Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-22 19:04:32    
Balozi wa China nchini Afrika kusini adai kuwachukulia hatua za kisheria wahalifu waliowaua raia 2 wa China

cri

    Tarehe 18 Oktoba mwezi huu, balozi wa China aliyeko nchini Afrika ya kusini Bwana Liu Guijin alionana kwa dharura na Ofisa wa wizara ya mambo ya nje ya Afrika ya kusini kuhusu tukio la raia wawili wa China kuuawa tarehe 17 nchini humo, na kuitaka Afrika ya kusini kuwachukulia wahalifu hatua za kisheria haraka iwezekanavyo.

    Tovuti ya mtandao ya wizara ya mambo ya nje ya China ilitoa taarifa ikisema kuwa, balozi Liu Guijin alisema tokea mwaka huu, raia kadhaa wa China waishio nchini Afrika ya kusini waliuawa, lakini hadi leo bado hakuna mhalifu hata mmoja aliyechukuliwa hatua za kisheria. Jambo hilo si kama tu limeleta tishio kubwa kwa maisha na mali za wachina waishio nchini Afrika ya kusini, bali pia limeleta athari mbaya kwa ushirikiano wa kawaida wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika ya kusini, na kupaka matope sifa ya kimataifa ya Afrika ya kusini. Viongozi na serikali ya China inafuatilia sana jambo hilo, ikitumai kuwa serikali ya Afrika ya kusini itachukua hatua mwafaka kulinda usalama wa maisha na mali za wachina waishio nchini Afrika ya kusini, na kutilia mkazo kazi ya kushughulikia kesi hiyo, kuwachukulia wahalifu hatua za kisheria haraka iwezekanavyo.

    Bwana Liu Guijin alisisistiza kuwa, serikali mbili za China na Afrika ya kusini zimeidhinisha makubaliano ya ushirikiano ya polisi kati ya China na Afrika ya kusini, mkataba wa kubadilishana wahalifu wa China na Afrika ya kusini na mkataba wa kusaidiana kisheria, makubaliano hayo yameweka hali nzuri katika pande mbili kupambana kwa pamoja na uhalifu wa kijamii wa Afrika ya kusini. Pia aliwaambia wachina waishio nchini Afrika ya kusini kufuata sheria za nchi hiyo na kutilia maanani usalama wao wenyewe.

    Naibu mkuu wa idara inayoshughulikia mambo ya Asia na mashariki ya kati ya wizara ya mambo ya nje ya Afrika ya kusini Bwana Sucral alitoa rambirambi kutokana na vifo vya raia wawili wa China, na kusisitiza kuwa, hali ya wasiwasi ya usalama ni tatizo la siku nyingi lililoko nchini Afrika ya kusini. Amesema serikali ya Afrika ya kusini inapenda kufanya mashauriano na China katika kupambana kwa pamoja na uhalifu.

    Bwana Shang Guoxing kutoka Shanghai na Li Wensheng kutoka mkoa wa Hunan tarehe 17 waliporwa na kupigwa risasi na majambazi watatu katika kiwanda chao umbali wa kilomita 75 kutoka mji wa Bloemfontein, mji mkuu wa sheria. Watuhumiwa hao watatu wamekamatwa na polisi wa Afrika ya kusini, watafikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza tarehe 19.

    Konsela wa China aliyeko mjini Johannesbourg Bwana Tang Qinghuang aliitaka polisi ya Afrika ya kusini kufuatilia kesi hiyo kwa makini ili watuhumiwa wasije kuachiwa huru kwa dhamana.

    Kutokana na sheria ya Afrika ya kusini, hatia ya uuaji ikithibitishwa, adhabu ya juu kabisa kwa washitakiwa ni kifungo cha maisha.

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-22