Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-26 20:54:57    
Barua za wasikilizaji 1026

cri

    Wasikilizaji wapendwa, ni watangazaji wenu Chen na Fadhili Mpunji tunawakaribisha katika kipindi hiki cha sanduku la barua. Leo kwanza tunawasomea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu, halafu tunawasomea makala walizotuletea wasikilizaji wetu kuhusu Mila za makabila mbalimbali.

    Msikilizaji wetu Noel E. Mashauri wa sanduku la posta 42 Kiomboi Iramba, Singida Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, nia ya barua yake kwanza ni kutushukuru kwa barua zetu tulizomtumia, ambazo ziliambatanishwa na bahasha zilizolipiwa. Pia barua ambayo ilikuwa na karatasi yenye maswali ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa miaka 55 ya China mpya, na aliendelea kusikiliza makala na kuyajibu maswali hayo.

    Anasema yeye binafsi anapenda sana kipindi hicho, kwani kinawapa wasikilizaji ufahamu zaidi kuhusu China ya sasa kwa ujumla. Na kwa niaba ya wasikilizaji wenzake anapenda kuwapa hongera kwa juhudi zao kuu. Na anapenda kutupa taarifa kuwa, kwa sasa walau anaweza kupata vizuri matangazo yetu kuliko pale mwanzo. Mawimbi yametulia na anasikia vizuri ingawa kuna wakati mwingine huwa mawimbi yanaingiliana na ya radio nyingine, ambapo hali hiyo inafanya baadhi ya matangazo hasa ya jumapili ya tarehe 5 Septemba mwaka huu yasisikike vizuri. Kwa maombi yake angeomba tujaribu kuimarisha matangazo yetu ili yasikiuke vizuri zaidi.

    Anasema katika vipindi, yeye hajaona kasoro, kwani vyote vina vitu muhimu kwake ambavyo anapenda kujifunza kuhusu China, na wananchi wake. Pili kuna maswali aliuliza ila majibu yake anafikiri hajayapata. Katika maswali hayo alitaka ajue, ni moyo gani walionao wachina, ambayo hukubali mambo wanayoambiwa pasipo hata kipingamizi na kushirikiana kwa pamoja. Vilevile viongozi hufanya kazi sawa na wananachi,

    Msikilizaji wetu Daud Omari Luhende Kanisani Misufini S.L.P 82 Morogoro Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, Mwezi wa sita na wa saba, ametuma barua mbili, lakini tangu atume hajasikia barua yake ikisomwa hewani. Anasema angependa afahamishwe kama zilifika au la. Pia anasema anapenda kutoa pongezi kwa China kupata medali za dhahabu katika siku ya kwanza ya mashindano ya olimpiki, pia anapenda kutoa pongezi kwa kutimiza miaka 40 tangu kuanzishwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania. Na mwisho ana maswali mawili:

    (1) Je, ni yuan moja ya China, sawa na shilingi ngapi za kitanzania?

    (2) Saa moja kamili jioni saa za Afrika mashariki ni saa ngapi hapo China? .

    -Tunapenda kumwambia kuwa, yuan moja ya China sawa na shilingi 140 za kitanzania kwa hivi sasa.

    -Saa moja kamili jioni kwa saa za Afrika mashariki sawa na saa sita usiku hapa nchini China

    Na anasema, anapenda kutukumbusha tumtumie kalenda, kalamu kitabu cha kujifunza kichina na maswali ya chemsha bongo maana hakuyapata vizuri kwa njia ya redio.

    Wasikilizaji wapendwa, tangu kuanzishwa kwa mashindano ya uandikaji wa makala kuhusu Mila yetu au Mila ya China, tumepokea makala zilizoandikwa na wasikilizaji wetu. Kuanzia leo tutawasomea makala hizo.

