Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-28 21:37:06    
Mji maarufu unaozalisha bidhaa ndogo ndogo nchini China

cri

    Mji wa Yiwu, ambao uko umbali wa kilomita 200, kusini mwa Hangzhou, mji mkuu wa mkoa wa Zhejiang, ni kituo kimoja maarufu cha usambazaji wa bidhaa nchini China. Mji huo wa ngazi ya wilaya wenye wakazi zaidi ya laki 6, sasa unajulikana nchini na duniani kote kwa uzalishaji wa bidhaa ndogo ndogo na soko la uuzaji wa bidhaa kwa jumla.

    Yiwu ni mji tajiri mkoani Zhejiang na hata katika nchi nzima, ambao wastani wa thamani ya uzalishaji mali wa kila mtu kwa mwaka ni zaidi ya dola za kimarekani 3,000. Katika mji wa Yiwu, kuwepo kwa mamilionea si kitu cha ajabu, magari ya BENZ na BMW yanaonekana kila mahali, na wakazi wengi wa huko wanatumia magari aina ya BUICK na HONDA. Karibu kila mgeni aliyefika Yiwu, anauliza imekuwaje wakazi wa Yiwu wametajirika hivyo?

    Bw. Zhou Weili mwenye umri wa miaka 33 ni mzaliwa wa Yiwu, alikuwa ni mchuuzi anayeuza mapambo ya kichwani ya wanawake baada ya kuhitimu masomo katika sekondari ya juu, lakini baada ya miaka 7 au 8 hivi, sasa amekuwa tajiri mashuhuri mjini humo.

    "Tulianza kuuza mapambo ya kichwani ya wanawake kuanzia mwaka 1995. Mwanzoni tuliagiza bidhaa kutoka miji mingine ikiwemo Guangzhou na Shenzhen. Mwaka 1998, sisi wenyewe tulijenga kiwanda chenye wafanyakazi karibu 200. Mwanzoni duka letu lilikuwa dogo sana, lakini hivi sasa kila mwezi tunasafirisha kontena moja au makontena mawili ya bidhaa kwa zaidi ya nchi 100 za Ulaya, Marekani, Afrika na mashariki ya kati."

    Bw. Zhou Weili alisema kuwa sera za mageuzi na ufunguaji mlango za serikali pamoja na msaada wa serikali ya wilaya zimefanya biashara yao kuwa nzuri. Hivi sasa kiwanda chake kinapanuka hatua kwa hatua, kimekuwa na wasanifu na tovuti ambayo biashara nyingi zinafanyika kwenye mtandao wa Internet.

    "Vitu viwili muhimu katika biashara ya kimataifa ni bidhaa bora na kusafirisha bidhaa katika wakati uliowekwa bila kuchelewa. Hivi sasa bidhaa zetu zinarekebishwa kuendana na desturi na mila za nchi mbalimbali."

    Ili kufanikisha shughuli zake za biashara, Bw. Zhou Weili hivi sasa anajifunza somo la biashara kwa njia ya posta. Mfanyabiashara huyu ambaye hapo zamani alikuwa mkulima, alidokeza lengo biashara yake. Alisema, "lengo linalofuata ni kuendeleza biashara na kujenga matawi yetu katika nchi za nje, na kuingia nchi za Ufaransa na Italia katika miaka mitano ijayo, tunaona kuwa bidhaa zetu zitatuletea faida kubwa huko."

    Ikilinganishwa Bw. Zhou Weili, Bibi Jin Luzhen ambaye alifika Yiwu kujaribu bahati yake baada ya kushindwa katika biashara ya awali, ana mawazo mengi.

    "Watu wanasema kuwa kufanya biashara katika mji wa Yiwu ni rahisi zaidi kuliko sehemu nyingine, hivyo tulifika Yiwu tukitaka kujaribu bahati yetu. Mwanzoni tulikuwa na duka moja dogo sana, tuliwaza kuwa tutaacha biashara yetu kama tukipata hasara. Mwanzoni tulikuwa na wafanyakazi zaidi ya 10 lakini hivi sasa tumekuwa na wafanyakazi zaidi ya 100."

    Bibi Jin Luzhen alisema kuwa bidhaa zao nyingi zinasafirishwa kwenda Russia na Pakistan, na thamani ya bidhaa wanazosafirisha kwa mwaka inafikia kiasi cha Yuan za Renminbi milioni 10. Mafanikio waliyopata katika mji wa Yiwu, yamewaletea mali na maisha mazuri. Bibi Jin alisema kuwa hivi sasa maisha yao yamekuwa mazuri kuliko watu wengi, na pato lake limefikia Yuan zaidi ya milioni moja kwa mwaka, kiasi ambacho ni sawa na dola za kimarekani laki 1.2. Amenunua gari aina ya HONDA, nimeanza kujifunza lugha ya Kiingereza na kompyuta, na sasa anaweza kutumia baadhi ya maneno ya Kiingereza katika biashara na wageni.

    Kabla ya miaka zaidi ya 20 iliyopita, mjini Yiwu kulikuwa na vibanda kadhaa vilivyokuwa vinauza vitu vidogovidogo kama vile vifungo, sindano na nyuzi, lakini hivi sasa mji huo umekuwa mji maarufu sana unaozalisha bidhaa ndogo ndogo nchini China, wakazi wa Yiwu wameendeleza soko lao dogo lilikuwa linauza vitu vidogo vidogo kuwa kituo muhimu cha kusambaza bidhaa kwenda nchi mbalimbali, kitu chochote kinachohitajiwa na watu katika maisha ya kila siku kinapatikana huko. Kila siku idadi ya watu wanaotembelea soko hilo inafikia laki kadhaa, na bidhaa za soko hilo zinasafirishwa kwenda sehemu mbalimbali za nchini pamoja na nchi zaidi ya 120 za mabara matano duniani. Mwaka jana, jumla ya thamani ya biashara iliyofanyika katika soko hilo ilifikia Yuan za Renminbi bilioni 24.

    Kutokana na takwimu, hivi sasa mashirika maarufu zaidi ya 4,000 kutoka nchini na nchi za nje, yameanzisha matawi yao ya biashara, na wafanyabiashara wa kigeni wanaokaa mjini Yiwu kushughulikia ununuzi ni zaidi ya 4,000. Kulikuwa na mtu aliyesema kuwa karibu nusu ya idadi ya wageni wa nchi za nje wanaofika Yiwu kila siku, wanafika kwa ajili ya kununua vitu katika soko la bidhaa ndogo ndogo, wakati zaidi ya 90% ya vyumba vya hoteli za ngazi ya nyota vinapangwa na wateja.

    Watu wanaamini kuwa wakazi wa mji wa Yiwu wataweza kutimiza lengo lao la "Kujenga super Market iliyo kubwa kabisa duniani na mahali pazuri pa kununua vitu duniani"

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-28