Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-21 16:02:17    
Tanzania na China zaimarisha ushirikiano wa kidiplomasia ili kukabiliana na changamoto ya utandawazi

cri

 

katibu wa kudumu wa wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Tanzania Bwana Phillemon L.Luhanja  

    Kutokana na mwaliko wa waziri wa mambo ya nje wa China, katibu wa kudumu wa wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Tanzania Bwana Phillemon L.Luhanja tarehe 13 Oktoba alifanya ziara nchini China. Yafuatayo ni mazungumzo kati ya Bwana Luhanja na mwandishi wetu wa habari.

    Suali--Kwanza tafadhali tuelezee kidogo hali ya uhusiano kati ya Tanzania na China.

    Jibu-Uhusiano kati ya Tanzania na China ni mzuri mno, umedumu kwa miaka 40. na katika miaka hii 40, tumekuwa na uhusiano wa karibu, viongozi wetu waasisi na waliofuatia wameendeleza ushirikiano kati ya nchi hizi mbili, na unazidi kuendelea. Siku za karibuni kumekuwa na ziara nyingi za viongozi mbalimbali wa kisiasa na watendaji ili kuimarisha uhusiano ambao umedumu miaka 40.

    Na katika miaka 40 iliyopita, kwa upande wa Tanzania tungeweza kusema kuwa, serikali na watu wa China wametusaidia katika mambo mengi makubwa hasa katika maswala ya miundombinu. Jambo kubwa ambalo tunajivunia ni ujenzi wa uhuru, kiwanda cha nguo cha urafiki, viwanda vya majembe. Hivi karibuni tena China imetekeleza mradi mkubwa wa maji katika mkoa wa Pwani, wilaya ya Bagamoyo, Chalinze, watu waliopata shida ya maji sasa wameanza kupata nafuu.

    Hivi karibuni rais William Benjamin Mkapa alikuja China kwa ziara, na mojawapo ya makubaliano ni ujenzi wa kiwanja cha michezo. Hii ni jambo kubwa sana. Na bado tunaendelea kushirikiana na hata mimi nimekuja kufuatilia baadhi ya masuala amabyo yamekubaliana ili tuweze kuyafuatilia na kuyatekeleza.

    Suali-Katika miaka ya hivi karibuni, mabadiliko makubwa yametokea duniani, ikiwa ni pamoja kwa Tanzania na China, je ushirikiano kati ya Tanzania na China sasa umekuwaje na utakuwaje katika siku zijazo?

    Jibu- Uhusiano wa Tanzania na China kwa sasa na siku zijazo utakuwa mkubwa zaidi. Kwa sababu tumeshakubaliana kama serikali mbili kufanya kazi pamoja kwa karibu sana hasa tukizingatia kwamba, tunaishi katika ulimwengu wa utandawazi, tukiungana na serikali ya China tutaendelea kulizungumzia suala hili la kwamba utandawazi uweze kunufaisha kila mtu. Kwa hiyo tutakuja kupigania suala la usawa katika masuala ya biashara, iwe biashara halali na inayozingatia usawa katika biashara. Hata leo tunazungumzia hilo suala na waziri wa mambo ya nje wa China Bwana Li Zhaoxin kwamba katika masuala ya kimataifa itabidi tushikamane, tuzungumze lugha moja wote wawili.

    Suali-Unaonaje sera ya kidiplomasia ya China kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika?

    Jibu-Kwanza nashukuru. Nimebaini kwamba, China imepiga hatua kubwa sana katika maendeleo. Sasa China imeanza kutoka nje kutaka ushirikiano hasa na nchi za Afrika. Kwa sababu inataka kushirikisha mbinu mbalimbali za maendeleo, kwa hiyo sasa hivi kidiplomasia nafikiri China inakwenda vizuri. Tayari imekwisha anzisha uhusiano na Afrika, ushirkiano wa China na Afrika tayari umefanya mikutano miwili. Kwa hiyo nafikiri imeanza kubadilika vizuri sana. China inataka kushirikiana na Afrika, na sisi waafrika pia tunafurahi kushirikiana na mwenzetu, ambayo ni nchi inayoendelea, lakini sasa imepiga hatua kubwa mbele, tutajifunza mbinu mpya ambazo mwenzetu China imetumia ili kwenda haraka katika maendeleo.

    Suali-Lengo lako la ziara hii nchini China ni nini?

    Jibu-Lengo langu la kuja China kuna mambo mawili, la kwanza ni kuonana na viongozi wa serikali ya China kujadiliana kuhusu utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili uliotiwa saini mwaka 2001. Nakuja ili tukae pamoja na tutafsiri vipengele mbalimbali ili tuanze kutekeleza sasa. Leo nimefanya mazungumzo na waizri wa mambo ya nje wa China Li Zhaoxin, tumeelewana vizuri. Tutakutana katika ngazi mbili za mawaziri na watendaji, Tanzania tumeialika serikali ya China kuja kuhudhuria mkutano wa kwanza unaotarajiwa kufanyika Dar es Salaam mwaka kesho mwezi Aprili.

    La pili, tumekubaliana kwamba, balozi zetu zote wakutane, kubadiliana mawazo kila wakati na kila pahali na watoe ripoti kwa Beijing na Dar es Salaam. Hasa katika balozi zile za kimataifa huko New York, Brussels, Geneva na Nairobi, ili tupate misimamo ya pamoja katika mambo ya kimataifa.

    Na mambo mengine tunayozungumzia ni kubadilishana wataalamu au wafanyakazi na suala la mafunzo.

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-21