    Na msikilizaji wetu Hamad Rashid Sebe SLB 121-80500 Lamu-Kenya ametuletea barua akiandika makala kuhusu mila ya kabila. Makala yake inasema hivi:

    Historia na mila kidogo ya kabila langu la Digo. Kabila hili linapatikana kwenye pwani ya kusini mwa mpaka wa Kenya na Tanzania. Mwazoni kulikuwa na watu wa Mijikenda waliokuwa wakiishi Singwaya, Singwaya ni mwambao wa pwani kusini mwa Somalia, mpaka wa Kenya na Somalia. Waliishi huko Karne ya 16-17, kabla ya kuwa na urafiki na wagalla wanaoishi nchini Somalia. Watu wa Mijikenda walipokuwa na urafiki na wagalla, wakagawanyika kwenye makundi mawili. Kabla ya kugawanyika walikuwa wakiishi pamoja kwenye kaya moja. Watu hao walikuwa wakiishi msituni, msitu ambao watu wa mijikenda wanaamini ina uwezo wa kuwapatia nguvu na kila kitu wanachotaka wakiomba wanapata., katikati ya hiyo kaya kuna kitu kinaitwa Fingo, fingo ndilo la kuwalinda wao hapo kwenye kaya, mijikenda maana yake ni makabila tisa wanaosikilizana kwa lugha, nayo makabila tisa hayo, kabila moja tu ndilo la dini ya kiislamu nalo ni kabila la wadigo.

    Lakini makabila yote manane ni ya waumini wa dini ya kikristo lakini asili yao wote ni moja. Makabila hayo tisa ya mijikenda ni (1) Digo (2) Giriama (3)Kambe (4) Duruma (5) Rabai (6)Ribe (7) Jibana (8) Chonyi (9) Kauma. Baba yao mzee muyeye ambaye alikuwa na wake wawili, mke wa kwanza alikua anaitwa Mbodze, na mke wa pili alikua anaitwa Matseze.

    Mke wa kuanza Mbodze alizaa watoto wanne-Diao, Ribe, Duruma na Rabai, Nabibi wa pili alizaa watoto watano-Giriama, Chonyi, Jibana, Kambe na Kauma. Singwaya pia kulikuwa na makabila ya Taita na Pokomo, baada ya watu wa mijikenda kukorofishana na wagalla hapo singwaya, watu wa Mijikenda wakaanza kuwaua wagalla, halafu katika yale makundi mawili ya mijikenda yaliyo gawanyika kundi moja likasema wa wagalla sio wabaya.

    Lakini kundi lengine likiwemo Digo lilikuwa likipinga. Galla waliposikia wana watetezi, wakadai walipwe fidia ya watu wao waliouwawa. Ndio maana mpaka sasa huku Kenya kuna msemo wa kusema "mgalla muuweni lakini haki yake mpeni" ndio hii fidia waliyotaka kutoka kwa kwa watu wa mijikenda, lakini wao wakakataa kuwalipa fidia na hapo vita vikali vikazuka kati ya wagalla na watu wa mijikenda.

    Walioweza kujikinga wenyewe walijikinga, na wagalla wakaanza mashambulizi makali. Hapo vita vikali vikatokea tena, mpaka watu wa mijikenda, pokomo na Taita wakafukuzwa kutoka kusini mwa somalia, lakini watu wa mijikenda walioweza kujikinga wenyewe walikuwa ni wa kabila la wadigo. Hapohapo wagalla na wadigo wakawekeana mkataba wa mila, wagalla wakasema sisi tutamiliki mwambao wa pwani ya Kenya, huku mpaka wa Kenya na Somalia, Na wadigo watamiliki mwambao wa pwani ya Kenya kule mpaka wa Kenya na Tanzania. Ndio mpaka sasa, mpaka wa Kenya na Somalia mwambao wa pwani ni wagalla asilia wa Somalia mpaka sasa, mpaka wa Kenya na Tanzania mwambao wa pwani ni wadigo. Na makabila yale yenye waumini wengi wa dini ya Kikristo yako malindi, na kilifi (Giriama, Kauma, Ribe, Chonyi, Rabai, Kauma, Kambe na Duruma) Hawa nusu wako wilaya ya kilifi nayo yako " Mariakani" na nusu yako kwenye wilaya ya kwale kule "Kinango".

