Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-01 19:33:33    
Maonesho Makubwa ya Utamaduni wa Ufaransa nchini China

cri

    Maonesho makubwa matatu ya utamaduni wa Ufaransa mjini Beijing yanayofanyika hivi sasa kutokana na Mwaka wa Utamaduni wa Ufaransa yanawavutia watazamaji wengi.

    Tokea mwaka 2003 mpaka 2005, nchi mbili China na Ufaransa zinabadilishana kufanya "mwaka wa utamaduni". Kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu maonesho ya "Mwaka wa Utamaduni wa Ufaransa" yalianza kufanyika nchini China. Maonesho makubwa matatu ni shughuli muhimu za mwaka huo wa utamaduni wa Ufaransa. Maonesho hayo ni "Picha Adimu za Rangi ya Mafuta", "Miaka 100 ya Usanifu wa Mitindo Nchini Ufaransa" na "Maisha ya Jenerali Charles de Gaulle". Ingawa maonesho hayo matatu ni ya aina tofauti lakini yote yanaonesha utamaduni mkubwa wa Ufaransa na kuwapatia watu wa China nafasi ya kuielewa zaidi Ufaransa.

    Mwakilishi wa upande wa China wa "Mwaka wa Utamaduni wa China na Ufaransa", ofisa wa Wizara ya Utamaduni ya China Bw. Pu Tong alisema, "Moja ya mada za mwaka huu wa utamaduni wa Ufaransa ni 'Ufaransa, nchi yenye uhuru wa kimawazo na uvumbuzi'. Kwa mada hiyo, Ufaransa inataka kuwafahamisha zaidi watu wa China jinsi nchi hiyo ilivyo na pia nini maana ya uhuru wa kimawazo katika usanifu. Naona watazamaji watapata ufahamu mpya kuhusu maana ya uhuru huo wa Ufaransa."

    Maonesho ya Ufaransa ya picha adimu za rangi ya mafuta yanayofanyika katika Jumba la Maonesho ya Picha la China ni maonesho ya mara ya kwanza nchini China. Picha 51 zimeonesha vilivyo uhodari wa wachoraji mashuhuri wa Ufaransa, na kabla ya hapo Wachina waliweza tu kuziona kwenye kitabu cha picha.

    Katikati ya ukumbi wa jumba hilo imetundikwa picha iliyochorwa na mchoraji mkubwa Edouard Manet "mtoto wa kiume anayepiga filimbi" na picha nyingine 11 za C. Monet na picha maarufu ya "nusu mwili kwa mwanga wa jua" iliyochorwa na Auguste Renoir, picha hizo zinawavutia watazamaji wengi. Picha hizo zinaonesha jinsi picha za rangi ya mafuta zilivyoanza, kuendelea na kubadilika kufikia leo nchini Ufaransa, na mchango mkubwa katika historia ya uchoraji duniani. Jinsi wachoraji walivyokuwa hodari wa kutumia na kutuliza mwangaza mwafaka wa jua ambao unabdilika haraka kwenye picha zao inawashangaza sana watazamaji.

    Inajulikana kwamba uchoraji wa picha za rangi ya mafuta katika karne ya 19 nchini Ufaransa uliathiri kwa kina usanii wa Kimagharibi na hata muziki na fasihi. Makundi ya uchoraji wa aina hiyo yalipokelewa zaidi kuliko aina zote duniani. Lakini kutokana na kuwa uchoraji huo ulivunja desturi za kale na ulikuwa haujali miiko ya dini na maadili ya kale, na ulifuatilia uhalisi wa binadamu na mazingira, uchoraji wa aina hiyo uliwahi kupingwa na kukosolewa. Hata hivyo watangulizi wa uchoraji huo walithubutu kukabiliana na changamoto hiyo na kuionesha katika nyanja ya uchoraji. Uchoraji huo ulijaa uhuru wa kimawazo na uvumbuzi wa mambo. Mmoja katika waandaaji wa maonesho hayo ya picha, mkuu wa Makumbusho ya Orsay mjini Paris Bw. Serge Lemoine alisema, "Sifa walizokuwa nazo kwa pamoja zilikuwa ni kutetea uhuru wa kuvumbua mambo mapya, walikuwa na ujasili wa kuacha asili. Hayo tunaweza kugundua kutoka picha hizo."

