Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-28 22:31:56    
Kazi ya China ya kuwasaidia walemavu wenye matatizo ya kiuchumi yapata mafanikio makubwa

cri

    Kazi ya China ya kuwasaidia walemavu wenya matatizo ya kiuchumi imepata mafanikio makubwa. Kazi hiyo yenye mtindo wa kipekee inafanyika kutokana na hali ilivyo nchini China. Katika miaka 20 iliyopita, idadi ya walemavu wenye matatizo ya kiuchumi vijijini nchini China imepungua hadi kufikia milioni 10 kutoka zaidi ya milioni 20, walemavu zaidi ya milioni 2.5 wamepata huduma zinazoweza kuwahakikishia kiwango cha chini kabisa cha maisha; walemavu wanaopata ajira wameongezeka na kufikia zaidi ya asilimia 80 kutoka asilimia 50; watoto walemavu wanaokwenda shule wameongezeka na kufikia asilimia 77 kutoka asilimia 6; na walemavu milioni 9.9 wamepata nafuu kwa kiasi fulani.

    Habari kutoka kwenye mkutano wa kikazi kuhusu kuwasaidia walemavu wenye matatizo ya kiuchumi zinasema kuwa hivi sasa kuna walemavu zaidi ya milioni 60 nchini China, ambayo ni asilimia 5 ya idadi ya watu wote nchini China. Miongoni mwa walemavu hao, walio wengi wana matatizo ya kiuchumi ambao wanachukua theluthi ya idadi ya watu maskini nchini China. Chama cha kikomunisiti cha China na serikali ya China siku zote inazingatia sana kazi ya kuwasaidia walemavu wenye matatizo ya kiuchumi, na kuchukua hutua kuwatatulia matatizo katika uzalishaji na maisha yao. Mpaka sasa, serikali kuu ya China imetenga fedha zaidi ya Yuan bilioni 5 na kuwasaidia walemavu maskini kuondokana na umaskini na kuwapatia mahitaji ya kila siku kupitia kazi zao wenyewe.

    China inashikilia njia ya kuwapatia ajira kuwa njia kuu ya kuondoa umaskini na kuchukua hatua nyingi zikiwa ni pamoja na kupunguza au kufuta kodi kwa mashirika yanayoajiri walemavu wengi na kuchukua sera ya kusukuma mbele maendeleo ya mashirika hayo, na kutoa na kubuni ajira mpya kwa walemavu. Hivi sasa, walemavu zaidi ya milioni 4 wanaoishi mijini wamepata ajira, na walemavu zaidi ya milioni 16.8 vijijini wanafanya shughuli za upandaji miti, ufugaji na sanaa za mikono.

    Hali kadhalika, serikali za sehemu mbalimbali nchini China zimewapa walemavu wenye matatizo ya kiuchumi huduma ya jamii kuwahakikishia kiwango cha chini kabisa cha maisha. Aidha, katika sehemu kadhaa, ruzuku maalum zinatolewa kwa walemavu wasio na ajira, walemavu wasio na uwezo wa kufanya kazi na kwa familia zenye walemavu wengi. Mpaka mwaka 2003, walemavu laki nne na 40 elfu ama walihudumiwa kwa pamoja katika vituo vya walemavu na vituo vya wazee, ama wanaokaa pamoja na familia za kawaida, na walemavu zaidi ya milioni 2.4 walipata misaada ya kiuchumi na huduma.

    Aidha, kutokana na mahitaji ya dharura ya walemavu wenye matatizo ya kiuchumi, shughuli za kuwasaidia watoto wenye ulemavu kwenda shule, kuwatibu walemavu na misaada ya kisheria zinafanyika katika sehemu mbalimbali nchini China. Juhudi kubwa zinafanyika, kuanzisha utaratibu kamili wa kuwasaidia watoto walemavu kupata elimu. Sasa watoto wenye ulemavu elfu 27 wamepewa vitabu bure, watoto walemavu elfu 20 wamekwenda shule na wengine laki kadhaa wamepona kupitia miradi mingi ya kuwasaidia walemavu nchini China.

    Hivi sasa, kuna vituo zaidi ya elfu 40 vya kuwasiliana na watu wanaojitolea kuwasaidia walemavu nchini China, watu milioni 1.86 waliojiandikisha katika vituo hivyo wanawatunza walemavu na kuwapatia ujuzi. Zaidi ya hayo, aina mbalimbali za shughuli za kuwasaidia walemavu zinafanyika katika sehemu mbalimbali nchini China zikiwa ni pamoja na "siku ya kuwasaidia walemavu", "watu wanaojitolea kuwasaidia walemavu" na "vijana chipukizi kuwasaidia walemavu". Mazingira mazuri ya kuwazingatia na kuwasaidia walemavu yanapatikana katika jamii ya China. \

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-28