Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-28 16:47:16    
Maisha ya Sumuya--Mwanamke hodari wa kabila la wamongolia

cri

    Bi. Sumuya ni naibu mwenyekiti wa baraza la mashauriano ya kisiasa la mji wa Bayanchuoer, mkoa unaojiendesha wa kabila la wamongolia, kaskazini mwa China. Bi Sumuya alizaliwa miaka 55 iliyopita wakati China mpya ilipoasisiwa, katika familia ya wafugaji wa kabila la wamongolia katika wilaya ya Urater.

    Wilaya ya Urater iko katika sehemu ya magharibi ya mkoa unaojiendesha wa kabila la wamongolia. Wakazi wa wilaya hiyo ni wakulima na wafugaji. Wazazi wa bi. Sumuya wote walikufa alipokuwa mtoto mdogo, yeye aliishi pamoja na bibi yake. Inakumbukwa kuwa alipokuwa mdogo, Sumuya alipenda sana kusoma, japokuwa bibi yake alikuwa maskini, lakini serikali ilimpa fursa ya kusoma kwenye shule ya makabila. Alisema :

    "Wakati ule, ili kuwasomesha watoto wa makabila madogomadogo, serikali ya China iliwatuma walimu kwenda nyumbani kwa wafugaji kuwaandikisha watoto, nilipoambiwa umuhimu wa elimu nilimwomba bibi yangu aniruhusu kwenda shule."

    Shule aliyosoma Sumuya ni shule pekee ya maskani yake iliyowaandikisha wanafunzi wa kabila la wahan na wamongolia, gharama zote za shuleni zilikuwa zikilipiwa na serikali, ikiwa ni pamoja na mavazi, chakula, makazi na nauli.

    Baada ya kumaliza masomo ya shule ya msingi, ili kumsaidia bibi yake kutunza familia, msichana Sumuya alipaswa kuacha shule na kurudi nyumbani kuchunga mbuzi. Kutokana na juhudi na uhodari wake, aliteuliwa kuwa mfanyakazi bora na kupelekwa mjini Beijing kwa matembezi, hata alibahatika kuonana na hayati mwenyekiti Mao Zedong.

    Alipokuwa na umri wa miaka zaidi ya 20, Sumuya alichaguliwa kufanya kazi katika serikali ya wilaya, na kushika wadhifa wa uongozi. Aliwahi kushughulikia kazi ya makada na elimu. Rafiki yake Bi. Zhang Guiying anakumbuka kuwa, Sumuya alitilia maanani sana umuhimu wa ujuzi katika ujenzi wa maskani yake, alifanya juhudi kuwabakisha watu wenye ujuzi. Pia alikuwa amefanya kazi nyingi katika kuimarisha kikosi cha walimu na kuboresha hali ya ufundishaji shuleni. Wakati alipokuwa akishughulikia mambo ya elimu, hali ya ufundishaji ya wilaya yake iliinuka kwa haraka, wanafunzi wengi walifaulu mtihani wa kwenda vyuo vikuu.

    Katika miaka 55 iliyopita mabadiliko makubwa yametokea maskani yake. Alipokuwa mtoto, sehemu hiyo kulikuwa hakuna shule ya sekondari, lakini sasa wilaya ya Urater imekuwa na shule zaidi ya 50 za sekondari, na asilimia 80 ya wafugaji wamepata elimu ya sekondari ya chini.

    Bi. Sumuya alisema kuwa, zamani wafugaji walikuwa waliishi maisha ya kuhamahama. Lakini sasa kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya wakazi na mifugo, hali ya mazingira ya kimaumbile ya maskani yake imeharibika sana. Hivyo kuanzia miaka ya 90 ya karne iliyopita, serikali imekuwa ikiwahimiza wafugaji kulisha mifugo kwenye mazizi, ili kuongeza mapato ya wafugaji huku wakihifadhi hali ya mazingira ya viumbe ya mbuga. Bibi Sumuya alisema:

    "Ukanda wetu wa mbuga una ukosefu wa mvua, hivyo lazima tutumie njia za kisayansi ili kustawisha uchumi wetu na kuinua hali ya maisha ya wafugaji."

    Katika mji wa Bayanzhuoer na maskani yake wilaya ya Urater, idadi ya wamongolia siyo kubwa sana, lakini kutokana na sera ya serikali ya kutoa kipaumbele kwa sehemu yenye makabila madogomadogo, limeanzishwa somo la kimongolia kutoka shule za chekechea, msingi, sekondari na hata chuo kikuu. Kituo cha radio na televisheni pia kina vipindi vya lugha ya kimongolia, magazeti na nyaraka za serikali zote zina nakala ya kimongolia, na lugha ya kimongolia inatumiwa sana.

    Bi. Sumuya alisema kuwa, serikali ya huko si kama tu inatilia mkazo kuendeleza elimu ya sehemu ya makabila madogomadogo na kuhifadhi lugha na utamaduni wa kikabila, bali pia inafuatilia kuwateua na kuwaandaa makada wa makabila madogomadogo. Bi Sumuya alianza kufanya kazi katika baraza la mashauriano ya kisiasa ya mji wa Bayanzhuoer miaka 7 iliyopita na kuteuliwa kuwa naibu mwenyekiti miaka 2 baadaye, na kuwa mwanamke mwenye ngazi ya juu kabisa wa kabila la wamongolia katika wilaya yake. Bi Sumuya aliishukuru sana serikali ya China mpya kwa kumuandaa katika maisha yake yote. Alisema:

    "Serikali inatilia maanani sana kutuandaa makada wa makabila madogomadogo, mimi nilikuwa mfugaji nisiyekuwa na ujuzi mwingi, lakini nilichaguliwa kufanya kazi kwenye idara za serikali, na kutoka naibu katibu wa chama wa wilaya hadi sasa kuwa naibu mwenyekiti, kwa jumla nimepelekwa mara saba kusoma katika shule ya chama, masomo hayo yananisaidia sana kazini."

    Baada ya kufanya kazi katika baraza la mashauriano ya kisiasa ya mji wa Bayanzhuoer, Bi. Sumuya alikuwa amefanya uchunguzi mara kwa mara ili kuweza kutoa mapendekezo kuhusu jinsi ya kuboresha hali ya elimu, na kupunguza uharibifu unaosababishwa na ufugaji wa kupita kiasi kwa mazingira ya viumbe ya ukanda wa mbuga.

    Bibi Sumuya mwenye umri wa miaka 55 mwaka huu anakaribia umri wa kustaafu, lakini kila siku anafanya kazi kwa ari kubwa. Alisema kuwa, anathamini sana fursa ya kufanya kazi, nia yake kubwa kabisa kubadilisha sura ya maskani yake kutokana na juhudi zake mwenyewe pamoja na wenzake.

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-28