora ya wananchi, shughuli za mikahawa zitastawi kwa nguvu."

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-14