Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-20 18:21:44    
Pato la wakazi wachina laongezeka kwa mfululizo

cri

    Tarehe 1 mwezi Oktoba ni miaka 50 kamili ilitimia tangu kuasisiwa China mpya. Katika miaka hiyo, uchumi wa taifa umepata maendeleo makubwa na kiwango cha maisha ya wananchi kimeinuka kadiri uchumi wa taifa unavyokuwa.

    Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, wastani wa pato la mkazi wa mjini ulikuwa ni Yuan 4,815, baada ya kuondoa kiwango cha mfumuko wa bei, ongezeko la pato lilikuwa 8.7%, ikiwa ni ongezeko la 0.3% kuliko lile la mwaka jana katika kipindi kama hiki. Wastani wa pato la mkazi wa kijijini ulikuwa Yuan 1,345, ongezeko halisi lilikuwa 10.9%, na ni ongezeko la 8.4% kuliko lile la mwaka jana katika kipindi kama hiki, ambalo ni kubwa zaidi tokea mwaka 1997.

    Ukifungua kitabu cha kumbukumbu ya mwaka 1989, 1997, 2001 na 2003, utaona kuwa wastani wa mapato ya mkazi wa mjini ulikuwa Yuan 1374, Yuan 5160, Yuan 6860 na Yuan 8500; wakati wastani wa pato la kila mkazi wa kijijini ulikuwa Yuan 602, 2090, 2366 na Yuan 2622.

    Pamoja na kuongezeka kwa pato la wachina, akiba ya fedha zinazowekwa benki pia inaongezeka kwa mfululizo: mwaka 1989, wastani wa akiba ya fedha zilizowekwa benki kwa kila mchina ulikuwa Yuan 461, mwaka 1997 ulikuwa 3744, mwaka 2001 Yuan 5780 na mwaka 2003 Yuan 7943.

    Ongezeko la pato kwa wakazi wa mijini na vijijini linatokana na maendeleo ya uchumi wa taifa na kutekelezwa kwa sera za serikali za kuongeza pato la wananchi. Tangu kuanza kutekelezwa kwa sera za mageuzi ya kisiasa, wastani wa ongezeko la uchumi wa taifa ulikuwa 9.4% kwa mwaka, hususan ni kwamba uchumi wa aina mbalimbali ukiwemo uchumi binafsi umekuwa na nguvu, ambao umechangia ongezeko la pato la wachina. Ili kuinua kwa mfululizo kiwango cha maisha ya wananchi na kukuza mahitaji ya nchi, katika miaka ya karibuni serikali ilitumia mbinu ya kuongeza kiwango cha mshahara na kuweka kima cha chini cha dhamana ya maisha, kuhimiza mageuzi ya kodi vijijini na kupunguza au kusamehe kodi za kilimo, hatua ambayo iliongeza moja kwa moja mapato ya wakazi wa mijini na vijijini.

    Tukichukua mfano wa ongezeko la pato la wakulima, tangu sera ya mageuzi na kufungua mlango kwa nje ianze kutekelezwa, serikali kuu kwa nyakati tofauti ilibuni maagizo 6 kuhusu vijiji, kilimo na wakulima, na kutunga sera za kuongeza pato la wakulima na msaada kwa wakulima. Bajeti ya serikali kuu ya mwaka huu ya kusaidia sehemu ya vijiji imeongezeka kwa Yuan bilioni 30 kuliko ya mwaka jana, na ruzuku iliyotolewa na serikali katika nusu ya kwanza ya mwaka huu kwa uzalishaji wa nafaka ilifikia Yuan bilioni 11.6. Kutokana na msaada wa sera za serikali, wastani wa pato la mkazi wa kijijini uliongezeka na kufikia Yuan 1,578 katika mwaka 1995 kutoka Yuan 686 mwaka 1990, na kufikia Yuan 2,622 katika mwaka 2003. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, ongezeko la pato la wakulima limefikia kiwango cha juu zaidi katika miaka iliyopita.

    Idara husika imekadiria kuwa kwa zaidi ya miaka kumi ijayo, pato la taifa (GDP) litaongezeka kwa kiwango cha zaidi ya 7%. Lengo la mbali la maendeleo ya uchumi ni kuinua kiwango cha maisha ya wananchi, kwa hiyo maisha ya wachina yataboreshwa kwa haraka na kwa kiwango kikubwa zaidi katika miaka kumi ijayo.

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-20