    Na Taita kuelekea upande wa Nairobi pia watu hufikiri wataita sio watu wa pwani ni wa bara, lakini wa wataita ni wa pwani (Coast Province), na pokomo wako karibu na mto Tana. Kutokea hapo sasa unaona waswahili wako hapa mombasa kisiwani na kule Lamu kisiwani wote walikombolewa na wadigo kutoka kwa wagalla, kwani Lamu na Somalia ni karibu sana kama si vita hivyo Lamu ingekuwa iko Somalia sio Kenya..

    Sasa tangu Karne ya 16-17 alama hizi nne (4) za majina ya kidigo ziko mpaka leo (1)Dighu-Digo (2) Shmuba-shimba (3)Siti-Tiwi (4) Lughu-Lunga. Ukitoka kwenye kivuko cha Likoni f katikati upande wa magaribi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya kwale kwa wadigo, huko ndido kwenye msitu mkubwa ulio na Kaya kubwa ya wadigo. Uuitoka hapo na kurudi tena kwenye barabara kubwa inayoelekea Tanzania, utaona kijiji. Hapo ndipo mahali ambapo wadigo walipokuwa wakioga wakati vita vya kikabila.

    Na kama wewe si mdigo ni mtu wa bara unataka kuoga hapo huwezi kuona kiti kilichotumiwa wakti wa kuoga na hata nyumba yenyewe ya mzee mwambodze utakayoiona sasa hapo ndio (Tiwi). Ukitoka hapo sasa moja kwa moja mpaka mwisho wa Digo na huko ni mpakani wa Kenya na Tanzania huko ndio kuna mji unaitwa (Lunga) Lakini sisi tunakuita Lunga-Lunga yaani maana yake "uifwate nifwate" yaani wa mijikenda, pokomo na Taita waliwafwata wadigo baada ya kutimuliwa na wagalla.

    Na Dighu- ni jina la Digo walio mashujaa kwa vita dhidi ya waGalla. Sasa mkitembelea Kenya sehemu zote hizi tatu mtajionea wenyewe wa macho yenu hali hiyo

    Pia kwenye mila za wadigo, mtoto akizaliwa kama ni mvulana siku ya kutolewa nje anatengenezewa upinde na mshale wa vijiti, halafu unafungwa juu ya mlango wa hiyo nyumba yao, hiyo ni kushiria yeye ni mchumi akachume chakula alete nyumbani. Na mtoto wa kike (msichana) akitolewa nje anatengenezewa bunda la kuni na kata yake ya vijiti, halafu zinafungwa juu ya mlango wa hiyo nyumba yao, hiyo ni ishara kuwa yeye ni mpishi na mwenye bidii atakwenda kutafuta kuni kuleta nyumbani kumpikia mume wake.

    Kwenye mila za kidigo, mtu akifariki, kuanzia siku ya kufariki familia yake, ndugu na marafiki zake wake kwa waume, watalala chini majamvini au mikekani kwa siku saba nje ya nyumba yake au yao kula na kunywa hapohapo kwa siku zote saba. Na ikiwa aliyefariki alikuwa ni mwanachama wa kifudu (kifudu ni ngoma ya Kidigo inayochezwa baada ya mwanachama kufariki) huchezwa baada ya siku saba za maombolezo halafu ngoma siku saba, lakini huchezwa na watu wenye umri wa zaidi ya miaka 40 kwani nyimbo zake huwa hazina maneno mazuri. Lakini zinaimbwa kidigo na watu wanacheza wakiwa wamesimama na kucheza kwa mduara.

    Halafu baada za hizo siku saba ngoma kwisha nyuma ya nyumba ya huyo marehemu shabiki, kitajengwa kibanda cha makuti matupu halafu vyombo vyote vilivyotumika kwenye ngoma vinawekwa ndani ya hicho kibanda cha hitima bila kutawanywa. Kama wasipofanya hivyo jamaa na familia ya huyo marehemu watapata shida sana siku atakapo kuja kwenye macho yao au kwenye masikio yao na kudai ngoma ya kibanda chake kila siku hadi watakapotimiza hayo yote. Anasema hizi ni baadhi ya mila la kabila la wadigo anazozifahamu yeye.

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-26