Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-15 16:21:33    
Kiwanda cha Nguo cha Waridi Nyeupe cha Tianjin, China nchini Misri

cri
    Kijana wa Misri aitwaye Saidi aliwahi kuwa mshonaji wa nguo, sasa pamoja na vijana wengine 29, yeye ni mfanyakazi rasmi wa Kiwanda cha Nguo cha Waridi Nyeupe. Tangu awe mfanyakazi wa kiwanda hicho mwezi uliopita, baada ya kufundishwa na walimu kutoka China, Bw. Saidi sasa anaweza kufanya kazi za kawaida mwenyewe.

    Kiwanda cha Nguo cha Waridi Nyeupe cha Tianjin China kilianzishwa mwezi uliopita kwenye Eneo Maalum la Kiuchumi la Suez nchini Misri. Eneo hilo la kando ya Mto Suez liko umbali wa kilomita 120 kutoka Cairo, mji mkuu wa nchi hiyo, na kilomita 40 kutoka mji wa Suez. Mkoa wa Suez ni mkoa muhimu wa kiuchumi nchini Misri, unajulikana kama mlango wa biashara wa nchi hiyo na nchi za kigeni kama vile za Afrika Mashariki, uarabuni na Asia ya Kusini Mashariki.

    Kiwanda cha Nguo cha Waridi Nyeupe kilichoko kwenye sehemu nambari 3 ya Eneo Maalum la Kiuchumi la Suez, ni kiwanda cha kwanza cha China kwenye eneo hilo. Kiwanda hicho kina karakana yenye eneo la mita 2000 za mraba, na vifaa mbalimbali vya kisasa vya kutengezea nguo.

    Meneja mkuu wa kiwanda hicho Bw. Yang Zhongshen alieleza kuwa vifaa vyote hivyo vilitengenezwa nchini China. Alimwambia mwandishi wa habari kwamba, kiwanda hicho kilichoanzishwa na kampuni ya mkoa wa Tianjin China sasa kina uwezo wa kutengeneza nguo zaidi ya laki 6 za hali ya juu kila mwaka, nguo nyingi hizo zinauzwa katika masoko ya nchi za Ulaya, na chache zinauzwa nchini Misri.

    Bw. Yang Zhongshen alisema kuwa, makampuni ya China yanaweza kufaidika na sera mbalimbali za kipaumbele kama vile ushuru na kadhalika yalipoanzisha shughuli zao kwenye Eneo Maalum la Kiuchumi la Suez, mbali na hayo viwanda vya nguo vya China nchini Misri pia vinaweza kuepuka vizuizi mbalimbali vilivyowekwa na nchi za magharibi vinapouza bidhaa kwenye masoko ya nchi hizo. Hayo ni madhumuni ya kampuni ya Tianjin kuanzisha kiwanda nchini Misiri.

    Bw. Yang Zhongshen alieleza kuwa, mpaka sasa Kiwanda cha Nguo cha Waridi Nyeupe kimetengewa dola za kimarekani laki 8 za kimarekani na upande wa China, na kimeajiri wafanyakazi 30 wa Misri, ambapo kitaajiri wengine 30 mwezi ujao. Akasema kuwa kama shughuli za kiwanda hicho zikiendelea vizuri, kampuni ya China inataka kutenga fedha zaidi ili kupanua uwezo wa uzalishaji.

    Meya wa Mkoa wa Suez Bw. Jalale aliwahi kutembelea China ukifuatana na rais Mubaraq wa Misri. Katika ziara hiyo, ujumbe wa serikali ya Misri ulitembelea Eneo Maalum la Kiuchumi la Mkoa wa Tianjin. Baada ya kurudi, rais Mubaraq alimteua Bw. Jalale kuwa mkuu wa mkoa wa Suez, na kumwelekeza aanzishe Eneo Maalum la Kichumi la mkoa huo kwa kuiga mfano wa Tianjin. Mwezi uliopita wakati Kiwanda cha Nguo cha Waridi Nyeupe cha Tianjin, China kilipoanzishwa, Bw. Jalale alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe ya ufunguzi. Alitembelea karakana na kukisifu sana kiwanda hicho. Alipohojiwa na mwandishi wa habari, alisema kuwa Kiwanda cha Nguo cha Waridi Nyeupe cha Tianjin, China, ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya mkoa wa Suez wa Misri na Mkoa wa Tianjin, China. Alieleza kutarajia makampuni mengine zaidi ya China kwenda nchini Misiri kuanzisha shughuli.

    Naibu katibu mkuu wa serikali ya Tianjin China Bw. Chai Zhongda mwezi Agosti mwaka huu alitembelea Misri, na alihudhuria sherehe ya ufunguzi wa Kiwanda cha Nguo cha Waridi Nyeupe. Alisema kuwa, mkoa wa Tianjin ungependa kuzidisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na Misri. Alieleza kuwa, thamani ya biashara kati ya Tianjin na Misri mwaka jana ilikuwa dola za kimarekani milioni 28. Mwaka huu, hadi mwezi Mei, thamani hiyo imefikia dola za kimarekani milioni 13 na laki 9. Hivyo kwa jumla, ushirikiano wa kiuchumi kati ya pande hizi mbili zinapanuliwa kwa mfululizo. Bw. Chai Zhongda alimwambia mwandishi wa habari kuwa, mpaka hivi sasa, kampuni 14 za Tianjin zimeanzisha matawi nchini Misri. Mbali na hayo, Eneo Maalum la Kiuchumi la Tianjin hivi sasa pia linajishughulisha na kazi ya ujenzi wa sehemu nambari 3 ya Eneo Maalum la Kiuchumi la Suez kwa kushirikiana na upande wa Misri.

    Bw. Chai Zhongda alieleza kuwa, ana imani kubwa kwamba, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Misri utakuwa mzuri zaidi katika siku za mbele.

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-15