    Maonesho yanayofanywa katika Makumbusho ya Taifa ya China, "Miaka 100 ya Usanifu wa Mitindo Nchini Ufaransa" yanaonesha usanifu mkubwa nchini Ufaransa. Katika sehemu yenye eneo karibu mita za mraba elfu nne vitu 220 vya sanaa vimewafumbua macho watazamaji. Tokea usanifu wa mwanzo wa gari mpaka gari la anga ya juu la Renault, na kutoka ndege ya Concorde hadi ndege ya airbus, na tokea miaka ya 20 ya karne iliyopita chupa ya kupashia moto maziwa mpaka nguo yenye simu ya mkononi, na marashi maarufu duniani kote ya Chanel, vyote vimeonesha usanifu hodari wa mambo mabalimbali tokea vitu vya maisha ya kila siku hadi sanaa katika zama za karibuni na za sasa nchini Ufaransa. Mwandaaji wa maonesho hayo naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Uchoraji cha China Bw. Fan Dian alieleza, "Usanifu wa vitu hivyo ni mifano ya usanifu katika karne ya 20. Usanifu huo umeonesha maendeleo ya sayansi na teknolojia na pia utamaduni mkubwa wa kijadi na pia wa kisasa."

    Maonesho mengine katika mji wa Beijing ni "maisha ya Jenerali Charles de Gaulle" yakionesha kiongozi pekee wa kitaifa wa "Ufaransa huru" aliyeongoza askari wake kulinda uhuru wa Ufaransa katika vita ya pili ya dunia na kuwa mkombozi na rais wa jamhuri ya tano ya Ufaransa. Mwaka 1964 de Gaulle alipokuwa madarakani aliitambua Jamhuri ya Watu wa China, na kuifanya Ufaransa kuwa ni nchi kubwa ya kwanza kabisa kuitambua China mpya miongoni mwa nchi za magharibi. Katika maonesho, watazamaji wanafahamu kwa kina zaidi maneno aliyosema kabla ya miaka 40 iliyopita de Gaulle kuwa: "Kuna uwezekano kuwa mioyo katika sehemu mbalimbali duniani mwishowe itaungana kuwa moyo mmoja, nao ni uhuru, usawa na upendo."

    Kwenye ufunguzi wa maonesho hayo, mkuu wa Shirikisho la Urafiki la Watu wa China na Nchi za Nje Bw. Lu Qiutian alisema, "Jenerali de Gaulle ni shujaa wa taifa la Ufaransa, ni moyo wa taifa la Ufaransa. Kutokana maonesho hayo watu wa China wanapata nafasi ya kumkumbuka mtu aliyeweka msingi wa urafiki kati ya China na Ufaransa, na kuelewa kwa kina zaidi utamaduni na historia ya taifa la Ufaransa."

    Wakati China na Ufaransa zinapotimiza miaka 40 ya uhusiano wa kibalozi, maonesho hayo matatu ya "Mwaka wa Utamaduni wa China na Ufaransa" yameleta utamaduni wa Ufaransa mjini Beijing, kitu ambacho ni jambo kubwa katika maisha ya utamaduni mjini Beijing. Kutokana na shauku ya kuelewa utamaduni wa Ufaransa na heshima kubwa kwa Jenarali de Gaulle watamazaji wanajazana katika maonesho. Mmoja wa watazamaji aliyeangalia maonesho yote matatu, Bi. Xie Hailan alisema, "Kama utamaduni wa China, utamaduni wa Ufaransa pia ni mkubwa, lakini kutokana nchi hizo mbili kutengana kwa umbali, hatukuweza kuuelewa moja kwa moja, lakini maonesho hayo yametuwezesha kuuelewa."

Idhaa ya Kiswahili 2004-11-01