Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-22 19:14:44    
Hifadhi ya Mtindo wa Kale wa Mji wa Beijing

cri

    Beijing ambao ni mji mkuu wa China ni mji maarufu wenye historia ndefu ya utamaduni. Katika miaka ya karibuni, kadiri ujenzi wake unavyoendelea ndivyo hifadhi ya mtindo wake wa kale inavyotiliwa maanani. Siku chache zilizopita idara inayohusika imetoa programu ya kuhifadhi mtindo wake wa kale, programu ambayo imeweka wazi kanuni kuhusu barabara, vichochoro, urefu wa majengo, mtindo na rangi za majengo na hifadhi ya miti maarufu na ya miaka mingi.

    "Programu ya kuhifadhi mtindo wa kale wa mji maarufu wenye historia ndefu ya utamaduni" umeweka mipaka ya hifadhi yake. Kuhusu programu hiyo Bw. Song Xiaolong, mkurugenzi wa Taasisi ya Mipango ya Ujenzi wa Mji wa Beijing alieleza kuwa lengo la kutunga programu hiyo ni kuhifadhi mtindo mahsusi wa Beijing kadiri iwezekanavyo wakati mji unapoendelea katika ujenzi wake wa kisasa.

    Historia ya mji wa Beijing inaweza kufuatiliwa hadi mwaka 1045 K.K., ambapo hadi leo mji huo una miaka zaidi ya elfu 3, ni mji mkubwa kabisa na kamili kati ya miji mikuu ya kifalme katika historia ya China. Humu mjini lipo kundi kubwa la kasri, mtindo wa mji wa kale, mpangilio wake wa ujenzi na zipo kumbukumbu nyingi za utamaduni.

    Hivi leo ujenzi wa Beijing unakwenda haraka; mabadiliko yaonekana kila kukicha. Hifadhi ya mji huo maarufu wa kihistoria imekuwa tatizo katika maendeleo ya ujenzi wa mji huo. Bw. Song Xiaolong alipozungumzia tatizo hilo alisema kuwa katika miaka iliyopita uharibifu wa mtindo wa mji huo ulitokea kwa kiasi fulani.

    "Tatizo lenyewe ni kuwa katika mji na hasa katika sehemu za nyumba za chini wakazi ni wengi kupita kiasi, kwa muda mrefu tatizo hilo limekuwepo. Pili ni kuwa "mandhari yake ya sehemu kubwa ya nyumba za chini inakabiliwa na changamoto", majengo marefu yanakuwa mengi zaidi na zaidi ambapo uharibifu wa mandhari hiyo unazidi kuwa mbaya. Zaidi ya hayo, awali kabla ya mitindo ya majengo mapya kutiliwa maanani sana, majengo mengi yanaachana sana na mtindo wa kale wa mji huo."

    Kutokana na sababu za kihistoria, sehemu ya mji wa kale ni kiini cha mji. Kwa hiyo mji huo unapohitaji kuendelezwa na kufanyiwa mageuzi, sehemu hiyo imekuwa kipaumbele, matokeo yake ni kuwepo kwa msongamano wa watu na magari. Tatizo la msongamano wa mawasiliano na upungufu wa miundo-mbinu haliwezi kutatuliwa, hali hiyo ni uharibifu mkubwa kwa kumbukumbu za utamaduni wa kihistoria.

    Hivi sasa, ujenzi unaendelea kuikabili Beijing. Katika muda wa miaka mitano ijayo mageuzi ya nyumba chakavu za chini kiasi cha mita za mraba milioni 7 yatakamilika. Mageuzi ya nyumba za zamani na hifadhi ya mtindo wa kale itakuwa mgongano mkali.

    Song Xiaolong alisema, "Mpangilio wa mji wa kale ni sehemu kubwa ya nyumba za chini, na majengo ya juu ni nyumba za kasri, pagoda, madhabahu, hekalu na milango ya kuta za mji, sehemu nyingine zote ni nyumba za chini, mpangilio kama huo ungechukuliwa na majengo marefu ya saruji, mtindo wake wa zamani ungeharibika."

    Lakini, katika mwendo wa maendeleo ya mji, ili kuboresha makazi mageuzi ya nyumba chakavu za chini zenye nyua za mraba ni ya lazima. Ni bahati nzuri kwamba watu wenye madaraka ya maamuzi wametambua zaidi na zaidi tatizo hilo. Katika miaka ya karibuni tume ya jiji imeweka mkazo katika kanuni za ujenzi. Katika miaka miwili iliyopita, tume ya Beijing imeweka sehemu 25 za utamaduni wa kihistoria chini ya hifadhi, eneo la asilimia 17 ndani ya mji limehifadhiwa, hatua ambayo imeokoa mji wa kale kwa kiasi kikubwa. Pamoja na hayo idara za mpangilio wa ujenzi na wafanyabiashara wa majengo pia wametumia njia mwafaka ili kuuendeleza mtindo wa zamani wa Beijing.

    Programu iliyotolewa hivi karibuni kwa kiasi kikubwa imehifadhi mtindo wa zamani wa Beijing, na mipaka yake ya hifadhi imepanuka. Kanuni ndani ya programu hiyo zimewekwa wazi kuhusu ujenzi wa miundo-mbinu, mazingira ya upandaji miti na mtindo wa mji wa kale, kumbukumbu za kihistoria zinahifadhiwa, na ni marufuku kubomoa ovyo yale ya zamani kwa ajili ya kujenga mengine mapya. Bw. Song Xiaolong alisema kuwa ili kukaribisha michezo ya Olimpiki itakayofanywa katika mji wa Beijing, majengo yote ya michezo yanapaswa kufuata kanuni hizo.

    "Programu hiyo imeweka kiwango cha urefu wa majengo, kimsingi hayaruhusiwi kuwa zaidi ya mita 45 kwenye sehemu ya ndani ya mji. Aidha, programu hiyo imeweka mahitaji kwa maumbo ya majengo, rangi za paa na kuta."

    Inasemekana kuwa baada ya kukaguliwa na idara inayohusika programu hiyo itakuwa na nguvu za kisheria. Hii ni mchango mkubwa kwa ajili ya kuhifadhi mji maarufu wa Beijing wenye historia ndefu ya utamaduni.

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-22