Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-18 18:37:42    
Mahojiano

cri

    Utambulisho:

    Leo katika kipindi hiki tunaye Miriam Odemba mrembo kutoka Tanzania. Miriam wewe ni mtanzania ambaye mpaka sasa umekuwepo nchini China mwaka mmoja.

    Swali: Kwanza Miriam nieleze unaonaje hali ya maisha ya China ikilinganishwa na ya nyumbani Tanzania.

    M: Kwa kweli nilikuja nchini China mwaka jana mwezi wa 3. Nimefurahia kukaa hapa China, kwa sababu naona kuna maendeleo makubwa na pia naweza kufanya kazi zangu za "model" na kuishi bila matatizo. Naona China kuna maendeleo na kwa sababu hiyo watu wengi wanataka kuishi China. Kutokana na kuja kwangu China na kukaa mwaka mzima nilikutana na rafiki Maria Kargbu anayetoka Sierra Leone ambaye akawa rafiki yangu. Huyu rafiki yangu Maria amenifundisha mambo mengi kwanza ya hapa China na pia katika mambo ya "modeling". Huwa tunakwenda sehemu mbalimbali kufanya maonesho ya mavazi, na tukiwa huko tunakutana na wachina na tunashirikiana nao vizuri. Wachina ni watu wazuri sana, ni wapole, wachangamfu, na hawana ubaguzi kwa watu. Haya ndiyo yamenifanya nivutiwe kukaa hapa China.

    Swali: Miriam sasa hivi wewe ni kama balozi wa Tanzania. Kwani hivi majuzi wewe uliiwakilisha Tanzania na rafiki yako Maria aliiwakilisha nchi yake kwenye mashindano ya kutafuta "miss kite". Tuelezee kidogo mashindano hayo yalikuwaje na kulikuwa na wagombea wangapi kutoa Afrika.

    M: katika mashindano hayo ya miss kite tulikuwa wasichana 150, wagombea kutoka karibu kila pembe ya duniani walikuja hapa China kwenye mji unaoitwa Wei Fang mkoani Shandong kushiriki kwenye mashindano hayo. Katika hao 150 walihitajika wasichana 20, mimi na rafiki yangu Maria tukabahatika kuwa kati ya hao 20, halafu kati ya hao 20 tukachujwa na kubaki wasichana 10, na kati ya hao tukachujwa na kubakia watano mimi na rafiki yangu tulibahatika na kufika hatua hiyo ya mwisho ya 5 bora. Mimi nimeingia katika tano bora nimekuwa mshindi wa nne katika mashindano ya miss kite.

    Miss kite ni mashindano mazuri pia kwa Tanzania na kwa Afrika. Hawa wenzetu wanataka kuitangaza "kite" (tiara) kwa kupitia mashindano haya, na wanataka kuitangaza hata kwa kutembelea nchi za Afrika. Kutokana na nafasi niliyopata, serikali ya Wei Fang inasema inapenda kwenda Tanzania kuona kama kuna uwezekano wa kuitangaza "kite" Tanzania.

    Swali: Kwa jinsi ilivyozoeleka Tanzania au hata Afrika Mashariki kurusha tiara ni mchezo unaofanywa na watoto, lakini huku China inaonekana kuwa ni watu wazima zaidi wanaofanya hivyo. Inaonekana hata nchi nyingine nako ni wakubwa watu wazima wanaoshiriki. Unadhani kuwa mashindano hayo yakipelekwa Tanzania au hata utamaduni huo ukipelekwa Tanzania utapokelewa na watanzania?

    M: kwa kweli naamini watanzania wataupokea utamaduni wa China, kwa sababu hiki ni kitu kama kipya lakini si cha ajabu kwa watanzania. Hata mimi nikiwa mdogo nakumbuka nilikuwa napenda kupeperusha tiara. Tulikuwa tunatengeneza tiara kwa kutumia magazeti, lakini hapa China, tiara inatengenezwa kwa ufundi sana. Nadhani itakuwa ni vizuri tiara za China zitaenda Tanzania kwani watanzania tutaachana na kukata magazeti na kutumia tiara za China, na itakuwa ni vizuri sana kwa watoto wa Tanzania.

    Swali: Watanzania wengi kwa kweli wanafahamu kwamba China ni nchi rafiki kwa nchi ya Tanzania, lakini bado wako watu wa kawaida kama wewe hawamfahamu hasa urafiki wa wachina kwa watu wengine katika maisha ya kila siku.

    M: Ni kweli wengi wanafahamu wachina ni marafiki wa watanzania. Hata katika maisha ya kawaida wachina walio wengi ni watu wenye upendo, huruma, labda ndiyo maana hata nchi yao inapata maendeleo. Nchi yao kwa sasa hivi ina maendeleo makubwa sana, na kweli ningependa hata sisi katika nchi yetu Tanzania, tufuate mwelekeo wachina. Najua kuwa sisi watanzania pia tunapendana sana na tunawapenda wenzetu, hilo tayari tunalo ninachopenda kuwaambia watu wa nyumbani ni kuwa tuchape kazi tuige mfano wa China.

    Swali: Unaona ni tofauti gani zilizopo kati ya mila na desturi za China na Tanzania.

    M: Mila na desturi za Tanzania ni tofauti na za kichina. Kwenye mambo ya chakula, wachina wanapenda kupika kwa kuchemsha lakini sisi watanzanina tunapenda kutumia nazi kama kupika wali na wao wachina wanapika kwa maji ni tofauti sana lakini katika umoja tunashirikiana. Halafu chai ya kichina ni nzuri sana. Chai ya kichina inapunguza mafuta mwilini hilo ni moja ya niliyojifunza katika masomo yangu hapa China kutoka kwa marafiki zangu wachina, Marafiki zangu wa kichina waliniambia nikinywa chai ya China inapunguza mafuta kwa ujumla vyakula vyao vinafanya mtu usiwe mnene.

    Swali: Kwa hivyo ninyi mnaofanya mambo ya urembo, mnaona wembamba ni mzuri kwenu, kwa hivyo mnaona kula chakula cha kichina kunafaa?

    M: Ndiyo. Chakula cha kichina ni kizuri sana kinasaidia kupunguza mwili. Pia ningependa kuwashauri watanzania wasiwe na mawazo ya ajabu kuhusu China kwa sababu ni nchi ambayo iko Asia, na kudhania kuwa ni nchi ambayo haina maendeleo. China kuna kila kitu sasa hivi China ni Marekani ya pili, kwa sababu watanzania wengi wanapenda Marekani, wanapenda kwenda England, hawamfahamu kuwa China ni nchi wafanyabiashara. China ni cnhi nzuri tu kama wakiweza kuja waje.

    Mwisho: wasikilizaji wapendwa huyo ni Miriam odemba mrembo kutoka Tanzania akiongea nasi katika kipindi hiki cha utamaduni, na kufikia hapa basi ndiyo tunakamilisha kipindi hiki asanteni na kwa herini

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-18